Monday , 5 June 2023
Home Kitengo Habari Uchaguzi wa TLS, waibuka na ‘sakata’ la Richmond
HabariSiasaTangulizi

Uchaguzi wa TLS, waibuka na ‘sakata’ la Richmond

Dk. Edward Hoseah, Mgombea Urais TLS
Spread the love

 

KINYANG’ANYIRO cha kuwania urais ndani ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimeibua siri mpya ya “sakata la mkataba tata” wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Corporation Limited (RDC) na Serikali ya Tanzania. Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).

Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi wa TLS, jijini Arusha, leo Alhamisi jioni, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah, ameeleza kuwa tuhuma zote zilizoelekezwa kwake, kuhusiana na suala hilo, hazikuwa za kweli.

“Siyo kwamba najitetea, hapana. Naweza kuthibitisha kuwa sikuwa na tuhuma zozote katika jambo hilo. Na hiyo si kwa maoni yangu, ni maamuzi ya Tume Maalum ya Majaji, iliyoundwa na serikali,” ameeleza.

Amesema, “baada ya Bunge kutoa ripoti yake, ambayo ilimtuhumu yeye kuzembea katika kazi zake za upepelezi, kulinundwa Kamati ya Nidhamu, iliyoshirikisha Tume ya Majaji, ambayo baada ya kumsikiliza, ilimuona kwua hana hatia.”

Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu

Dk. Hoseah alilazimika kutoa ufafanuzi huo, baada ya baadhi ya wajumbe, kumshutumu kuwa alishindwa kuchukua hatua madhubuti, kukabiliana na watuhumiwa wa ufisadi wa Richmond.

Dk. Hoseah ni miongoni mwa wanachama watano wa TLS waliojitosa katika mbio za urais wa chama hicho. Uchaguzi mkuu wa viongozi wa TLS, umepangwa kufanyika kesho Ijumaa, katika ukumbi wa mikutano wa ICC, jijini Arusha.

Wengine wanaowania nafasi hiyo, ni pamoja na aliyewahi kuwa rais wa TLS miaka ya nyuma, Francis Stola; Flaviana Charles,  Shehzada Walli na Albet Msando.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na mkurugenzi mtendaji wa TLS, Kaleb Lameck Gamaya, zoezi la upigaji kura, linatarajiwa kuanza kesho, saa 12 asubuhi. Wagombea wote watano, walipata nafasi ya kunadi sera zao, mbele ya wajumbe wanaokadiriwa kufikia takribani 3000.

Katika uchaguzi huo, Dk. Hoseah, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Flaviana, ambaye aliwahi kuhudumu kwenye nafasi ya Makamu wa Rais wa chama hicho, katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2015.

Flavian anajivunia uzoefu wake wa uongozi ndani ya TLS, huku Dk. Hoseah akijivunia rekodi yake iliyotukuka ya miaka 36 ya utumishi wa umma, kuanzia msaidizi wa aliyekuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri, Francis Nyalali, Hakimu Mkazi, Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara, mkurugenzi wa uchunguzi wa Takukuru hadi mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo.

Baadhi ya mawakili wanaomuunga mkono Dk. Hoseah, ni pamoja na aliyekuwa rais wa TLS na mwanasiasa machachari wa upinzani, Tundu Antipas Lissu; mwanasheria mashuhuri nchini, Prof. Abdallah Safari; Jenerali Ulimwengu, Peter Kibatara, pamoja na mawakili kadhaa maarufu katika mikoa ya Mbeya, Arusha na Mwanza na Dar es Salaam.

Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, aliyeyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina anasema, “lolote linaweza kutokea katika nafasi ya urais.”

Anaongeza, “yoyote kati ya Dk. Hoseah Flaviana anaweza kushinda, ingawa wengi wanamuona Dk. Hoseah kuwa na nafasi kubwa ya kuibuka kidedea.”

Akizungumzia sakata la Richmond, Dk. Hoseah alisema, “usije kuongea Richmond, bila kusoma Hansard (taarifa sahihi za Bunge). Mimi ni mtaalamu wa sheria za ushahidi, kama wewe unajua, tupambane. Sheria inataka usimpeleke mtu mahakamani, kama huna ushahidi wa kuthibitisha kesi yeko bila mashaka.”

Anasema, “kukimbilia mahakamani, bila kuwapo ushahidi, kunamnufaisha mtuhumiwa. Nikiwa mtaalamu wa sheria za ushahidi, nimejiridhisha kuwa kwenye Richmond, hakukuwa na ushahudi wa kutosha wa kupeleka kesi mahakamani.

“Hivyo basi, hata kama walitaka nipeleke kesi mahakamani, lakini nilikuwa nimejiridhisha kuwa hakukuwa na ushahidi, sikuweza kufanya hivyo. Mimi siyo mtu wa kushinikizwa kwa mambo ambayo, nina uhakika hayawezi kusimama mbele ya sheria.”

Dk. Hoseah alitoa kauli hiyo, wakati akijibu swali la Baraka Mbwilo, mmoja wa mawakili vijana ambao ni wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi.

Sakata la Richmond liliibuka bungeni mwaka 2008, kufuatia Bunge kuunda Kamati Teule ya uchunguzi wa mkataba huo. Iliongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe.

Kampuni ya Rchmond, ilijifunga kwenye mkataba na serikali wa kuzalisha megawati 100 za umeme na kisha umeme huo, kuuzwa kwa Tanesco.

Dk. Harrison Mwakyembe,

Mkataba kati ya Richmond na Tanesco, ulifungwa wakati wa utawala wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Aliyekuwa Waziri wake mkuu, Edward Lowassa, alilazimika kujiuzulu kwa kile alichokiita mwenyewe, “vita vya urais wa 2015.”

Dk. Mwakyembe aliwahi kunukuliwa akisema, kilichomponza Lowassa katika Richmond si umiliki, bali akiwa waziri mkuu alishiriki katika kusimamia mchakato wa kampuni hiyo kupewa tenda.

Katika uchunguzi huo, Kamati ya Dk. Mwakyembe, haikuwahi kumhoji Dk. Hoseah wala Lowassa.

Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe, Kamati Teule ilimkwepa kumhoji Lowassa makusudi, kwani walitambua kuwa kwa cheo chake na utendaji wake, angeweza kuathiri matokeo ya kazi ya kamati kabla haijawasilishwa bungeni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Kifo cha mwanafunzi UDOM: Tume yamsafisha naibu waziri

Spread the loveTUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini (THBUB),...

Habari MchanganyikoTangulizi

Bosi NIC apandishwa kizimbani, akabiliwa na mashitaka 365

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar: Bakharesa hajavamia shamba letu

Spread the love  IKULU Visiwani Zanzibar, imeeleza kuwa eneo la kiwanda cha...

Habari za SiasaTangulizi

Zanzibar watangaza rasmi kuwa shamba la Razaba ni mali yao

Spread the love  SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetangaza rasmi kwamba shamba...

error: Content is protected !!