KITENDAWILI kuhusu tarehe rasmi ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini, sasa kimeteguliwa. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Seleman Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ametangaza kuwa tarehe 24 Novemba 2019 ndio siku ya kufanya uchaguzi huo leo tarehe 23 Agosti 2019 jijini Dodoma.
“Kwa mujibu wa kanuni za uchgauzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 ibara ya 4 ibara ndogo ya 1 na 3, waziri mwenye dhamana ya tawala za mitaa na serikali za mitaa anawatangazia umma na vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu kuwa, uchaguzi ni tarehe 24 Novemba 2019,” amesema Jaffo.
Akielezea sehemu ya ratiba ya zoezi hilo, Jaffo amesema upigaji kura utaanza majira ya saa 2.00 asubuhi na kumalizika saa 10 Alasiri.
Amesema, wasimamizi wa uchaguzi watatoa maelekezo ya uchaguzi huo siku 62 kabla ya siku ya uchaguzi, wakati watumishi watakaosimamia zoezi la uandikishaji na uandaaji orodha ya wapiga kura watateuliwa siku 52 kabla ya uchaguzi.
Pia, amesema uandikishaji na uandaaji orodha ya wapiga kura utaanza siku 47 kabla ya uchaguzi siku ya uchaguzi huo ambapo zoezi hilo litafanyika ndani ya siku saba. Fomu za uteuzi zitachukuliwa siku 26 kabla ya siku ya uchaguzi na wahusika watarejesha fomu hizo ndani ya siku saba tangu siku ya kwanza ya kuchukua.
“Ukomo wa madaraka katika nafasi zote zilizogombewa mwaka 2014, viongozi hao watakoma kushika nafasi ya uongozi siku saba kabal ya siku ya wagombea kuchukua fomu ya uteuzi,” amesema Jaffo.
Jaffo amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji na upigaji kura kwa ajili ya kuchagua viongozi bora.
Leave a comment