June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Uchaguzi wa marudio ni kuvunja Katiba’

Spread the love

BAADHI ya wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wamepinga uchaguzi marudio uliopangwa Machi 20, kutokana na kwenda kinyume na sheria na katiba ya Zanzibar. Anaandika Faki Sosi.

Mmoja wa wajumbe hao, Nassor Khamis Mohammed ameeleza hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam amesema kuwa maamuzi ya kurudiwa kwa uchaguzi huo ni kwenda kinyume sheria ya nchi pamoja na kudhulumu haki za Wazanzibari.

Amesema kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salim Jecha amefuta uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, kwa matakwa yake na shinikizo la waliomtuma kutokana na kutoshirikisha wajumbe wa Tume.

Nassor pia ni wakili wa Mahakama Kuu Zanzibar, na mwanasheria aliyewahi kufanya kazi ya uhakimu wa mkoa, na katika mkutano huo uliofanyika Hoteli ya Lambada, Ilala, alifuatana na mjumbe mwingine aitwaye Ayoub Bakar Hamad.

Amesema kitendo cha mwenyekiti wa Tume kuchukua maamuzi bila ya kushirikisha wajumbe wa tume ni ukiukaji wa kifungu na 119(10) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachoeleza kuwa ni lazima uamuzi wa tume uungwe mkono na wajumbe wa Tume.

Amesema kuwa uchaguzi huo haukuwa na dosari kwani wao wajumbe wa ZEC walishuhudia hatua kwa hatua uchaguzi ulivyokwenda na hakukuwa na malalamiko yoyote yaliyotolewa na chama chochote cha siasa.

Alisema sheria ya uchaguzi inaelekeza kuwa wakati wa uchaguzi, yeyote mwenye malalamiko kuhusu taratibu za uchaguzi, anajaza fomu maalum na kuiwasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi.

Amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilifikisha mbele ya Tume malalamiko wakati kura matokeo yakiwa yameanza kutangazwa na Tume lakini hata yalipofuatiliwa kwa majadiliano, yalitupiliwa mbali kutokana na kubainika yamejikita katika uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao ulishakamilika.

Nassor amesema kuna kila dalili zinazoonesha mwenyekiti wa tume alishinikizwa kufuta uchaguzi wote Oktoba 28 mwaka jana, kutokana na aliyoyasema mbele ya wajumbe alipoitisha kikao Novemba mosi.

Siku hiyo, Nassor amesema, Jecha aliomba wajumbe wamuunge mkono kwa maamuzi yake ya kufuta uchaguzi, na kwamba alithubutu kusema kwamba yapo “mazingira ambayo ukifikishwa kusema uongo kwenye Uislamu sio dhambi.”

“Mwenyekiti wa Tume amedhihirisha kuwa anatumika kwa maslahi ya CCM, na kwamba alikuwa mtu mwenye ndimi mbili kwa kuupotosha umma na kwamba muongo hujisahau kwa kutoa matangazo yenye kukinzana ya yale aliyotoa kwenye Gazeti rasmi la Serikali.

Amesema kwenye gazeti hilo alisema amefuta “matokeo ya uchaguzi” na kwenye matangazo mengine amesema amefuta “uchaguzi na matokea yake yote.”

Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ulishakamilika katika ngazi ya uwakilishi na udiwani na walioshinda, walishakabidhiwa hati zao za ushindi.

Amesema anashangazwa na serikali kuitisha uchaguzi wa marudio usio halali kisheria kwa gharama kubwa huku Rais wa Jamhuri ya Muungano akihangaika kuzuia matumizi mabaya ya fedha za umma.

Nchi yenye uchumi mdogo kama Zanzibar alisema haipaswi kuruhusu matumizi ya mabilioni ya fedha za umma kwa uchaguzi ambao tayari ulishakamilika na washindi wa uwakilishi kupata hati zao.

Amesema hali iliopo Zanzibar kwa sasa sio shwari kutokana na kutokuwepo maafikiano ndani ya Tume kwa kuwa baadhi yao hawakubaliani na kufutwa kwa uchaguzi, sembuse kurudiwa.

“Nchi ilipofika imetokana na hatua ya iliyochukuliwa na Mwenyekiti wetu na kwamba tunamshauri ajipime na ajitolee maamuzi magumu ili kuepusha nchi na janga linalonyemelea,” amesema Nassor.

Amependekeza kuwa nchi ifuate matakwa ya katiba ya kutaka mwenyekiti wa Tume awe ni mtu mwenye sifa ya ujaji wa mahakama kuu au mahakama ya rufaa ya nchi yoyote.

“Tunatoa wito kwa wajumbe wenzetu wa Tume ya Uchaguzi kuachana na mchakato wa uchaguzi wa marudio wa 20 Machi kwani jambo hilo halina maslahi kwa nchi yetu,” amesema.

Amesema kutokana na uchaguzi kuhitaji wadau kushirikishwa, vikiwemo vyama vya siasa, mbona Tume haijaita wawakilishi wa vyama kuwaeleza matatizo yaliyosababisha kufutwa uchaguzi na umuhimu wa sasa uchaguzi kurudiwa.

Badala yake ameomba vyama vya siasa vitafute mtu atakayekuwa mpatanishi wa kimataifa ambaye atavitaka vishiriki mazungumzo.

 

error: Content is protected !!