Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Uchaguzi unaoaminika, hauwezi kusimamiwa na wanaotiliwa shaka – Dk. Amani Karume
Habari za SiasaTangulizi

Uchaguzi unaoaminika, hauwezi kusimamiwa na wanaotiliwa shaka – Dk. Amani Karume

Aman Abeid Karume, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Spread the love

 

WIKI mbili zilizopita, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume, alizungumzia kwa kirefu historia ya Mapinduzi Visiwani. Akakumbusha jinsi mwafaka wa mwisho uliozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani (SUK), ulivyofikiwa na sababu za kukwama miafaka miwili iliyopita.

Karume ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, alieleza kuwa baada ya yeye kuingia madarakani, Januari 2001, akajiridhisha kuwa Zanzibar haiwezi kuendelea, ikiwa wananchi wataendelea kunyukana wao kwa wao na tena kila baada ya uchaguzi. Katika makala haya, Dk. Amani Karume anasema yafuatayo:

“Nilikakaa na Mzee Mkapa (Rais Benjamin Mkapa) na kuniambia, ‘Amani tutaendelea hivi mpaka lini? Tunavutana kila siku, hatuwezi tukakaa na tukazungumza.

“Ilikuwa baada ya vurugu za Pemba, ambazo watu kadhaa walipoteza maisha na wengine walikwenda ukimbizi nchini Kenya.

“Tukakutana na wenzetu kutoka Chama cha Wananchi (CUF), kuzungumza. Hapo ndipo tulipoanza mazungumzo yaliyozaa mwafaka wa pili,” anaeleza kiongozi huyo kwa upole.

Anasema, “kumbuka huko nyuma, kulikuwa na mwafaka wa kwanza mwaka 1999, ambao ulitokana na uchaguzi wa mwaka 1995, ambao haukufanikiwa.”

Anasema, kutofanikiwa kwa mwafaka huo, kwa maoni yake, kulitokana na msuluhishi wake alitoka nje.

Mwafaka wa kwanza wa Zanzibar, ulisimamiwa na Chifu Emeke Anyauke, ambaye alikuwa akimwakilisha aliyekuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola (Common Wealth), Dk. Moses Annaf.

Anasema, “mwafaka ule haukufanikiwa kwa sababu, ulisuluhishwa na watu kutoka nje.” Anasema, hata katika familia, ndungu wananaozungumza lugha moja, wenye utamaduni mmoja, mnaoswali misikiti na makanisa hayohayo; na walioleana, hawawezi kusubiri mtu atoke huko kuwasuluhisha.

Anasema, “nadhani ndio maana mwafaka ule haukufanikiwa. Kwa sababu, sio rahisi mjumbe kupeleka ujumbe uliokamilika.  Wakati mwingine, anaweza akaelezwa neno muafaka, lakini akaona huku halifungui milango; akaamua kuingiza lake; kumbe ndio anaharibu kabisa.”

Kwa maoni yake, “njia rahisi ya kujadiliana, ni kukaa mimi na wewe kuzungumza. Wewe unaeleza  ya kwako nakusikiliza vizuri na mimi nitaeleza yangu. Kisha tunatafuta mahali pakuanzia.”

Anasema, katika mazungumzo yaliyozaa mwafaka wa pili, walizungumza wenyewe na mazungumzo yalianzishwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mahasimu wao CUF. Hawakushirikisha mtu ama taasisi kutoka nje.

Alipoulizwa iwapo hilo ndilo lililomsukuma yeye kukutana na Maalim Seif, katika kuelekea mwafaka uliozaa SUK, Dk. Karume anakiri kuwa hiyo ilichangia, ingawa anasema, mkutano wake na Maalim Seif ulikuja baadaye sana.

Anasema, “mimi nilikutana na Maalim Seif baada ya kila kitu kumalizika kwenye kamati za makatibu wakuu wa chama na CCM kuridhia kuwapo kwa maridhiano ya kudumu.”

Anaongeza, “chimbuko lilikuwa ni vyama, makatibu wakuu wetu –  Philiph Mangula (CCM) na Maalim Seif  (CUF) – pamoja na wajumbe wao, walianza kujadiliana mambo mengi ya msingi.

“Walijadiliana reforms yaani marekebisho fulani fulani ya taratibu zetu za utawala. Walizungumza marekebisho ya mfumo wa tume ya uchaguzi, wakatoa mapendekezo yao, sisi tukakubaliana nayo na yote walikuwa wamependekeza ili kuwe na fairness (usawa) kwenye uendeshaji wa uchaguzi.”

Dk. Amani Karume ambaye alikuwa rais wa Zanzibar kutoka mwaka 2000 hadi 2010 anasema, “uchaguzi lazima uwe credible, ili upate fairness lazima wote wawili muelewane na mkubali kwamba utaratibu ni huu.”

Karume anasema, “Maalim na timu yake wakasema, wanalalamikia mahakama kwamba ilikuwa na upande mmoja tu, upo bwana? Lakini vichekesho ni kwamba hata upande huo unaofikiriwa unapendelewa na mahakama, nao wakalalamikia mahakama, kwa hivyo tukakubaliana tufanye marekebisho ya mahakama.

“Tukaunda Judicial Service Commission, hii ikafanya mahakama iwe totally independent kwa sababu hauwezi kuwa na hukumu iliyosahihi kama huna independent of judiciary, judiciary lazima iwe independent body.”

Anataka pendekezo jingine lilikuwa ni kuundwa kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). Kabla ya hapo, kazi ya kwenda mashitaka ilikuwa inafanywa na polisi.

“DPP hapa imo ndani ya katiba ya Zanzibar, anateuliwa na rais. Lakini rais akishamteua anakuwa hana mamlaka ya kumtoa, wala hawezi kumfukuza kazi mpaka amalize muda wake, na hiyo imefanywa ili kumpa nafasi DDP kufanya kazi zake kwa uhuru.

“Tukafanya hayo na mengine. Lililotushinda kufanya kwa wakati ule, ilikuwa hiyo kuundwa kwa Serikali ya pamoja.  Tulishindwa kwa sababu kila jambo lina wakati wake. Kuunda Government of National Unit (GNU), ilikuwa sehemu ya mazungumzo yale. Tukaondoka hapo hilo likiwa halikuwezekana,” anasimulia.

Anasema, “sasa kutokea hapo, tunakaribia uchaguzi, wengine wakapendekeza kwamba tuwe na permanent voter register, tukafanya. Si tunatafuta uchaguzi uwe credible, free and fair (uchaguzi huru, haki na wenye uwazi)?

“Kama watu wako, wapiga kura huwajui, malalamiko yalikuwa wengine wanapiga kura tatu, wengine tano,  sasa si unayaondosha hayo ukiwa na permanent voter  register?

“Hapa Zanzibar tuna kadi zetu za kupiga kura na sote tumekuwa registered (tumesajiliwa humo). Kila mpiga kura ili aweze kupiga kura, ni lazima uwemo humo. Huwezi kupiga kura labda ya uchaguzi wa Rais wa Jmahuri ya Muungano, kama hujasajiliwa humo.

“Kwa uchaguzi wa Zanzibar, lazima uwe na ID (kitambulisho) cha MZanzibar Mkaazi halafu pia uwe na kitambulisho kingine cha kupigia kura. Hilo pia walilipendekeza tukalifanye, tukakubali sisi tukalifanya.

“Lililotushinda ni  National Government of  Unit kwa sababu muda wa uchaguzi ulikuwa unakaribia. Tukaenda kwenye uchaguzi, baada ya kumaliza uchaguzi, Dk. Karume anasema na kuongeza, “umeniuliza swali muhimu,  kwamba ilikuaje ukakutana na Maalim Seif? Nitakwambia.”

Anasema: Baada ya uchaguzi, Rais Mkapa kamaliza muda wake kaingia Rais Jakaya Kikwete, ambako katika hotuba yake ya mwanzo tarehe 30 Desemba bungeni Dodoma, akazungumzia habari ya mpasuko Zanzibar. Akasema, Mpasuko huo unamkosesha usingizi. Akaahidi kuushughulikia.”

“Mimi nikaona ameanzisha mjadala mpya. Wakati huu, Katibu Mkuu wa CCM, ni Yusuph Makamba. Akapewa maelekezo wakutane tena na Maalim Seif ili waendelee na mazungumzo ya ku-heal (ponya) huo mpasuko. Wakakutana Bagamoyo, muda umekwenda sana mpaka walipomaliza.

“Wakati wanazungumza walikuwa wanakuja kutu-brief sisi mpaka wakafika pahala wakatengeneza ile format yenyewe ya mfumo wa GNU utakavyokuwa, mawaziri wanagawana vipi, watatoka vipi.

“Na huo mfumo unaona sasa hivi na Katiba ya Zanzibar, ulijadiliwa huko wakati huo. Baadaye Rais Kikwete akaitisha mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC) Butiama mwaka 2008, tukaenda tukazungumza.

“Katika mazungumzo yale, likatoka agizo kwamba msimamo wetu ndio huu; sasa wenzetu Zanzibar muende mkaunde Serikali ya aina hii.

“Pale kidogo hatukuelewana, baadhi ya wajumbe wakasema ngoja kidogo, mbona tuna harakishana kiasi hicho? Jambo hili ni jipya kwetu na kulipeleka kwa haraka haraka bila kuangalia utaratibu mzuri,  huenda lisifanikiwe.”

Anasema, “tukatoka na msimamo mwingine kule, basi turudi tuje tuzungumze na wananchi kuhusu maamuzi yale, ili tupate kuyafahamu vizuri na halafu tufanye kura ya maoni.”

Anasema, “kwa sababu mimi nilikuwa rais wa Zanzibar, hata na mimi kidogo nilikuwa na mushkeri kuchukua jukumu ambalo linatokana na vyama vichache, katika nchi inayofuata mfumo wa vyama vingi.

“Tukasema, wengine hatujawahusisha na hivyo, tutakuwa tunachukua dhamana kubwa sana na jukumu lenyewe litakua kubwa kwetu, lakini pia maamuzi mazito kama yale ni vizuri tukapata mamlaka kutoka kwa  wananchi wote kwa kuwa hao ndio wengi.

Kwa hiyo, Dk. Karume anasema,  pendekezo lao likawa warudi Zanzibar wakafanye kura ya maoni na ikiwa wananchi wote watakubali, basi ndio wataenda kutekeleza.

“Tukifanya hivyo, itakuwa na sisi tunakosha mikono yetu, pamoja kwamba sisi tayari tumeshaamua, lakini tunatafuta na wengine waliunge mkono isije ikaonekana sisi wasaliti. Likakubalika wazo hilo tukarudi hapa.”

Anasema, “sasa wenzetu unfortunately (kwa habati mbaya), wakasema sasa mnaona? Wakalalamika sana, unaona mnapitisha mambo yenu? Tukaanza tena majadiliano mengine huku muda unakwenda. Ndio hilo likasababisha mimi nikakutana tena na Maalim Seif, kwamba sisi CCM nia yetu sio mbaya.

“Watu walifikiri sisi CCM tunataka kupiga chenga hili jambo ambalo tulishakubaliana. Kwamba,  tulishafanya maamuzi na tumeshapata baraka za chama. Kilichosalia, ilikuwa ni utekelezaji. Basi!

“Wenzetu wale wakatulaumu kwamba baada ya kupokea hayo mapendekezo, tunataka turudi hapa tuwasikilize wananchi wanasemaje. Wakaona tunataka kama kuwapiga chenga, lakini sisi tulichofanya ni kukwamua pale palikokwama. Na huo ndio wajibu wetu.

“Madhali vyama vyetu vimeshatupa mamlaka ya kufanya jambo, mimi nikafanya utaratibu wa kurekebisha sheria sasa ya kura ya maoni Zanzibar. Hapa tulikuwa hatuna sheria hiyo, tukafanya kura ya maoni, matokeo yake majority (wengi) ya wananchi wa Zanzibar wakakubali.”

Amesema, “wananchi wa Zanzibar waliliridhia kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa kuwa wameshachoka malumbano. Hawataki mivutano ya kisiasa isiyokuwa na faida,  wanataka kuendeleza umoja wao, wewe journalist (mwandishi), tembea huko uwaulize wananchi, watakuambia.”

Alipoulizwa anadhani wananchi wa Zanzibar wanafurahia ushirikiano wa Maalim Seif na Dk. Hussein Mwinyi, rais wa sasa wa Zanzibar, rais huyo mstaafu anasema, “exactly. Mambo si ndio hayo.

“Sisi viongozi lazima tuchukue dhamana jamani, tuchukue responsibility. Unapowaongoza wananchi chukua responsibility, kuna maamuzi mengine magumu lazima uyakabili, lakini unayakabili kwa hekima na hekima yenyewe ni kwamba unawashirikisha na wao pia.

“Na sisi hili tulilipendekeza, kwamba tuwashirikishe na wao na ndio maana they are happy. Watu lazima wawe na furaha wakiona viongozi wao wenye msimamo tofauti wa kisiasa, wamekaa pamoja. Kwani tofauti ya kisiasa ni kitu gani? Watu wanabadilisha dini itakuwa misimamo ya kisiasa, ushanifahamu?

“Kipi kikubwa zaidi hapo, dini inayomhusisha Mungu ambayo kuna hukumu siku moja na watu wanabadili kwa sababu ya mapenzi yao. Sembuse siasa? Ni kwamba, tulifanya maamuzi magumu, mazito lakini kwa faida ya wananchi  na leo wananchi wako na furaha.”

Anasema, serikali ya sasa inayoongozwa na Rais Mwinyi, imewapa wananchi wengi wa Zanzibar matumaini makubwa.

“Kwanza, watu wanapenda amani, watu wa Zanzibar wanapenda umoja na mshikamano. Kuvutana vutana, mikwaruzo kwaruzo isiyoisha, hawapendi. Wameshachoka nayo. Hivyo, watu wana matumaini makubwa sana.”

Kuhusu hatua ya Maalim Seif kusita kuingia kwenye serikali, Dk. Karume anasema: “Siwezi nika-coment juu ya kusitasita, kwa sababu sina uhakika wa hilo. Lakini kwa nini haturudi nyuma kwa yale yaliyotokea baada ya kuundwa kwa GNU mara ya kwanza mwaka 2010-2015?

“Walikaa pamoja, walishirikiana waliunda Serikali,  waliendesha pamoja.  Nchi ilitulia, mambo yalikwenda alhamdulilah. Lakini mwaka 2015 hadi 2020, mambo yakabadilika, sasa yalipobadilika wenzetu wapinzani wakakataa, wakakaa kando. Walivyokaa kando basi, hawa walikuwa wako tayari kuendeleza, wakaendesha.”

Alipoulizwa juu ya madai kuwa Seif na chama chake walishinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na baada ya kunyang’anywa ushindi wao, wakaamua kususa, Dk. Karume anasema, “…sasa hilo mimi siwezi kuwajibia. Wanaweza kujibu wenyewe.  Hilo   siyo swali langu, lakini pengine kwa sababu ya imani hiyo, waliamua kukakaa kando, basi sawa.”

Anasema, “lakini ile kukaa kando ni unfortunately (bahati mbaya) kwa maendeleo ya nchi yetu.  Kwa sababu wameiacha hali imekuwa tete sana, hofu imekuja tena,  wengine wanaona tunarudi kulekule.

Kipindi hiki, hivi karibuni nilikuwa nasoma magazeti Rais Mwinyi anasema tena kwa masikitiko, kila alipopagusa anakuta mambo yameharibika. Sasa kama hivyo ndivyo, na mimi naamini ndivyo, tujiulize tulifika vipi hapo?

“Tulifika kwa sababu wale wakosoaji hawakuwepo! Kwa hivyo checks and  balances hazikuwepo. Sasa ndio inavyotakiwa hivyo kuwepo, kwa sababu checks and balances ni muhimu sana. Nilivyosikia Maalim Seif amekubali kuingia katika serikali na kushirikiana na wenzake, mimi nimefurahi sana na mimi nam-respect (namheshimu) sana yule bwana.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!