BAADA ya jana kutangazwa kwa Uchaguzi Mkuu ndani ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Kiomoni Kibamba ametangaza kufunguliwa kwa zoezi la uchukuaji fomu kuanzia kesho tarehe 8 Juni, 2021. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Uchaguzi huo mwaka huu utafanyika Jijini Tanga tarehe 8 Agosti, huku uongozi uliopo sasa chini ya Wallace Karia ukimaliza muda wake katika kipindi cha miaka minne.
Wakili Kibamba amesema kuwa zoezi hilo la uchukuaji fomu litakuwa katika nafasi ya urais pamoja na wajumbe wa kamati tendaji, litakalodumu katika kipindi cha siku tano mpaka tarehe 12 Juni, 2021 na kisha taratibu zingine kufuata.
“Nautangazia umma rasmi kuanzia tarehe 8, tutaanza kutoa fomu za uchaguzi kwa rais na wajumbe wa kamati tendaji, zoezi hili litakuwa kwa siku tano mpaka 12 saa 10 kamili, litakuwa zoezi la kuchukua na kurudisha fomu,” alisema Kibamba.

Mwenyekiti huyo amesema amefungua zoezi hilo kwa matakwa ya kanuni ya 10(1) za uchaguzi za TFF kwa kutakiwa kutoa tangazo siku 60 kabla ya siku ya kupiga kura.
Katika uchaguzi huo nafasi zitakazogombaniwa ni urais ambapo ipo nafasi moja na ujumbe wa kamati tendaji ambapo wanahitajika watu sita.
Kanuni ya 10 kanuni ndogo ya kwanza, ya kanuni za uchaguzi za TFF inaitaka kamati kutoa Tangazo la uchaguzi siku 60 kabla bya siku ya kupiga kura.
Fomu za uchaguzi huo zitatolewa kuanzia kesho kwenye makao makuu ya shirikisho hilo yaliyopo Karume, Ilala jijini Dar es Salaam au kwenye tovuti.
Gharama za fomu kwenye nafasi ya urais itakuwa shilingi 500,000 huku fomu kwa nafasi ya kamati ya utendaji zitatolewa kwa gharama za shilingi 200,000.
Leave a comment