Spread the love

Ni rahisi kutumia sababu za kisheria kusema Tanzania kuna uchaguzi wa nafasi ya Spika wa Bunge. Lakini sio rahisi kueleweka katika utamaduni wa kisiasa kusema kuna uchaguzi wa nafasi tajwa.

Dk. Tulia Ackson ameteuliwa kuwania nafasi ya Spika wa Bunge na chama chake cha CCM kati ya watia nia 71 wa chama hicho.

Uteuzi wa Dk. Tulia ni dhahiri ndiye Spika wa Bunge kuanzia mwaka 2022 – 2025. Na hivyo anapanda ngazi kutoka kuwa Naibu hadi Mkuu wa Bunge.

Kwanza, hakuna namna ambayo atashindwa kwa sababu ni kichekesho kusema ana mshindani ambaye angalau anaweza kupata kura kutoka nusu ya wabunge wa Tanzania… haiwezekani!

Kwahiyo ni kama vile nchi yetu inajitekenya na kuchekelea yenyewe, sababu ni rahisi sana, mazingira yanaonesha hakuna uchaguzi wenye mantiki isipokuwa sheria inadumishwa tu na kusema ‘taratibu’ zilifuatwa.

Pili, asilimia 99 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaundwa na Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hiki ndicho chama tawala nchini Tanzania tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Wakoloni wa Uingereza.

Tatu, haiwezekani wabunge wa CCM wakapingana na chama chao, ili iweje? Wamfurahishe nani? Watake wasitake watamchagua Dk. Tulia ambaye “haijulikani” anagombea au kushindana dhidi ya nani.

Nne, vyanzo vyangu vya taarifa vimeniambia pana makundi mawili; wapo wanaoona kumteua Dk. Tulia ni sawa, na wengine wanaona sio sawa. Lakini wote hawa ni wanachama wenzake wa CCM, hutarajii kuona kinyume, huku mkononi wakijiandaa na mtanange wa 2025.

Ndipo sasa, tunarudi palepale, kwani huu uchaguzi nani na nani wanashindana? Jibu unalo.

Awali nilidhani kuwalaumu wanasiasa wa upinzani kwanini hawazingatii “kugombea” nafasi ya Spika.

Lakini nikakumbuka habari za pimbi, mnyama anayependa kujishughulisha na kujichosha bila manufaa yoyote. Nimewaelewa.

Nani anapenda kujihusisha kwenye uchaguzi wa Bunge lenye mkondo mmoja na ambalo halitampatia kura hata moja.

Hata uchaguzi wenyewe utajikuta unajiuliza sasa hapa akina nani wanashindana na dhidi ya nani na wapigakura wenyewe akina nani?

Ukifika hapo ni bora kutafuta kitabu kizuri cha hadithi ya mapenzi ujisomee au kuburudishwa na vipaji kwenye mashindano ya AFCON 2021 huko Cameroon.

Nimeona namna hiyo. Nimejibu maswali ya wale mlioniuliza kikashani. Asanteni.

Mwandishi wa Makala haya ni Markus Mpangala. Anuanipepe; mawazoni15@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *