May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi Muhambwe, Buhigwe: NEC yawapa neno wagombea, wasimamizi

Spread the love

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, amevitaka vyama vya siasa, wagombea na wasimamizi wa chaguzi ndogo za Buhigwe na Muhambwe, zinazotarajiwa kufanyika kesho Jumapili tarehe 16 Mei 2021, kufuata sheria. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma…(endelea).

Jaji Kaijage ametoa wito huo leo Jumamosi tarehe 15 Mei 2021, baada ya kukagua maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Buhigwe mkoani Kigoma.

“Vyama vya siasa vinavyoshirki katika uchaguzi wa kesho vinaowajibu wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigiwa na  kujumlisha kura. Wajibu wa mawakala ni  kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea,  tume inawakumbusha mawakala na wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni,” amesema Jaji Kaijage.

Kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Jaji Kaijage amesema yanaendelea vizuri.

Buhigwe linafanya uchaguzi mdogo baada ya aliyekuwa mbunge wake (CCM), Dk. Phillip Mpango, kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania. Wakati Muhambwe unafanyika baada ya  aliyekuwa mbunge wake (CCM), Hayati Atashasta Nditiye, kufariki dunia.

Mbali na chaguzi za majimbo hayo, pia kata tano zitafanya uchaguzi siku ya kesho.

Kata hizo ni, Buziku na Bugalana za mkoani Geita. Igunga mkoani Tabora, Miuta (Mtwara) na Ligoma (Ruvuma).

error: Content is protected !!