July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi Mkuu Oktoba 2015 ni 50/50

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva

Spread the love

MADUDU yanayokithiri katika uandikishaji wa Dafta la Wapiga Kura kwa njia ya kielektroniki (BVR) yanauweka Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu njia panda. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Mzunguko wa uandikishaji wa wananchi kwenye daftari hilo umeacha idadi kubwa ya vijana na wanachuo bila kuandikishwa ambapo wachambuzi wa mambo ya kisheria, kisiasa na kijamii wanasema, iwapo kundi hilo litasimama imara na kudai haki hiyo kisheria, Uchaguzi Mkuu hautafanyika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba amesema, pamoja na kuwepo kwa mazingira hasi “hata wakiinuka sisi tutasimama kuhakikisha haki inasimama.”

Mwanaharakati Dk. Bisimba amesema, taarifa za udhaifu wa BVR katika kuandikisha wananchi wamekuwa wakiziripoti kwa maandishi kwenye Ofisi za NEC na kwamba, mazingira magumu kuelekea Uchaguzi Mkuu waliyaona tangu mwanzo.

“Mazingira magumu tuliyaona tangu kura ya maoni, lakini hata katika BVR nako unaweza kujiuliza, inakuwaje mfumo huu wa digital mtu anajiandikisha zaidi ya mara moja?” anahoji Dk. Bisimba na kuongeza kuwa, tayari kuwa watu wameachwa na daftari hilo.

“Kuna shida kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu katika hali hii, kupiga kura ni haki ya kila mtu aliyefikisha umri wa kujiandikisha.

“Haiwezekani kupiga kura kwa wachache halafu wengine wenye sifa za kupiga kura waachwe nje. Daftari la awali nalo halifai, limechaka,” amesema Dk. Bisima na kuongeza “hakika mazingira ni magumu.”

Mwanasheria wa Mahakama Kuu, Mabere Marando ameeleza kuwa, mwelekeo wa kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu upo wazi endapo kundi la watu walioachwa bila kuandikishwa watakwenda mahakamani kuzuia uchaguzi.

Wakili Marando amesema, watu walio na umri wa kupiga kura wanayo haki ya kuzuia uchaguzi huo ‘jambo hili linaweza kufanyika mapema.”

Amesema, “upo uwezekano huu kama kundi moja litajitokeza na kupinga kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mpaka watu waandikishe,” na kuwa hapo Rais aliye madarakani atalazimia kuendelea kuwepo madarakani.

“Katika hilo mimi nitasimama kuwa mwanasheria, wapo watu ambao hawajaandikishwa na daftari linapitishwa juu juu tu. Mazingira yanaelekea huko.”

Hata hivyo, Naibu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (JUKATA), Hebrone Mwakagenda anaonya kuwa, haki ya kupiga kura ikikosekana inaweza kuibuwa matatizo.

Amesema, kwa hali ilivyo ndani ya mfumo wa BVR, nafasi ya kurekebisha makosa ni ndogo sana, “BVR haina nafasi ya kurekebisha makosa haya” na kuongeza kuwa; ‘hili ni tatizo.’

Mwakagenda anasema, hana imani kama uchaguzi Mkuu unaweza kushindikana kutokana na matatizo ya BVR lakini anasema, ni lazima vikwazo vya uandikishaji vikaepukwa ili kuwepo mazingira ya kufanyika uchaguzi huo.

“Kwangu haiwezekani kuacha uchaguzi, kuna matatizo ya hapa na pale na tume (NEC) inapaswa kuhakikisha kuwa lazima kila mtu anayepaswa kujiandisha,” amesema.

Mratibu wa Utetezi wa Haki za Binaadamu, Onesmal Ole Ngurumo anasema, haki ya kupiga kura kwa watu waliotimiza umri ikivunjwa, wana haki ya kuzuia uchaguzi mahakamani “na katika hili tutasimama nao.”

Ngurumo amesema, hatua ya kuzuia uchaguzi mahakamani inaweza kufanywa mapema kwa kuwa haki hii ni ya msingi kwa Watanzania.

Amesema, lipo tatizo hapa na utatuzi wake una ugumu “taasisi yetu kwa kuwa inahusu Haki za Binaadamu, sisi tuko tayari kusimama na kundi ambalo limekosa haki hiyo kufungua kesi mahakamani,” amesema.

Miongoni mwa matatizo makubwa ya BVR ni pamoja na vituo vya kujiandikisha kuwa tofauti na vile vya kupigia kura, mashine za BVR kuondolewa kabla ya watu kujiandikisha, kuharibika mara kwa mara, upungufu wa wataala wa mashine hizo.

Pia mashine zimekuwa zikishindwa kusoma alama za vidole na kumekuwepo na idadi ndogo ya mashine hizo kwenye sehemu iliyo na wakazi wengi kama vile Ilemela mkoani Mwanza.

Hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Dk. Sisti Cariah amekiri kuwepo kwa tatizo la mashine sehemu mbalimbali nchini lililosababisha kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wasioandikishwa katika daftari.

Dk. Cariah alikiri kuwa, kuna tatizo la wanavyuo katika kupiga kura kutokana na kutokuwepo maeneo husika daftari hizo likipita wakati wa uandikishaji na kwamba, ‘waliopo Dar es Salaam wanaweza kufunguliwa dirisha la kujiandikisha na si wa vyuo vya mikoani.’

Hatua ya NEC kukiri kuwepo kwa matatizo ya BVR na hata kusababisha baadhi ya maeneo kushindwa kufikia lengo, kunaelezwa kutoa mwanya kwa malalamiko ya kutofanyika Uchaguzi Mkuu hivyo kumfanya Rais Kikwete kuendelea kuwepo madarakani.

Kutokana na sintofahamu hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba ameitaka kimeingilia kati na kuitaka NEC kuweka hadharani majina ya watu waliojiandikisha.

“Idadi ya watu waliondikishwa katika kila kata ikiwekwa wazi na NEC itasaidia kulinganisha na makadirio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ili kufahamu idadi ya watu wasioandikishwa.”

Wakati Rais Kikwete na NEC ‘wakijiapiza’ kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu, wanaharakati na wachambuzi wanaonesha kuwepo kwa mazingira hasi ya dhamira hiyo.

Mei 3, 2013 Prof. Ibrahim Lipumba amesema, kumekuwepo na njama za Rais Kikwete kuongezewa muda wa kutawala.

error: Content is protected !!