January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi Mkuu Burundi wafanyika kimabavu

Maofisa wa Uchaguzi Burundi wakiwa tayari na vifaa vyao

Spread the love

HATIMAYE uchaguzi mkuu wa Burundi uliopingwa sio tu na wananchi bali nchi mbalimbali, umefanyika siku ya Jumatatu.

Uchaguzi huu una utata kwani haukupata baraka za kimataifa, Umoja wa Afrika (AU), taasisi za kiraia, na wananchi wa Burundi kwa ujumla.

Taasisi za kiraia zimetoa tamko la pamoja kwa kuwataka wananchi kuacha kupiga kura kwa kuuita uchaguzi huo kuwa ni wa unafiki na kuzitaka jumuiya za kimataifa kutotambua uhalali wa uchaguzi huo, huku Umoja wa Ulaya ukitishia kutotoa misaada.

Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), aliitaka Burundi mara kadhaa kuahirisha uchaguzi huo baada ya vyama vya upinzani kusema kuwa vitaususia uchaguzi huo.

Uchaguzi huo haukuungwa mkono na viongozi waandamizi umethibitishwa baada ya baadhi ya viongozi kukimbia nchi kwa kuhofia maisha yao, ikiwa ni pamoja na Spika wa Bunge Pie Ntavyohanyuma aliyekimbia nchi siku moja kabla ya uchaguzi huo, akiungana na warundi wapatao 127,000 waliokimbia nchi tangu Rais Nkurunzinza atangaze kugombea kipindi cha tatu, huku wananchi wapatao 70 wamepopteza maisha yao tangu fujo hizo zianze.

Ntavyohanyuma akizungumza na France 24 siku ya jumapili amesema “Ningependa kumuambia (Nkurunziza) kuwa anachokifanya ni kinyume na katiba . Ninataka afahamu kuwa kulazimisha uchaguzi ni upumbavu.” Amesema Ntavyohanyuma

Mbali na Ntavyohanyuma kuingia mitini viongozi wengine waliokimbia ni Gervais Rufyikiri (makamu wa Rais), maofisa wa tume ya uchaguzi na majaji wa mahakama ya katiba ikiwa ni pamoja na makamu wa Rais wa Mahakama ya Katiba, Sylvère Nimpagaritse aliyekimbia mara baada ya majaji wenzake kulazimishwa kuhalalisha Nkurunzinza kuingia madarakani kwa kipindi cha tatu.

AU siku ya jumapili imetangaza kuwa haitashiriki kama muangalizi wa uchaguzi huo kwani mazingira yanaonyesha kuwa uchaguzi hautakuwa wa huru na haki.

“Baada ya kubaini kuwa na ukiukwaji wa taratibu ili kuleta uchaguzi huru na wa wazi ..AU haitasimamia uchaguzi wa bunge na Rais, kamishina Nkosazana Dlamini-Zuma amesema.

Watu milioni tano wamesajiliwa katika daftari la kura, huku upinzani ukisusia uchaguzi huo wakilalamika kuwa hautakuwa huru.

Vyama hivyo vimesusia kushiriki, hata hivyo Pierre Ndayicariye kamishna wa uchaguzi amedai hajapokea taarifa rasmi kuthibitisha kugoma kwa wapinzani hao.

Katika hatua nyingine Charles Nditije Kiongozi wa upinzani amesisitiza kuwa barua ya kugoma kushiriki uchaguzi imepelekwa kwa Kamishna wa uchaguzi.

Uchaguzi huu unafanyika katika vipindi viwili , uchaguzi wa wabunge ulioanza siku ya Jumatatu wiki hii na uchaguzi wa Rais utakaofanyika julai 15 mwaka huu.

Burundi ilikuwa kwenye machafuko tangia Aprili baada ya Nkurunziza alipoonyesha nia ya kurudi madarakani kwa mara ya tatu kinyume na katiba ya nchi, na hivyo kusababisha machafuko hata kutishia kupinduliwa kwa serikali yake.

Uamuzi huu wa Nkurunzinza na serikali yake ni kinyume cha makubaliano ya amani yaliyowekwa sahihi mwaka 2006 huko Arusha na hivyo kusitisha vita vya miaka 13 ya wenyewe kwa wenyewe.

Makubaliano yaliyovunjwa ilikuwa ni Azimio la Amani la Arusha na moja ya makubalino hayo ni pamoja na uundwaji wa katiba mpya pamoja na mambo mengine inapaswa kuwa na vipindi viwili vya Rais kuwepo madarakani; kuwa na taasisi zenye demokrasia (Bunge na Baraza la mawaziri).

Ikiwa ni pamoja na bunge lenye uwakilishi wa 60% ya wahutu (wanaofanya asimilia 85 ya warundi wote) na watusi watawakilishwa bungeni kwa asilimia 40; uanzishaji wa jeshi la ulinzi na idara ya usalama; uundaji wa baraza litakaloshughulikia utekelezaji wa makubaliano ya mkataba wa Arusha.

error: Content is protected !!