January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi mkuu ACT-Tanzania shakani

Katibu Mkuu wa ACT-Tanzania, Samson Mwigamba akionesha katiba ya chama hicho

Spread the love

HATIMA ya Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania), iko mikononi mwa Jaji Mwandambo wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).

Hii inatokana na Lucas Kadawi Limbu, kufungua shauri la madai Na. 17 la mwaka 2015, dhidi ya Samson Mwigamba na mawakala wake.

Uchaguzi mkuu wa ACT-Tanzania umepangwa kufanyika Machi 29 mwaka huu, lakini Limbu ambaye anajitambulisha kama Mwenyekiti “halali” wa chama hicho, amefungua shauri kujiridhisha kama Mwigamba na wenzake wako madarakani kwa msaada wa Rais Jakaya Kikwete kama wanavyotamba au la.

Anasema “nataka kujiridhisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kama kweli Samson Mwigamba (Katibu Mkuu), Peter Mwambaja (mweka hazina) na Masanga M. Masanga (Mwenezi), wanasaidiwa na Rais Kikwete kuendelea kubaki madarakani wakati ni kinyume cha katiba ya ACT-Tanzania”.

Kwa mujibu wa Limbu, shauri hilo ambalo limefunguliwa tangu  tarehe 30 Januari 2015, limetajwa leo na kuahirishwa hadi tarehe 15 Aprili mwaka huu.

Alipoulizwa kama haoni kwa tarehe hiyo tayari ACT-Tanzania itakuwa imemaliza uchaguzi wake, Limbu amesema, “sisi hatukutaka kuweka pingamizi kuzuia uchaguzi huo ambao sio halali, isipokuwa tumemwachia Jaji atumie busara yake”.

Limbu anasisitiza kwamba, hata Jaji Mwandambo akiacha uchaguzi huo ufanyike, bado hatua hiyo itakuwa sawa na kazi bure kwani itakapobainika huko mbele kuwa Mwigamba hawakuwa viongozi halali, hawataweza kulalamika kwamba walipoteza fedha.

“Mimi ndiye mwenyekiti halali wa ACT-Tanzania, hakuna mtu wala kikao kilichokaa na kuniondoa, hizo mbwembwe za msajili wa vyama kwamba anawatambua Mwigamba na wenzake ni za kuwaridhisha tu.

Amefafanua kuwa inashangaza kuona msajili wa vyama anadai kumtambua Mwigamba na wenzake ilhali walikwitangaza kujiuzulu tangu tarehe 5 Desemba 2014 katika Kamati Kuu.

“Sasa watu hao hao wanawezaje kuitisha kikao cha Sekretarieti tarehe 23 Desemba 2014 na ‘kujipachika’ madaraka ya kunisimamisha halafu eti tarehe 10 Februari 2015, msajili anatoa barua ya kutambua maamuzi yao.

“Yaani tarehe 16 Februari 2015, msajili ametoa barua nyingine ya kutangaza kuniengua kwenye Baraza la Vyama vya siasa. Hapa ndipo nataka kufahamu nani yuko nyuma ya ufisadi huu. ACT walikaa lini kunifukuza na kupelekea taarifa kwa msajili,” anahoji.

Limbu ambaye anashirikiana na Leopord Mahona na Greson Nyakarungu katika shauri lake, amesema kuwa uchaguzi ulioitishwa na wakina Mwigamba sio halali kwa mujibu wa katiba.

ACT-Tanzania ambayo iko mbioni kumpokea Zitto Kabwe ambaye ametimuliwa uanachama na chama chake cha Chadema, imekuwa kwenye msuguano wa uongozi baina ya waanzilishi na wananchama waliojiunga baadaye.

Desemba 31, mwaka jana, Kamati Maalum ya ACT-Tanzania, ilipitisha kwa pamoja azimio la kuwafukuza kutoka ndani ya chama hicho, viongozi wake watatu wajuu, Samson Mwigamba, Prof. Kitila Mkumbo, mjumbe wa kamati kuu (CC) na Shaban Mambo, Makamu mwenyekiti Bara, huku Zitto Kabwe akitajwa kuwa sababu ya kutimuliwa kwao.

Akisoma azimio la kufukuzwa viongozi hao, Mwenyekiti  Limbu alisema, Prof. Kitila na Mwigamba wamevuliwa uwanachama kwa kosa la kuanzisha chama kipya ndani ya chama cha sasa.

Limbu amesema, Kitila na Mwigamba wamethibitika kupeleka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa katiba mpya ya ACT, kisha kuisambaza mikoani, kinyume na katiba iliyopo ya chama hicho; kuchapisha bendera mpya, kadi na nembo.

Aidha, Prof. Kitila na Mwigamba wanatuhumiwa kupokea fedha kutoka kusikukojulikana, ikiwa ni sehemu ya mabilioni ya shilingi yaliyokwapuliwa kutoka Akaunti ya Escrow.

Vilevile, Prof. Kitila na Mwigamba wamefukuzwa uwanachama wa chama hicho kwa kukiri kukiingiza katika mkataba wa uendeshaji na kampuni ya kigeni kutoka Senegal na bila chama kufahamishwa.

Taarifa zinasema, mbali na makosa hayo, Prof. Kitila na Mwigamba wamefukuzwa katika chama, kutokana na kushiriki maandalizi ya kufanya “mapinduzi” ya kumwondoa mwenyekiti wa sasa Limbu ili Zitto Kabwe aweze kushika usukani wa chama hicho.

error: Content is protected !!