May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi Buhigwe, Muhambwe: ACT-Wazalendo yakubali kushindwa

Spread the love

 

LICHA ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutotangaza matokeo rasmi ya chaguzi mdogo wa Ubunge wa Buhigwe na Muhambwe, mkoani Kigoma, Chama cha ACT-Wazalendo, kimekipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kutwaa majimbo hayo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma … (endelea).

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo Jumapili tarehe 16 Mei 2021, ACT-Wazalendo kilichuana vikali na CCM, ambapo wagombea wao walikuwa; Jimbo la Muhambwe Dk. Florence Samizi (CCM) na Julius Masabo (ACT-Wazalendo) na Buhigwe waliogombea, Galula Kudra (ACT-Wazalendo) na Mwalimu Eliadory Kavejuru (CCM) .

Baada ya uchaguzi huo kumalizika, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amekipongeza CCM kwa kushinda katika Jimbo la Muhambwe, huku akiwapongeza wasimamizi wa uchaguzi huo.

 

“Nawapongeza CCM kwa ushindi wa halali kabisa Jimbo la Muhambwe. Kila la Kheri kwa Mbunge mpya. Tutakutana Uchaguzi unaofuata tukiwa Imara zaidi.”

“Nampongeza Msimamizi wa Uchaguzi wa Muhambwe na OCD wa Kibondo kwa kufanya kazi kwa weledi. Ninalaani matukio ya kuumiza watu yaliyotokea,” ameandika Zitto katika ukurasa wake wa Twitter.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo amesema, kwa mujibu wa matokeo yaliyokusanywa na mawakala wa chama hicho, mgombea wao katika Jimbo la Muhambwe amepata asilimia 41 ya kura.

“Tumekusanya matokeo ya uchaguzi katika vituo vyote 336 vya kupigia kura Jimbo la Muhambwe. Kura zetu, 41% ya kura zote, haziwezi kutupa Ushindi. Uchaguzi uliendeshwa vizuri. Kasoro kadhaa zilizojitokeza zisingebadili matokeo. Tunatumia uchaguzi huu kama Mafunzo kujiimarisha zaidi,” ameandika Zitto.

Naye aliyekuwa mgombea wa ACT-Wazalendo Muhambwe, Masabo kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika “A Fairly Win to the CCM (ushindi halali kwa CCM) Uhambweni.”

Kuhusu uchaguzi wa Muhambwe, Zitto amedai mchakato wake ulikuwa na dosari, hivyo chama chake kimepata funzo.

“Kwa upande wa Jimbo la Buhigwe, uchaguzi ulivurugwa. Matendo yale yale yaliyofanywa katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 Ndio yamefanywa Mwaka huu Buhigwe. Tuna mafunzo tumepata katika kuendelea kujenga chama chetu Kwa ajili ya chaguzi zijazo,” ameandika Zitto.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Shaka Hamdu Shaka, amesema chaguzi hizo hazikuwa na dosari zozote, bali ACT-Wazalendo kimeshindwa kutokana na kushindwa kujiandaa vyema na kushiriki chaguzi hizo.

“Chama chake kimeshindwa kuingiza timu uwanjani iliyojiandaa vizuri, sisi tumejiandaa muda mrefu na wagombea wetu wanakubalika bila shaka yoyote” amesema Shaka.

Chaguzi hizo ndogo zimeitishwa na NEC, baada ya aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe, Atashatsta Nditiye, kufariki dunia, na aliyekuwa Mbunge wa Buhigwe, Dk. Philip Mpango, kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

error: Content is protected !!