October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi 2020: Membe aungana na wapinzani kuiangamiza CCM

Spread the love

BERNARD Membe, Waziri wa Mambo ya Nje Mstaafu, ameungana na hoja ya wapinzani ya kudai Tume Huru ya Uchaguzi, itakayowezesha Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba 2020, kuwa wa huru na haki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, jana tarehe 18 Machi 2020, Membe amesema anaunga mkono harakati za kudai Tume Huru ya Uchaguzi.

Mwanadiplomasia huyo amedai kuwa, mazingira ya kisiasa yaliyopo nchini yanahitaji tume ya uchaguzi inayojitegemea, na kutekeleza wajibu wake kwa uwazi katika ngazi zote.

Membe aliyefukuzwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa kosa la utovu wa nidhamu hivi karibuni, amesema hata alipohojiwa na Kamati ya Maadili  juu ya tuhuma zilizokuwa zinamkabili, alizungumzia kuhusu umuhimu wa upatikanaji wa tume hiyo.

“Nilisema katika kamati ya maadili na wacha niseme tena, mazingira ya kisiasa yaliyopo yanahitaji tume ya uchaguzi ambayo ni ya kujitegemea, yenye uwazi katika ngazi zote za kitaifa na wilaya. Kwa hiyo ninaunga mkono sauti zote kuhusu suala hilo,” ameandika Membe katika ukurasa wake wa Twitter.

Wimbo wa upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais, wabunge na madiwani mwezi Oktoba mwaka huu, umekuwa ukiimbwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani.

Ambapo Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alielekeza viongozi wa chama hicho katika ngazi zote, kuanza mikutano ya hadhara kwa ajili ya kudai tume hiyo, ifikapo tarehe 4 Aprili 2020.

Wakati akizungumza na wanahabari hivi karibuni, Mbowe alisema watafanya mikutano hiyo hata  kama mamlaka zitawazuia kufanya hivyo.

Hata hivyo, serikali imepiga marufuku shughuli zenye asili ya mikusanyiko ya watu wengi kwa muda wa siku 30, kuanzia tarehe 17 Machi hadi 17 Aprili 2020, ili kudhibiti ueneaji wa Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu, inayosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19).

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),katika nyakati tofauti waliiomba serikali kuhakikisha uchaguzi huo unakua huru na wa haki.

Kelele za wapinzani hao juu ya upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi, au mchakato wa uchaguzi huo kuwa huru, haki na wa uwazi zimeibuka kwa madai kwamba, vyombo vya usimamizi wa masuala ya uchaguzi vinakibeba chama cha CCM.

error: Content is protected !!