January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ubunge waipasua CCM Bukoba Vijijini

Spread the love

BAADA ya mgogoro kati ya Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki na aliyekuwa Meya wa Manispaa hiyo, Dk. Anatory Amani, kukiathiri Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hivyo kufanya vibaya katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana, sasa mgogoro mwingine unakinyemelea chama hicho wilayani Bukoba Vijijini. 

Mgogoro huo ni sawa na wajenzi wanaojenga nyumba moja, halafu wanagombea fito. Chama kimoja wanachama wake wanapambana kugombania kiti cha ubunge ambao sasa unashikiliwa na Jason Rweikiza. Anaandika Ashura Jumapili(endelea).

Rweikiza ananyukana na Nazir Karamagi katika vita hiyo. Itakumbukwa kuwa katika kura za maoni ndani ya CCM 2010, Karamagi-aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo 2005/2010, alidondoshwa na Rweikiza.

Vita ya wawili hawa sasa imekigawa chama chao katika halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini. Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Kapten mstaafu Dauda Kateme, ameingizwa katika mgogoro huo.

Rweikiza na Karamagi ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).

Viongozi hawa tayari wameshakuwa kwenye mnyukano na kujitangaza waziwazi kuwa wanataka kuwania ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Mfarakano huo pia umewagawa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba Vijijini, Novatus Nkwama na Katibu wake, Maulid Acheni.

Sio hao pekee, bali hata Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) wilayani humo, Katibu Frate Mrema na Mwenyekiti wake, Avit Barongo wanavutana kuhusu uamuzi wa kikanuni na katiba yao.

Hivi karibuni kumetokea mgawanyiko wa vijana hao wakitofautiana kuhusu mahala pa kuweka kambi kwa lengo la maboresho ya kuwaandaa kisiasa na kiitikadi.

Inadokeza kuwa vijana wanaomuunga mkono Rweikiza, walitaka kambi hiyo iwekwe shuleni kwake Kata ya Kanyengereko wakati wale wanaomtaka Karamagi, walipendekeza iwe katika shule ya msingi Nyakibimbili tarafa ya Rubale. 

Nicholas Basimaki ni mmoja kati ya vijana wa UVCCM, ambaye alihojiwa na kusema “hali ya  makundi ndani ya CCM inaweza kusababisha baadhi ya wananchama kukisaliti kutokana na migogoro isiyokuwa na tija.”

Kijana huyu amewahi kugommbea uwenyekiti wa UVCCM wilayani humo mwaka 2012, ambapo kuhusu kambi hizo anasema kwa mtazamo wa kisiasa, kutokuelewana kwa viongozi kunasababishwa na wao wenyewe.

“Wakati wa uchaguzi kuna baadhi ya viongozi wanaokuwa madarakani na wengine wanahitaji kuingia kusaka maslahi,”anasema Basimaki.

Katibu wa UVCCM Wilaya ya Bukoba Vijijini, Frate Mrema, anasema umoja huo una kanuni zake na taratibu. Kwamba, kikao cha kwanza cha maandalizi ya kambi ya vijana wao kilifanyika na kuwakutanisha makatibu kata zote za jimbo hilo.

Anasema katika kikao hicho, makatibu 27 walipendekeza kambi ya vijana kuwekwa kata ya Nyakibimbili lakini katibu kata wa Kemondo, alipendekeza kambi hiyo iwekwe Kemondo na kuhudhuriwa na wajumbe 28.

“Kikao cha pili kilikuwa cha kamati ya utekelezaji ya vijana wilaya, miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ilikuwa kuhusu kambi. Wajumbe wa kikao hicho walikubaliana ipelekwe Nyakibimbili lakini mwenyekiti wa UVCCM, Maulid Acheni alisema ipelekwe kata ya Kanyengereko shuleni kwa Rweikiza.

“Kauli hiyo ilipingwa na wajumbe na kumtaka kuheshimu maamuzi ya watendaji wa kata wa umoja huo na muafaka haukupatikana, ndipo mwenyekiti akawaomba wajumbe kuwa atatoa jibu kuhusu kambi itawekwa wapi baada ya kuwasiliana na Rweikiza,” anasema. 

Mrema anaongeza kuwa, tangu siku hiyo, mwenyekiti hakurudi tena ofisini wala kutoa mrejesho wa mazungumzo yake na mbunge. Kwamba baadaye alipita kila kata akiwa na gari la Rweikiza na kutoa mialiko ya  kambi kuanza akisema itafanyikia Kiizi kata Kanyengereko.

“Nilipata taarifa za mwenyekiti wangu kutoa mialiko kwa njia ya simu kutoka kwa makatibu kata, wakinituhumu kubadilisha uamuzi wao wa kwenda Nyakibimbili.

“Lakini niliwajulisha kuwa maamuzi yao hayatenguliwa, kambi itafanyika Nyakibimbili na ya pili ni batili, haikufuata taratibu,”aliongeza Mrema. 

Kwa mujibu wa Mrema, vijana waliamua kuchagua kata ya Nyakibimbili ili kuepuka makundi ya wanasiasa wanayoyajua wao ili kila kiongozi wa chama awe huru kwenda kuwaona kuliko kuegemea upande fulani. 

Mrema anasema “sijui mwenyekiti wangu alihaidiwa nini na mfadhili wake (mbunge), maana hata usafiri wa gari alipewa siku mbili akizunguka kuhamasisha vijana kwenda Kanyengereko kabla ya kikao.”

Julius Rweyemamu- mkazi  wa Kata  ya Kemondo, anasema mgogoro uliopo ndani ya CCM umeanza kuleta madhara  kwa wakazi  wa jimbo hilo kwa kile kinachodaiwa kuhujumiwa kwa baadhi ya miradi ya maendeleo waliyoiibua.

Anasema kuwa wananchi wa Kemondo waliamua kubuni mradi wa ujenzi wa shule ya msingi Mujureki kwa sababu eneo hilo liko mbali na shule, lengo likiwa kusogeza elimu karibu na watoto. 

Anasema “licha ya kipato chetu kuwa kidogo lakini tulijinyima na kununua kiwanja pia tulikusanya vifaa vya ujenzi na halmashauri kutoa stakabadhi za kukusanya michango”.

“Hata hivyo, mradi huo ulihujumiwa, tulielezwa kuwa ujenzi huo umesimamishwa ukiwa katika hatua ya kuezekwa  kwa madai kwamba, eneo hilo  halifai kwa ujenzi. Jambo hili lilihuzunisha juhudi za wananchi  kwa  kuwa ujenzi huo umeishatumia Sh.18 milioni,”anasema Rweyemamu.

error: Content is protected !!