January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ubomoaji jengo la ghorofa 16 wawekwa kiporo

Spread the love

UBOMOAJI wa jengo la ghorofa 16 lililopo Mtaa wa Indira Gandhi, Posta – Dar es Salaam utaanza rasmi baada ya kampuni iliyopewa dhamana ya kubomoa jengo hilo kusaini mkataba. Anaandika Regina Mkonde … (endelea).

Kampuni iliyopewa dhamana hiyo inaitwa Patty Interplan Ltd ambapo inatarajiwa kulipwa gharama za ubomoaji huo kutoka katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Akizungumza na MwanaHalisi Online msemaji wa kampuni hiyo Mhandisi Swithurn Mgaya amesema kuwa, taratibu za ubomoaji jengo hilo zitaanza ramsi pindi kampuni yake itakaposaini mkataba wa ubomoaji na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

“Tuko kwenye maandalizi ya ubomoaji, hatujaanza kubomoa kama ilivyosemwa na baadhi ya vyombo vya habari sababu wahandisi wanasubiri manispaa kufanya mkataba wa kubomoa na Kampuni ya Patty Interplan Ltd iliyopewa dhamana ya kubomoa jengo hili.

“Nafikiri ifikapo mchana mkataba huo utasainiwa kwa kuwa baadhi ya viongozi wa manispaa walikuja leo kuangalia mandhari ya jengo ili watupe maelekezo,” amesema Mgaya.

Manispaa ya Ilala itakapofanya mkataba na kampuni hiyo, inatarajiwa siku chache zijazo ubomoaji kuanza baada ya maandalizi ya ufungwaji wa vyuma maalum vinavyozunguka jengo ili kukinga vifaa visitoke nje ya jengo na kujeruhi watu pamoja na kuharibu mali za watu waliokaribu na jengo hilo yatakapo malizika.

Hatua ya ubomoaji jengo ilifikiwa baada ya tamko la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alilolitoa mwezi uliopita la kuitaka Manispaa ya Ilala ndani ya siku 18 baada ya tamko hilo kutolewa, kubomoa jengo hilo ambalo ujenzi wake haukufuata sheria na taratibu za ujenzi jambo linalohatarisha usalama wa watu vilevile kukwepa ajali za kubomoka majengo kama ilivyotokea ajali ya jengo lililopo karibu nalo lililobomoka mwaka 2013 na kuua pamoja na kujeruhi watu.

Kwa mujibu wa wafanyakazi wa kampuni ya Patty Interplan Ltd walisema kuwa, jengo hilo halikujengwa kwa kufuata sheria na kanuni za ujenzi vilevile vifaa vilivyotumika vilikuwa hafifu kitendo kinachochangia majengo mengi kutokuwa imara na kubomoka.

“Jengo limejengwa kwa nondo kuanzia chini hadi juu, kwa jengo kama hili lenye ghorofa nyingi lilitakiwa kujengwa kwa nondo kubwa chini halafu juu ndiyo nondo ndogo zitumike, kama unavyoona vifaa vilivyotumika hafifu ndiyo maana limesanza kuweka nyufa kabla ya kuisha, zege lililotumika kujenga ngazi simenti yake haikuwa kali,” amesema mfanyakazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Masoud.

error: Content is protected !!