UBALOZI wa Marekani nchini Tanzania umetoa tamko la kulaani tukio la kushambuliwa kwa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na watu wasiojulikana, lililotokea usiku wa kuamkia jana Jumanne tarehe 9 Juni 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Tukio hilo lilitokea nyumbani kwa Mbowe, maeneo ya Area D Dodoma, ambapo watu hao wasiojulikana walimpiga na kumsababishia majeraha mwilini, pamoja na kuuvunja mguu wake wa kulia.
Kwa sasa Mbowe anatibiwa majeraha hayo katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam, alikohamishiwa jana akitokea Hospitali ya DCMCT Ntyuka jijini Dodoma, alikokimbizwa baada ya kujeruhiwa.
Kufuatia tukio hilo ambalo Chadema linadai linatokana na sababu za kisiasa, Ubalozi wa Marekani umetoa wito kwa mamlaka husika, kufanya uchunguzi wa kina na huru mapema, kwa ajili ya kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua haraka.
Ubalozi wa Marekani umetoa wito huo jana tarehe 9 Juni 2020, kupitia tamko lake ililotoa katika ukurasa wake wa Twitter.
“Ubalozi unatoa wito wa kufanyika haraka kwa uchunguzi wa kina na huru na kisha kukamatwa na kushtakiwa kwa wale wote waliohusika katika shambulio hilo,” inaeleza taarifa ya ubalozi huo.
Chadema katika nyakati tofauti kupitia viongozi wake, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema na John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema, wakati wakizungumzia tukio hilo, walidai linatokana na sababu za kisiasa.
Viongozi hao wa Chadema walidai, tukio la kushambuliwa kwa Mbowe ni mfululizo wa viongozi wa vyama vya upinzani kunyanyaswa, ili kuwaziba midomo pamoja na kusitisha harakati zao.
Ubalozi wa Marekani kupitia tamko lake hilo, nao pia umedai kwamba tukio hilo ni mlolongo wa matukio ya utumiaji nguvu na unyanyasaji yanayofanywa dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani.
“Ubalozi unaliona tukio hili katili na lisilo na sababu la kuvamiwa kwa kiongozi wa upinzani kama tukio la hivi karibuni katika mlolongo mrefu wa matukio ya kusikitisha ya utumiaji nguvu nba unyanyasaji yanayofanywa dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani,” inaeleza taarifa ya ubalozi huo.
Ubalozi wa Marekani umefananisha tukio hilo na tukio la kushambuliwa na risasi Lissu, lililotokea tarehe 7 Septemba 2017, jijini Dodoma.
“Ubalozi unatambua mojawapo ya matukio haya ya kikatili ni jaribio la mauaji lililotokea dhidi ya mbunge na kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, ambalo ufumbuzi wake haujapatikana hadi leo.”
“Kwa mara nyingine, tunatoa wito kwa vyombo husika kuwabaini, kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wale wote waliohusika na tukio hilo,” inaeleza taarifa ya ubalozi huo.
Aidha, Ubalozi wa Marekani umetoa pole kwa Mbowe na familia yake kufuatia kadhia hiyo, ambayo imewaweka katika kipindi kigumu, na kumtakia apone haraka.
Leave a comment