August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ubadhirifu Bil 4.5 wamtibua Maswi

Eliakim Maswi, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Mji wa Babati

Spread the love

ELIAKIM Maswi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, ameeleza kuwepo kwa ubadhirifu wa Sh. 4.5 Bil, katika Halmashauri ya Mji wa Babati, anaandika Dany Tibason.

Ni fedha zilizotolewa kwa wananchi kwa ajili ya mikopo ya viwanja pamoja na ulipaji wa fidia. 

Amesema, kufuatia hali hiyo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wanaendelea na uchunguzi kwa kuwahoji watendaji mbalimbali waliohusika na  ubadhirifu huo ili waweze kuchukuliwa hatua stahiki.

Ametoa kauli hiyo katika Ukumbi wa Bunge wa Msekwa mjini Dodoma leo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), wakati wa mahojiano na halmashauri hiyo.

Maswi ameeleza kuwa, ubadhilifu ni mkubwa ambapo inafikia bilioni 4.5, na kwamba ni tofauti na ilivyoelezwa awali kwamba ubadhirifu ulikuwa chini ya Sh. 1 Bil kwenye kitabu cha taarifa za halmashauri kilichokabidhiwa kwa LAAC.

“Mheshimiwa mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Babati, ilikuwa na wizi mkubwa wa fedha za viwanja ambazo wananchi wamelipia na mpaka sasa hawajapewa viwanja na fedha zimeliwa, wapo waliostahili kulipwa fidia baada ya ardhi yao kutwaliwa na halmashauri nao hawajalipwa,”amesema.

Katibu Tawala huyo amethibitisha kuwa, ndani ya halamshauri hiyo kumetawala vilio kutoka kwa wananchi.
Amesema, kuna maeneo matano yanayohusu ubadhirifu huo wa ardhi ambapo wananchi wanateseka, baada ya Takukuru kumaliza kazi yake hatua za kisheria zitachukuliwa na hakuna atakayevumiliwa.

Kibiki Mohammed, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo amekiri kuwepo na tatizo hilo na kwamba, uchunguzi unaendelea.

Hoja hiyo iliibuliwa na Edward Mwalongo, Mbunge wa Njombe Kusini (CCM) ambaye ni mjumbe wa kamati ya LAAC, ambaye alihoji ni kwanini halmashauri inadaiwa fedha za viwanja zaidi ya Sh. 1 Bil.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Leah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum (CCM)  huku akisema, kuna haja halmashauri hiyo kuangaliwa vizuri katika matumizi yao ya fedha wanazokusanya.

Abdallah Chikota, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema, halmashauri hiyo haijafanya vizuri katika eneo la ardhi.
“Serikali imekataza kutwaa ardhi ya wananchi bila kuwalipa fidia, sasa mnajifanya mnaviwanja vingi na mtaviuza, nyie hamna ardhi kama halmashauri, ardhi ni ya wananchi nyie tafuteni fedha muwalipe wananchi ndio mtwae ardhi zao,” amesema.

Vedastus Ngombali, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ameshangazwa na mtindo wa utafunaji fedha unaofanywa na watendaji wa halmashauri hiyo, huku wao wakijitetea kuwa, wote ni wageni na wengine wanakaimu.

 

error: Content is protected !!