January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ubabe unaitwa ni ujasiri, udhaifu huitwa uungwana!

Naibu Spika Job Ndugai

Job Ndugai, Spika wa Bunge

Spread the love

SIKUONEKANA wiki iliyopita. Nilikuwa mjini Dodoma kushuhudia mjadala wa muswada wa marekebisho ya sheria ya katiba mpya. Kwa bahati mbaya nimeishia kusikiliza vijembe, matusi, mipasho na hatimaye ngumi.

Wabunge wa upinzani wakiongozwa na wa Chama cha Wananchi (CUF) walitoka nje ya ukumbi wa Bunge kupinga upendeleo wa wazi uliokuwa unaonyeshwa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Huku nyuma wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakabaki wanawajadili wabunge wa upinzani badala ya kujadili muswada wenyewe. Nilidhani mnadhimu mkuu wa CCM na serikali bungeni, William Luvuki angesimama na kuomba mwongozo wa naibu spika ili kuurejesha mjadala mahala pake, lakini haikutokea.

Nilibaki nimeduwaa mpaka muda wa kuchapisha gazeti la wiki iliyopita ukapita, nikarudi Dar es Salaam nikiwa mikono mitupu.

Wengi wamejadili juu ya vurugu zilizotokea bungeni. Mawazo mengi yametolewa. Mimi nataka leo nijikite zaidi katika upotoshaji unaoelekea kukubalika katika siasa za Tanzania juu ya hali ya uongozi wa taifa na taasisi zake.

Baada ya naibu spika kuamuru polisi wamtoe kwa nguvu nje ya ukumbi wa Bunge kiongozi wa upinzani bungeni Freeman Mbowe, wabunge kadhaa walimpongeza kwa hatua hiyo. Alimiminiwa pongezi na wabunge wenzake wa CCM kuwa ni mtu jasiri; aliyejaa busara na uvumilivu.

Wengine wakamfananisha na Rais Jakaya Kikwete kwa jinsi alivyo muungwana na mwana demokrasia. Kwa ufupi, naibu spika akaonekana na kuitwa jasiri ilihali Rais Kikwete akionekana na kuitwa muungwana.

Kwa hali yoyote na kwa sababu yoyote, kitendo cha kutumia polisi ndani ya ukumbi wa bunge hakikubaliki. Bunge ni eneo nyeti lenye utakatifu na upekee wa aina yake. Viongozi wakubwa wa dunia, wafalme na wenye mamlaka hawapendi hata kutembelea maeneo ya Bunge.

Katika nchi zinazoheshimu demokrasia, Bunge lina heshima kubwa kuliko hata mhimili wa utawala na ule wa mahakama; kwa sababu ndipo sheria hutungwa na ndipo viongozi wa mhimili wa utawala huidhinishwa. Kitendo cha kuzoea kutumia polisi ndani ya ukumbi huo, kimenajisi heshima ya bunge letu.

Tumezoea kuona polisi wanatumika kukamata vibaka mitaani, wakisumbuana na machinga, waandamanaji na wanafunzi. Hatujazoea na hatupendi kuzoea kuona polisi wakikamata, kupiga na hata kuwatukana wawakilishi wa wananchi.

Kuna hatari ya kuwajengea hofu wawakilishi wa wananchi na kuwafanya wasite kuihoji serikali kwa uhuru wakihofia kuwa spika ataita polisi wawatoe nje na kuwapiga. Kitendo cha kutumia polisi ili kuzuia maoni ya wawakilishi wawapo bungeni hakikubaliki na hakiwezi kukaribia kuitwa ujasiri au busara.

Polisi kwa kawaida hutumika katika masuala ya jinai na sidhani kama kumgomea spika au naibu wake ni kosa la jinai ndani ya kanuni za Bunge. Pengine labda ndiyo maana hata yeye naibu spika aliishia kutoa “msamaha” mara moja na kusema kiongozi huyo wa upinzani arejee bungeni jioni hiyo hiyo.

Pamoja na “msamaha” huo, tayari doa kubwa jeusi lilikuwa limeingia katika mhimili huu muhimu wa dola. Kwanza, kwa kutumia polisi kuzuia mawazo fulani na wakati huo huo kuruhusu mawazo fulani tu ndiyo yasikike.

Pili, kwamba, kwa mara nyingine tena, bunge letu limedhalilika mikononi mwa naibu spika Ndugai. Ni Ndugai huyu huyu ambaye amehusika katika matukio yote ya kuwatoa nje wabunge pale wanapotofautiana mawazo na serikali.

Nihitimishe sehemu hii kwa kutamka pasipo shaka kuwa, unaoitwa ujasiri wa Ndugai, ni ubabe uliokithiri, ni hujuma kwa mhimili wa bunge na ni uhaini dhidi ya utawala wa wananchi ambao ndilo chimbuko la mamlaka zote hapa nchini. Ubabe kuuita ujasiri ni dalili pevu za kufilisika kisiasa na kimaadili.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alituachia urithi mkubwa wa fikra na falsafa nzito nzito. Aliwahi kusema, “bila CCM imara, taifa litayumba.” Kwa ujumla wake, taifa ni mjumuiko wa mhimili yote mitatu ya dola.

Tunaendelea kushuhudia kuyumba kwa mihimili yote. Bunge limeyumba na kujidhalilisha chini ya uongozi dhaifu wa spika na naibu wake. Kama lingekuwa huru, lilipaswa kuwafukuza kazi hawa viongozi ili lirejeshe heshima ya chombo hiki.

Mhimili wa mahakama umepoteza hadhi mbele ya umma. Siku hizi kumwambia mtu aende kutafuta haki yake mahakamani, ni sawa na kumtusi tusi la nguoni. Ndani ya mahakama haki inanunuliwa kwa fedha na kujuana; na ikipatikana bila kununua wala kujuana, inachelewa sana.

Hata wanaofanya kazi mahakamani, wakidhulumiwa hawafikirii kutumia mahakama kupata haki zao. Mahakama imegeuka kuwa taasisi ya kisingizio cha kutoa haki, lakini kimsingi haki haipo huko.

Tumesikia tuhuma nzito za uteuzi wa majaji kinyume cha sheria. Tumesikia tuhuma nzito za majaji kujihusisha na kuwakingia kifua wafanya biashara wa madawa ya kulevya.

Tumesikia malalamiko ya Taasisi ya Kuzuia na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), kuwa mahakama inakwamisha kesi zote za rushwa kwa sababu mahakimu ni moja ya makundi yanayolengwa na TAKUKURU. Tuhuma hizi tatu juu ya mahakama zingetosha kuifanyia marekebisho makubwa idara ya mahakama na tume ya kuchunguza mienendo ya majaji wetu na jinsi walivyoteuliwa.

Mhimili mwingine ni wa utawala. Huu unaongozwa na rais ambaye ni mkuu wa nchi. Chama kinachoyumba na kuyumbisha nchi kinaongozwa na huyu na rais. Mahakama inayonuka rushwa imeteuliwa na rais huyu huyu. Bunge lililopoteza mwelekeo huitishwa na huyu rais na laweza kuvunjwa na rais huyu. Huyu anaweza kuwa chanzo cha madhaifu yote tunayoyashuhudia katika mihimili mingine.

Udhaifu wa kiongozi wa mhimili wa utawala umeambukiza na kueneza udhaifu katika sekta zote nchini. Mila na desturi haziruhusu watendaji kutamka hadharani yale waliyo nayo mioyoni mwao kuhusu udhaifu wa kiongozi wa mhimili wa utawala. Uwajibikaji wa pamoja unatafsiriwa kuwa udhaifu wa pamoja.

Badala yake, wapambe wake na wale wanaonufaika na udhaifu wake wameubatiza udhaifu huu kuwa ni uungwana, upenda watu na uvumilivu.

Kwa kiongozi wa nchi kuwa na madaraka makubwa lakini akawa na udhaifu na kushindwa kuyatumia kwa haki ni dhambi sawa na kuyatumia vibaya. Katiba za nchi changa hukimbilia kuweka vifungu katika katiba ili kuwabana viongozi wanaotumia madaraka yao huku wakisahau viongozi wanaoshindwa kutumia madaraka hayo.

Kwa udhaifu wa kiongozi wetu, watu wengi hawana pa kukimbilia kwa sababu, tumegundua kwa kuchelewa kuwa udhaifu wa kiongozi huambukiza maeneo mengine na udhaifu hutanda kama buibui.

Kutumia polisi ndani ya ukumbi wa Bunge hatuwezi kuuita ujasiri, kwa hiyo kushindwa kuongoza dola hatuwezi kukuita uungwana. Ni udhaifu unaopaswa kutendewa haki kwa kumpeleka mahakamani mhusika. Hatuna hiyo mahakama labda tuiunde kama nyingine zinazopendekezwa.

Tuna mahakama ya ardhi, biashara, kazi, na ile kuu. Zote zinapendekezwa za familia, kadhi, madawa ya kulevya, trafiki, rushwa, ufisadi, chaguzi mbalimbali, na sasa ninapendekeza mahakama ya kuwashtaki viongozi wababe kama na wadhaifu kama rais wetu.

error: Content is protected !!