June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uandikishaji BVR wakwama

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda (kulia) akiwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika katika uzinduzi wa uandikishaji wa daftari la wapiga kura kwa kutumia BVR

Spread the love

UANDIKISHAJI wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters’ Registration (BVR) uliopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kukamilika ndani ya siku saba, umekwama. Edson Kamukara anaandika…(endelea).

MwanaHALISI Online, imebaini kukwama huko kumesababishwa na idadi kubwa ya wapigakura waliojitokeza katika aneo lengwa la Makambako mkoani Njombe, kuzidi uwezo wa vifaa na utendaji wa NEC.

Awali, NEC ililenga kutumia siku saba kuandikisha watu wote wenye sifa, lakini kwa hali ilivyo, sasa inakiri ‘kasoro’ hizo na inafikiria kuongeza muda zaidi ili kuhakikisha watu wote wenye sifa za kuandikishwa wanapata haki hiyo.

Mpaka sasa watu walioandikishwa na NEC hawafikii hata nusu ya idadi ya wananchi wenye sifa za kuandikishwa.

Viongozi wa NEC hawakuwa tayari kupokea simu zao walipotafutwa na MwanaHALISI Online, lakini Mkurugenzi wake, Julius Malaba, alikaririwa na vyombo vya habari, akisema “Tume imeguswa na hali hiyo na hivyo inajipanga kuitatua”.

“Tumeiona hiyo changamoto ya wingi wa watu kati ya waliojitokeza kujiandikisha. Tumetoa wito watu waendelee kujitokeza kujiandikisha na sisi tutahakikisha wote wanaandikishwa; iwe kwa kuongezwa vifaa au vinginevyo,” anasema Malaba.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, mmoja wa maafisa waandikishaji ambaye ameomba kuhifadhiwa jina, anasema NEC bado imeelemewa kutokana na kuwa na vifaa pungufu na utendaji duni.

Anasema matarajio ya NEC yalikuwa kuandikisha wapigakura zaidi ya 65,000 kwa takwimu za uchaguzi mkuu wa 2010, ingawa idadi hiyo kwa sense ya 2012 imefikia wapigakura zaidi ya 93,000.

“Kwa sasa kit moja ya BVR ikiwa na mtendaji mzoefu na kusitokee kasoro yoyote kama ya kamera na alama za vidole kugoma, inaweza kuandikisha watu 100 mpaka 103 kwa siku.

“Ina maana kwamba kwa siku NEC inaandikisha watu zaidi ya 5,400 ambapo kwa siku saba ni sawa na kuandikisha watu zaidi ya 37,000,” anasema mtoa taarifa huyo.

MwanaHALISI Online pia limedokezwa kuwa, mbali na vifaa vya uandikishaji kuwa pungufu na kasoro za kugoma mara kwa mara, vile vile watendaji wa NEC hawakupata mafunzo mazuri ya namna ya kutumia mashine hizo.

“Waandikishaji wanababaika, watu wanafika wengi, wanapanga foleni kutwa nzima, halafu mara wanaambiwa kamera inagoma au alama za vidole hazisomi…watamalizaje kuwandika watu wote kwa siku saba,” mtoa tarifa wetu anabainisha.

Malaba katika tamko lake anakaririwa akisema kuwa, hadi kufikia siku ya tano, NEC walikuwa wameandikisha watu 19,396.

Anasema kwa siku ya kwanza, waliandikisha watu 3,014, siku ya pili watu 4,727, siku ya tatu watu 5,301 na siku ya nne watu 6,354- takwimu ‘anazoziita’ kuwa zinaonesha ongezeko la ufanisi.

Mapungufu ya Makambako, yanathibitisha malalamiko ya vyama vya siasa na wadua kwamba NEC haikujiandaa vya kutosha kuandikisha wapigakura kwa mfumo wa BVR.

Kwamba, kuendelea kulazimisha mfumo huo kwa lengo la kutimiza matakwa ya sheria ya kura ya maoni ya kupitisha Katiba mpya inayopendekezwa Aprili 30, mwaka huu, kutawakosesha watu wengi haki ya kujiandikisha.

error: Content is protected !!