July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uandikishaji BVR giza nene

Msimamizi wasaidizi wa kuandikisha vitambulishi vya wapiga kura kwa mfumo wa BVR, Halima Hamisi akisubiri wananchi kwa ajili ya kujiandikisha

Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetakiwa kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika uandikishaji wananchi kwenye daftari la kudumu la mpiga kura kwa mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR). Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Pia NEC imetakiwa kuagiza maeneo ambayo wananchi hawajaandikishwa kazi hiyo irudiwe ili kuwapa nafasi ya kuingizwa katika daftari hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Martina Kabisama – Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za Kiraia wa Kuangalia Chaguzi Tanzania (TACCEO) unaoratibiwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), amesema “NEC inapaswa kuruhusu asasi nyingi za kiraia kutoa elimu ya uraia”.

Elimu hiyo itawezesha kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo ambalo ni haki ya Watanzania kwa mujibu wa Katiba.

Kabisama amesema katika uangalizi waliofanya katika mikoa ya Njombe, Lindi, Mtwara na Ruvuma, wamebaini ukiukwaji wa Sheria na Kanuni za Uchaguzi.

Anasema, “ukiukwaji huo ulihusu elimu ya mpiga kura na uchaguzi kutokutolewa kwa maeneo ya vijijini. Hali hiyo imepelekea baadhi ya maeneo kuwa na mwamko mdogo wa wananchi kwenda kujiandikisha.

“Wilaya ya Ruangwa siku tatu za mwanzo mwitikio ulikuwa mdogo sana na katika kituo cha uandikishaji cha Kitandi Gulioni 27 Aprili mwaka huu, waliandikishwa watu 44 tu,” amesema.

Kwa mujibu wa Kabisama, ukiukwaji mwingine ni “wananchi kuandikishwa bila kuchukuliwa alama za vidole.Tukio hili lilishuhudiwa katika wilaya ya Tunduru, Kata ya Nanjoka, Kijiji cha Mandingo, Kituo cha uandikishaji cha Shule ya Sekondari cha Frank Weston ambapo wananchi wasiojua kusoma na kuandika waliandikishwa bila kuchukuliwa alama za vidole”.

Aidha, uandikishaji ulifanyika hadi saa 6:00 usiku. 2 Mai mwaka huu, uandikishaji kwa baadhi ya maeneo katika wilaya ya Namtumbo uliendelea hadi saa 6:00 usiku ili kukamilisha siku saba zilizopagwa kwa maeneo hayo.

Pia, uandikishwaji katika kituo cha shule ya Msingi Namtumbo ulifanyika hadi saa mbili usiku na baadaye kuhamishiwa katika jengo la Halmashauri baada ya mashine za BVR kuzimika kwa ukosefu wa chaji ambapo uliendelea hadi usiku wa saa sita.

“Vituo vingine navyo vilihamishia uandikishaji halmashauri ambapo zoezi liliendelea hadi saa sita usiku. Katika Kijiji cha Ilikuyamandela, uandikishaji uliendelea hadi saa sita usiku na kulazimika kuahirisha kutokana na mashine za BVR kuzimika kwa ukosefu wa chaji na kuacha zaidi ya watu 80 bila kuandikisha,” ameleza Kabisama.

Ameongeza kuwa, baadhi ya vituo vya uandikishaji viliwekwa kwenye nyumba za ibada, hospitali na kwenye mabanda ya mama lishe, jambo ambalo linaweza kupelekea waumini wa dini nyingine kutokwenda kujiandikisha.

“Vituo vya uandikishaji kuwekwa kwenye nyumba za ibada uliweza kushuhudiwa katika Kanisa la Lutherani Ilembula, Kanisa la Pentekoste (Ufwala), Kanisa la Kristo Isoliwaya (Wanging’ombe): Pia baadhi ya vituo viliwekwa katika mazingira duni na yasiyo salama hasa kipindi hichi cha mvua,” ameongeza Kabisama.

Aidha, katika Wilaya ya Lindi vijijini, tarehe 2, 3 na 4 Mei mwaka huu, uandikishaji ulikuwa ukianza saa 6:00 mchana katika kata ya Chiponda, Kijiji cha Chiodia ‘B’ na maofisa wa NEC walishidwa kufika kwa wakati kutatua matatizo ya kiufundi na kupelekea wananchi waliojitokeza kushidwa kuandikishwa.

“Utaratibu wa kuandikisha kwa idadi ya kata na vijiji kwa muda wa siku saba tu na kuhamisha mashine kwenye kata nyingine unaonekana kuleta athari kwa wananchi.

“Hali hii imepelekea wananchi wengi kutokuandishwa hasa katika vijiji vya Mpaa, Kaya ya Mpapa, Tarafa ya Mbuji Wilaya ya Mbiga ambapo kukamilika kwa muda wa siku saba kuliachwa zaidi ya watu 200 bila kuandikishwa,” amefafanua Kabisama.

error: Content is protected !!