July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uamuzi wa shauri la aliyedaiwa kujinyonga kituo cha Polisi lasogezwa mbele

Spread the love

 

MAHAKAMA ya Wilaya ya Kinondoni imeahirisha kutoa uamuzi juu ya maombi ya familia ya marehemu Stella Moses (30) aliyedaiwa kujinyonga kwenye kituo cha Polisi cha Mburahati ya kutaka mwili wake ufanyiwe uchunguzi. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Familia ya Stella tangu mwaka 2020 haikuwa na imani na kifo cha mwanamke huyo ambapo walishinikiza Polisi kufanya uchunguzi wa kifo hicho mpaka kufikia kufungua shauri dhidi ya Mkuu wa jeshi la Polisi IGP Simon Sirro na wenzake juu ya mashaka yao ya mazingira ya kifo cha mwanafamilia huyo.

Jana tarehe 13 Juni 2022, mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Kinondoni ,Erick Rwihumbiza, wakili wa Wakili wa Serikali Daisy Makakala ameieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo lipo kwenye hatua ya uamuzi na kwamba ilikuwa iamuriwe na Hakimu Aron Luyamuya ambaye hakuwepo mahakamani kutokana dharura ya kiofisi.

Wakili wa muombaji Peter Madeleka amedai mahakamani hapo kuwa shauri hilo lilipaswa kuweka kwenye kumbukumbu za kimahakama lakini Karani akadai kuwa jalada la kesi hiyo halipo mikononi mwake.

Hakimu Rwihumbiza amesema kuwa kwa vile shauri hilo lipo kwenye hatua ya uamuzi jalada litakuwa lingalipo kwa Hakimu Luyamuya.

Wakili Madeleka amedai mahakamani hapo kuwa ni mara ya pili jalada la shauri halijaonekana na kuomba shauri hilo likitajwa tena lipatikane ili haki ya familia ya Stella ipatikane upesi.

Shauri hilo limeahirishwa hadi tarehe 28 Juni 2022.

error: Content is protected !!