September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uamuzi kesi ya MAWIO bado

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha utoaji uamuzi kuhusu ubishani wa kisheria ulioibuka kufuatia hatua ya upande wa mashitaka kutaka washitakiwa wasomewe upya mashitaka yakiwemo yale mawili yaliyofutwa, anaandika Faki Sosi.

Hatua hiyo imeikumba kesi ya tuhuma za uchochezi inayomkabili Tundu Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki pamoja na waandishi wa habari waandamizi nchini, Jabir Idrissa na Simon Mkina.

Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Ismail Mahboob ambaye ni Meneja wa kampuni ya Flint, inayochapisha magazeti mbalimbali likiwemo la Mawio ambalo kesi hiyo imezalika kutokana na habari ilizochapisha katika toleo lake la Januari mwaka huu.

Leo ilikuwa ni siku ambayo Hakimu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba alipanga kutoa uamuzi wa ubishani uliotokea tarehe 29 Agosti baada ya mawakili wa upande wa mashitaka kutaka kusoma upya mashitaka dhidi ya washitakiwa.

Ombi hilo lilipingwa na mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na Peter Kibatala, kwa maelezo kuwa kisheria mashitaka yaliyofutwa na mahakama, hayawezi kurudishwa kwa utaratibu wa kuyasoma upya, isipokuwa kilichotakiwa kutendeka, ni ama kukatia rufaa uamuzi wa awali au kuomba mapitio ya uamuzi huo.

Upande wa mashitaka ulitaka kusoma upya mashitaka yote manne kwa kutumia mwanya wa kuyasoma kwa ajili ya mshitakiwa wa kwanza, Jabir, ambaye hakuwepo mahakamani kesi hiyo ilipofikishwa kwa mara ya kwanza.

Jabir ambaye alikuwa mgonjwa, anahusishwa katika kesi hiyo kwa kuwa mwandishi wa habari iliyokuwa na kichwa cha maneno “Machafuko yaja Z’bar” ambayo ililalamikiwa na serikali na mbali na kuandaa kesi hiyo, ililifungia kwa muda usiojulikana gazeti hilo.

Mkina ndiye mhariri wa gazeti hilo wakati Lissu alikuwa mchangiaji wa maoni katika habari iliyochapishwa.

Hakimu Simba ameamua kupanga tarehe 19 mwezi huu kutoa uamuzi wa ubishani uliohusu usomaji upya wa mashitaka kwa washitakiwa. Katika siku hiyo pia kesi hiyo ndiyo itatajwa tena.

Kesi ilipofikishwa kwa kutajwa tarehe 29 Agosti, mawakili Kishenyi Mutalemwa na Nassoro Katuga wanaoiwakilisha jamhuri waliingia na hati mpya ya mashitaka wakitaka kuyasoma upya kwa kile walichoeleza “mshitakiwa wa kwanza, Jabir Idrissa amefika mahakamani kwa mara ya kwanza.”

Wakili wa utetezi Kibatala alipinga akieleza kuwa hata kama mahakama itaridhia kupokea hati hiyo, ichukuliwe kama ni kuiona tu na sio kuitambua kama hati halali kwa kuwa “hati ina mashitaka yaliyofutwa tayari… na waendesha mashitaka wenyewe waliridhia kufutwa mashitaka.”

Alikazia hoja yake akieleza kuwa mahakama iliyafuta mashitaka mawili – la kwanza na la tano – baada ya upande wa mashitaka wenyewe kuridhika hayakuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Wakili Mutalemwa aliomba muda wa saa moja, kupitia maelezo ya kisheria ili aweze kujibu hoja za utetezi lakini hata alipokubaliwa, alishikilia maelezo ya kutaka mahakama iruhusu washitakiwa wasomewe mashitaka yote.

Hakimu Simba alikataa rai hiyo. Badaa yake akambana mwendesha mashitaka kusoma mashitaka yaliyokubaliwa – la pili, tatu na nne – vinginevyo angewaachia watuhumiwa kwa kukosekana mashitaka mbele ya mahakama hiyo.

Upande wa mashitaka ulisoma mashitaka hayo matatu yaliyobaki kwa washitakiwa; la pili likimkabili Jabir, Mkina na Lissu, wakidaiwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika Gazeti la MAWIO, toleo Na. 182 la tarehe 14-20 Januari, 2016 lenye kichwa cha habari, ‘Machafuko yaja Z’bar’.

Shitaka la tatu linalo Ismail akidaiwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika Gazeti hilo la MAWIO toleo namba 182 la tarehe 14-20 Januari, 2016 lenye kichwa cha Habari ‘Machafuko yaja Z’bar’.

Shitaka la nne linamkabili Ismail akidaiwa kuchapisha gazeti bila kupeleka kiapo kwa Msajili wa magazeti.

 

error: Content is protected !!