January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uamuzi kesi kina Mbowe leo, maombi yatawala

Spread the love

 

KESI ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu, inaendelea leo Jumanne, tarehe 14 Desemba 2021, kwa Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam kutoa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Uamuzi huo, unahusu pingamizi la upande wa utetezi waliloweka dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa Mohamed Ling’wenya yasipokelewe mahakamani kama kilelezo wakidai, hakuwahi kuyatoa bali alilazimishwa kuyasaini, baada ya kuteswa alipokamatwa.

Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo, ndiye atakayetoa uamuzi huo na tayari washtakiwa wote wanne akiwemo Mbowe wamefikishwa mahakamani hapo na Jeshi la Magereza.

Kama kawaida, Mbowe na wenzao wameonekana wakiwa na nyuso za tabasamu wakati wakiwasili mahakamani hapo, Mawasiliano jijini Dar es Salaam na kupokewa na wanachama na viongozi wa Chadema.

Maombi mbalimbali yalitawala eneo hilo kwa kila mmoja kuwaombea washtakiwa hao huku wengine wakiwa wameshikilia bibilia na wengine wamepiga magoti.

Mbali na Mbowe na Ling’wenya, washtakiwa wengine ni Adam Kasekwa na Halfani Bwire.

Kasekwa, Ling’wenya na Bwire waliowahi kuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kikosi 92KJ, mkoani Morogoro.

Washtakiwa wote wanne, wanatuhumiwa kwa makosa ya kupanga vitendo vya kigaidi maeneo mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo Kilimanjaro, Dodoma, Dar es Salaam na Arusha kwa kulipua vituo vya mafuta, kufanya vurugu kwenye mikusanyiko ya watu na kudhuru viongozi wa umma.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!