January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uamsho wacharuka kortini

Wafuasi kundi la Uamsho

Spread the love

VIONGOZI wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), wanaokabiliwa na tuhuma za ugaidi, wamegoma kula wakidai bora wapigwe risasi za kichwa wafe kuliko kugeuza madai yao ya Zanzibar kuwa nchi inayojitegemea. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).

Madai hayo yalitolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Renatus Rutta wakati kesi yao ilipokuwa inatajwa.

Awali kabla ya kutolewa kwa madai hayo, upande wa Serikali ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo wanaomba kuahirisha kesi huku wakisubiri kumbukumbu za Mahakama Kuu kwa ajili ya kukata rufaa.

Baada ya kuelezwa hayo, ndipo Sheikh Farid Hadi Ahmed aliibua madai mazito na kueleza kwamba chanzo cha kupata mateso ndani ya magereza ni kutokana na mchakato wa katiba ya kuhakikisha Zanzibar inapata mamlaka sahihi.

“Madai yetu yote ilikuwa Zanzibar ipate mamlaka yake sahihi, baada ya kuonyesha msimamo huo ndipo misukosuko ikaanza kwetu, tukapewa kesi ya ugaidi bandia, hivyo madai yetu hatuwezi kuyageuza hata watuite wahaini tunaeleza tu.

“Tulifanyiwa mambo mengi ya ukatili, sisi tunadai heshima ya nchi yetu, tulitamka wazi hatutaki Muungano, tunataka Rais wetu apewe heshima yake kama Rais wa Zanzibar,”alidai.

Akizidi kutoa madai hayo, Sheikh Farid alieleza kwamba hawana ajenda ya siri, walifanya mihadhara zaidi ya 200, walitakiwa kushtakiwa Zanzibar na sio Bara, kwani mazingira wanayowekewa ni kutaka kudhulumiwa haki zao.

“Tunatoa wito kwamba serikali iliyopo madarakani imezeeka ni kikongwe. Mshtakiwa huyo na wenzake 22 waliomba siku saba kesi yao isikilizwe na endapo zitaisha hatua watakayochukua itaonekana kwani hawawezi kudhulumiwa na wakakaa kimya.”

Pia wanataka Kamishna wa Zanzibar ajieleze kwanini aliamua kuwaleta Tanzania Bara kuwashtaki.

Naye mshtakiwa Salum Ally, aliomba wapigwe risasi kichwani wamalizwe kwa sababu wamechoka.

Alidai kwamba amekuwa muathirika mkubwa kutokana na vitendo alivyofanyiwa ikiwemo kulawitiwa, kuingizwa chupa na vijiti sehemu ya haja kubwa.

Baada ya kutolewa kwa madai hayo, Hakimu Rutta aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 25 mwaka huu.

error: Content is protected !!