September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Twiga wakiri ngoma ngumu kuwatoa Zimbabwe

Spread the love

SOPHIA Mwasikili, Nahodha wa Timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars) amesema mechi yao dhidi ya Zimbabwe utakuwa mgumu kutokana na uzuri wa wapinzani wao, anaandika Regina Mkonde.

Twiga Stars inatarajia kuvaana na Zimbabwe kesho katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika, kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Mwasikili amesema katika mechi nne walizokutana na timu hiyo kulikuwa na upinzani mkali kutokana na ubora wa wachezaji wa timu hiyo.

“Tunakabiliwa na timu ngumu ya Zimbabwe, mechi nne za awali tulizocheza nao ilitupa upinzani wa hali ya juu uwanjani,” amesema Mwasikili.

Amesema, pamoja na ubora wa wapinzani wao lakini wamejipanga kuibuka na ushindi katka mechi ya kesho na ile ya marudiano, kutokana na mafunzo waliyopewa na kocha wao Nasra Juma.

Kwa upande wake, Nasra Juma, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, amesema timu yake iko tayari kwa mechi ya kesho, baada ya kufanya mazoezi kuanzia Februari 7, 2016 mpaka sasa.

“Matayarisho yalikuwa mazuri, tulifanya mazoezi asubuhi na jioni. Licha ya kukosa mechi za kirafiki lakini tulifanikiwa kucheza na timu za wanaume ambazo zilihimarisha wachezaji wetu,” amesema Nasra.

Nasra amesema kuwa, walihitaji kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki ili kuwajenga wachezaji kujiamini na kucheza vizuri ili kupata ushindi lakini hawakufanikiwa kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha na wadhamini.

Kocha huyo amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu ili kuwapa moyo wachezaji na kuwafanya kujiamini na kwamba itasaidia kushinda mechi hiyo.

Baraka Kizuguto, Afisa Habari wa TFF amesema, TFF imemaliza maandalizi yake ya mchezo wa kesho na kwamba tiketi za mchezo huo zitauzwa kesho Chamanzi.

error: Content is protected !!