May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Twiga Stars wamshukuru Rais Samia

Spread the love

 

TIMU ya Taifa ya wanawake nchini ‘Twiga Stars’ imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kudhamini mashindano ya kombe la Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki na kati (CECAFA) ambalo kwa mwaka huu litafanyika nchini Kenya. Anaripoti Wiston Josia…(endelea)

Hayo yamesemwa hii leo Agosti 26, 2021 na wachezaji wa Twiga Stars kwenye Mkutano uliofanyika na waandishi wa Habari, jijini Dar es Salaam kwenye hotel ya Serena.

Michuano hiyo ambayo kwa mwaka huu Tanzania itawakilishwa na Timu ya wanawake ya Simba ‘Simba Queen’ ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu bara kwa upande wa Wanawake.

Akitoa shukrani hizo hii leo moja ya wachezaji wa Twiga stars Ester Mabanzo alisema kuwa wao wataendelea kuitetea nchi yao na kumshukuru Rais Samia kwa kukubali kuwa sehemu wa udhamini wa michuano hiyo.

“Kwanza tunamshukuru mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutudhamini na kutuunga mkono, tunapenda kumu hakikishia tutaendelea kufanya mazoezi kwa nguvu na kujituma kutetea nchi yetu bila kujali watu wanasema nini”.Alisema mchezaji huyo

Rais Samia alitoa ahadi hiyo ya kudhamini michuano ya CECAFA kwa wanawake Ikulu jijini Dar es Salaam, Agosti 22, mwaka huu, kwenye hafla ya kupokea kombe la CECAFA kwa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23, walilotwaa nchini Burundi mara baada ya kuwafunga wenyeji kwa changamoto ya mikwaju ya penati 6-5.

Katika tukio hilo Rais Samia alisema kuwa alipata ombi kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF), Wallace Karia juu ya kuanzishwa kwa michuano hiyo ya CECAFA kwa wanawake na hivyo kuomba udhamini.

Rais Samia Suluhu Hassan

“Kuna ombi tulinong’ona na Rais wa TFF, wanataka kuanzisha CECAFA ya wanawake, lakini mashindano haya wanataka udhamini, akatolea mfano mwenzake Kagame anadhamini michuano Fulani huko, sasa itakuwa vyema na wewe ukidhamini haya”

“Nikamuliza anitajie kiasi gani ili niangalie misuli yangu, akanitajia hicho kiasi ambacho sitaki kukisema hapa, lakini nilipima misuli yangu nikaona mwenyewe sitaweza, lakini nitajua wapi nitakapozipata.”

“Kwa hiyo niwatangazie kuwa nitadhamini michuano hiyo”Alisema Rais Samia

Ikumbukwe timu hiyo ya wanawake kwa sasa ipo kambini na wanafanya mazoezi yao kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kujifua kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Baraza la vyama vya soka kusini mwa Afrika ‘COSAFA’

error: Content is protected !!