March 4, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yaendelea kulisakama TWAWEZA

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa TWAWEZA

Spread the love

SHIRIKA linaloshughulika na masuala ya utafiti nchini, linalofahamika kwa jina la TWAWEZA, lidai kutishwa na vyombo vya serikali. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Kutishwa kwa watendaji wa Twaweza, kumethibitishwa leo tarehe 3 Agosti 2018 na Mkurugenzi Mtendaji wake, Aidan Eyakuze.

Hata hivyo, Eyakuze amesema, “pamoja na kupokea vitisho hivyo, shirika langu litaendelea kufanya kazi zake za kitafiti na halitakubali kurudishwa nyuma.”

Eyakuze aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuwa kwa sasa shirika lake, linapita katika kipindi kigumu chenye changamoto nyingi.

Amesema, “…hatutatikisika. Hatutarudi nyuma. Twaweza litaendelea kufanya kazi zake kwa mujibu wa misingi na sharia za nchi.”

Amesema, tangu shirika hilo litoe taarifa zake za kitafiti mbili kupitia wanachoita, “Sauti za Wananchi,” mahusiano yake na taasisi za serikali yamekuwa mabaya.

Amesema, “tangu Twaweza izindue ripoti zake, imepokea barua mbili kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), zilizohoji uhalali wa program (mpango) ya Sauti za Wananchi na kutaka litoe ufafanuzi kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yetu.”

Tarehe 5 Julai mwaka huu, Twaweza ilizindua ripoti mbili zenye vichwa vya habari, “Kuwapasha viongozi na Nahodha wa Meli yetu wenyewe,” ripoti ambazo zinaonekana kuwaudhi baadhi ya viongozi serikalini.

Katika moja ya ripoti hizo, Twaweza walidai kuwa umaarufu wa Rais John Pombe Magufuli, umeshuka kutoka asimilia 96 mwaka 2016 hadi asilimia 71 mwaka 2017.

Akiongea kwa kujiamini, Eyakuze amesema, uhuru wa shirika lake katika kutekeleza majukumu yake, wanaupa kipaumbele kikubwa, hasa wakati wa kufanya kazi za kitafiti, ikiwamo kuhoji na hata kutoa majibu ya utafiti.

“Tumekubaliana kuwa tutaendelea kufanya kazi zetu pasipo kujibana na kujidhibiti. Tutafanya kama kawaida na kwa kushirikiana na serikali,” ameeleza.

Kwa mujibu wa Twaweza, kati ya Watanzania 10, saba wanaunga mkono utendakazi kazi wa Rais Magufuli.

Hii ina maana kuwa umaarufu wa Rais Magufuli umeshuka kwa asilimia 25, jambo ambalo linaonekana kuikera serikali.

error: Content is protected !!