July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

‘Tuutukuze utalii wa ndani’

Spread the love

WATANZANIA wametakiwa kujenga tabia ya kutembelea hifadhi mbalimbali za wanyama kwa ili kukuza utalii wa ndani, anaandika Dany Tibason.

Hayo yalielezwa na maofisa utalii ambao ni Daniel Mweta na Eunice Msangi walipokuwa wakitoa maelezo kwa mgeni rasm, Geoffrey Mwambe, Mkuu wa Wilaya Manyoni mkoani Singida alipotembelea mabanda katika maonesho ya wakulima,wafugaji na wavuvi yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni mjini humo.

Maofisa hao wamesema, Watanzania wengi bado hawaoni umuhimu wa kufanya utalii wa ndani wakidhani utalii ni kwa ajili ya watu kutoka nje ya nchi.

Wamesema, pamoja na mambo mengine wamekuwa wakitoa elimu juu ya kuhamasisha kuhusu uhifadhi na utalii wa ndani.

Wakitoa maelezo kwa mkuu huyo wa wilaya wameeleza kuwa, kiwango cha mtalii wa ndani ambacho anatakiwa kulipa ni kidogo na ni fedha ya Tanzania na si Dola ya Marekani.

Hata hivyo maofisa hao wamemweleza mkuu huyo kuwa utalii wa Tanzania unakabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja kukosekana vitanda vya kutosha.

Wamesema, kutokana na ukosefu wa vitanda vya kutosha TANAPA imeanzisha mpango wa kuwepo kambi za mahema ambayo kwa sehemu zinaonekana kukubalika.

Naye Mwambe amewaambia kwamba, licha ya kuwa TANAPA kutoruhusiwa kufanya biashara lakini ni bora wakaansika mapendekezo ambayo yatapelekwa kwa Waziri Prof. Jumanne Maghembe ili naye ayawakilishe kwa Kassimu Majaliwa, Waziri Mkuu.

Amesema kuwa, ni vyema wakapatikana wawekezaji ambao wanaweza kujenga mahotel makubwa ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa vitanda katika sehemu za utalii.

error: Content is protected !!