July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tutawatambua kwa fikra na matendo yao

Rais wa Jakaya Kikwete (katikati) akiwa na Marais wastaafu, Benjamin Mkapa (kushoto) na Ali Hassan Mwinyi (kulia).

Spread the love

VITABU vinne vya mwanzo vya maandiko ya Kikristo vya Agano jipya, vinazungumzia maisha, kifo, ufufuo na mafunzo ya Yesu. Vitabu hivi-Matayo, Marko, Luka na Yohana kwa pamoja vinajulikana kama vitabu vya injili.

Vitabu hivi vinatoa ushuhuda na mafundisho ambayo yanakumbusha wajibu wa waumini wa Kikristo katika maisha yao ya duniani.

Vitabu hivi vinaeleza kwamba maisha na matendo ya Yesu yalikuwa sio ya kutilia shaka hata kidogo bali ni mafundisho ambayo tunapaswa kuyaishi hapa duniani.

Ni matendo haya ambayo yalimfanya Yesu aitwe majina mengi kama “Mwana wa Mungu”, “Masiha”, “Mwokozi” na mengine na katika moja ya mafundisho ya Yesu alituasa juu ya kutokea kwa manabii wa uongo.

Bila shaka umewahi vilevile kusikia wimbo maarufu wa injili ukiwa kwenye daladala, basi au nyumbani, ambao unawakumbusha kutambua watu wema na wabaya katika jamii kwa matendo yao wala si haiba yao, wala si mavazi yao na wala si ukwasi wao.

Kibwagizo cha wimbo huu kinasema “utamtambuaje aliyeokoka… utamtambua kwa matendo”. Kwa tasfsiri yangu, watu wema ni watu wa liookoka, watu wanaomjua Mungu, watu wenye matendo mema.

Na ukitazama video ya wimbo huu na kutafakari kwa kina utagundua umebeba ujumbe mzito kwa Watanzania nje ya mtazamo wa kidini hasa kuelekea uchaguzi mkuu.

Moja ya kauli mashuhuri za Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ni aliposema “kila nyakati na kitabu chake.”

Ninavyotafakari vitabu vya mafundisho ya Yesu, najikuta nikiogelea awamu za uongozi wa Tanzania kuanzia kwa Mwalimu Julius Nyerere.

Bila shaka kila Rais aliingia madarakani kwa mtindo wa aina yake kulingana na nyakati na kila mmoja alibatizwa au alijibatiza jina au majina yake kutokana na matendo yake.

Maneno, maandishi na matendo yao bila shaka yanatoa mafundisho ambayo tulitakiwa au tunatakiwa kuyatafakari kwa kina na kwa maslahi mapana ya taifa letu.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliingia madarakani akipokea nchi ya Tanganyika kutoka kwa Wakoloni kama Waziri Mkuu mtendaji na hatimaye Rais wa Tanzania na kazi yake kubwa ilikuwa kuvunja fikra ya kikoloni kwa madhumuni ya kujenga nchi ya Ujamaa na Kujitegemea.

Mzee Ali Hassan Mwinyi alipokea madaraka kwa Nyerere chini ya mfumo wa chama kimoja, chama kushika hatamu na alijenga taswira ya ujenzi wa soko huria na hatimaye kubatizwa jina la “Mzee Ruksa”.

Mzee Ali Hassan Mwinyi alibeba agenda ya fursa za kiuchumi kuendana na wimbi la mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi. Ni katika kipindi hiki ambapo nchi yetu ililazimika kubadili sera na sheria zake ili kuendana na mabadiliko haya.

Benjamin Mkapa akapokea madaraka kutoka kwa Mwinyi na kubatizwa jina la “Mr.Clean” na kujenga taswira ya ubinafsishaji kuendana na kasi ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi, wakati huu Mkapa akajibatiza jina la “Mzee wa Ukweli na Uwazi”.

Mkapa alingia madarakani chini ya mfumo wa vyama vingi, ni katika kipindi hiki ambapo Mwalimu Nyerere alituachia ujumbe mzito. Alituasa kuwa “Ikulu ni mahala patakatifu…sasa ukiona mtu anapakimbilia kwa gharama yoyote hata kununua watu, mtu huyo ni wa kuogopwa kama ukoma…hatufai kuwa kiongozi wetu”.

Ujumbe huu unawakumbusha wananchi kutazama kwa makini ajenda zilizobebwa na wanaotaka kugombea uongozi wa nchi katika taasisi kubwa ya urais.

Awamu ya nne ya uongozi ikanzishwa kauli mbiu ya “Ari mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya” ambapo kwa mujibu wa wachambuzi wa kisiasa na makada wa chama tawala, dhana nzima ilikuwa kuendeleza yale yote ambayo aliyanzisha Mkapa na kiongozi mmoja wa kiroho akatuhakikishia kwamba Jakata Kikwete alikuwa “chaguo la Mungu”. Bila shaka kipindi cha uongozi wa awamu ya nne tumejifunza mambo mengi na kuna wakati tukajikuta kwenye msongo wa mawazo kisiasa hasa kutokana na maneno na matendo ambayo tunayatafakari na kuyashuhudia. Bila shaka ni darasa la kutosha kuelekea uchaguzi wa 2015. Kwanini?

Ukitazama awamu zote nne, kuna jambo la kujifunza katika mbio za urais kuelekea Ikulu. Kwanza kuna suala la nguvu ya ushawishi na pili kuna nguvu ya fedha.

Nyerere hakupendwa kwa sababu ya kutumia nguvu ya fedha bali alipendwa kwa sababu ya maono yake, hekima, busara pamoja na kuelewa changamoto za nyakati zilizoikumba jamii.

Alitambua kwamba Watanganyika walikuwa wanahitaji uhuru na jamii, iliamuamini kwa sababu ya upeo na uzalendo wake katika harakati za kudai uhuru. Alikuwa amebeba agenda kubwa ambayo ndio ilikuwa lugha ya Watanganyika kwa wakati huo.

Mwinyi alibeba agenda ya fursa za kiuchumi kuendana na wimbi la mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yaliyotokea duniani kote katika kipindi cha miaka ya 1985 hadi 1990 na kuendelea.

Ni katika kipindi hiki ambapo nchi yetu ililazimika kubadili sera na sheria zake ili kuendana na mabadiliko haya. Japokuwa yalivyopokelewa tofauti na matarajio kulingana na nyakati ilikuwa ni darasa la Watanzania kujifunza kukabiliana na changamoto za nyakati.

Katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi, nguvu ya fedha imechukua nafasi kubwa kuliko nguvu ya ushawishi, nguvu ya hoja imetekwa na nguvu ya fedha.

Umejengeka utamaduni mpya wa nani kasema kuliko kasema nini, nguvu za hoja zimekuwa si kipaumbele. Pamoja na changamoto hii hatuna budi kupima kwa umakini agenda ambazo limebebwa na wale ambao wanatangaza wokovu wa Watanzania kupitia taasisi ya urais. Lakini vilevile tunapaswa kujua sifa na rekodi za kiutendaji katika utumishi wa umma za wagombea ikiwa ni pamoja na kuchunguza sifa za marafiki na wapambe wao. Bila umakini katika kujua na kuchunguza haya kwa umakini, tutajikuta tukitengeneza mtandao wa kimafia.

Tunapaswa kupata viongozi wenye upeo, maono na uadilifu. Hatupaswi kupuuza msingi wa kufanya michakato ya kupata viongozi bora na kuchagua pesa kutuchagulia viongozi.

Iwapo tutapuuza kupata muda wa kutosha wa kutafakari matokeo ya maamuzi yetu tunajikuta tukiishi na maamuzi ambayo vinginevyo tusingekuwa tayari kufanya.

Je, umetafakari vya kutosha juu ya maneno, matendo na mitazamo yao ya kitaifa kwa wale ambao wametangaza kuwapeleka Watanzania kwenye wokovu, kuondokana na umasikini, rushwa, ujinga, maradhi na ufisadi?

Germano Walter, amejitambulisha kama msomaji wagazeti hili ambaye anapatikana kwa simu; 0788332480

error: Content is protected !!