July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Tutaondoa vikwazo kwa wanafunzi wa kike’

Wanafunzi wa kike wanaosoma shule ya msingi

Spread the love

SERIKALI imesema imejipanga kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyowakumba wanafunzi wa kike pindi wanaposhindwa kuhudhuria masomo yao ili kuwasaidia kutimiza ndoto zao walizojiwekea. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Afisa Elimu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Mafunzo na Ufundi, Madina Kiwanga wakati akifungua maadhimisho ya siku ya hedhi duniani, iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja.

Kiwanga amesema, siku hii imeadhimishwa nchini kwa mara ya kwanza ili kuwawezesha wanafunzi hao kujijengea desturi ya usafi na kujiepusha na kutumia vifaa visivyo salama katika kipindi hicho.

“Siku hii nchini kwetu imeadhimishwa kwa mara ya kwanza, ila kwa kidunia ni mara ya pili lengo kuu likiwa kuongeza uelewa umuhimu wa hedhi salama kwa watoto wa kike na akina mama,” amesema Kiwanga.

Ameongeza, “sambamba na hilo katika siku hii tumejipanga kuongeza mikakati kabambe ya kuhakikisha hedhi salama kwa wanafunzi inazingatiwa ili kuwaepusha na magonjwa ya saratani.”

Amefafanua kuwa changamoto zinazowakumba wanafunzi wa kike katika kipindi cha hedhi ni kukosa maji safi na salama, kutokuwa na vyoo bora mashuleni, pedi za kutosha sambamba na kutohudhuria kikamilifu katika masomo yao kutokana na maumivu yanayowakumba.

“Katika kuadhimisha siku hii, serikali imejipanga kikamilifu kuwawekea mazingira salama na miundombinu wanafunzi wote wa shuleni kwa kuwapa na elimu ya kujikinga na maradhi yanayoweza kuwakumba pindi watakaposhindwa kuwa wasafi na kwa wale wa vijijini na wasiokuwa na elimu waweze kujifunza kwa kampeni zitakazoendeshwa na wizara ya elimu kwa kushirikiana na wizara ya afya pamoja na wadau mbalimbali,”amesema.

Naye Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania, Ibrahim Kabole, amesema kutokana na hali hiyo inayowakumba wanafunzi wa kike katika mashule, kwa mujibu wa  takwimu walizozifanya zinaonyesha kuwa hupoteza takribani siku arobaini kwa mwaka.

“Wanafunzi hushindwa kuhudhuria vipindi shuleni kwa mwaka zaidi ya siku arobaini kutokana na hali ya hedhi inayowakumba, pamoja na kuhofia hali ya magonjwa kutokana na kukosa mazingira rafiki ya kujisaidia,”amesema Kabole.

error: Content is protected !!