May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tutaenzi maono ya Rais Magufuli – Waziri Majaliwa

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania

Spread the love

 

KASIM Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania amesema, serikali itaenzi na kuendeleza jitihada, maono na juhudi za aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli hususan katika ulinzi wa rasilimali za Taifa pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Jumanne, tarehe 13 Aprili 2021, wakati akiwasilisha hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2021/2022, bungeni jijini Dodoma.

Amesema, mambo mengine yatakayoenziwa ni pamoja na nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kuenzi lugha ya Kiswahili, kuunganisha na kuwajali wananchi wanyonge na kudumisha umoja wa kitaifa.

“Kwa kasi tuliyoanza nayo, serikali itaendelea kuongeza nguvu zake na hatimaye kukamilisha miradi hiyo.

“Serikali itaendelea kuimarisha huduma za jamii zikiwemo afya, elimu na maji pamoja na utekelezaji wa miradi inayoendelea na uanzishwaji wa miradi mipya.

“Pia itaimarisha makusanyo ya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na mashine za POS na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuendeleza rasilimali fedha katika miradi ya kimkakati na kielelezo,” amesema.

Waziri Majaliwa amesema, serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo kutekeleza miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii, pia kuchukua hatua za kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo magonjwa ya mlipuko kwa kuzingatia maelekezo  yanayotolewa na wataalam.

Waziri Majaliwa ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya Sh. 116,7. Bil kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa matumizi ya mwaka 2021/2022.

error: Content is protected !!