October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tundu Lissu: Nawahurumia wadhamini wangu

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

TUNDU Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema anawahurumia wadhamini wake katika kesi ya uchochezi inayomkabili. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

“Niliwashauri wadhamini wangu wamuombe hakimu kujitoa kwenye udhamini wa kesi yangu. Wao hawana kosa lolote lile kutokana na mimi kutokuwa mahakamani.

“Hawakusababisha kuondoka kwangu, na hawana uwezo wa kunirudisha nchini,” amesema Lissu alipofanya mahojiano na mwandishi wa habari hii kwa njia ya mtandao wa Whatsapp, leo tarehe 20 Januari 2020.

Wakati Lissu akisema hayo leo tarehe 20 Januari 2020, kesi hiyo imeendelea kusikilizwa ambapo Thomas Simba, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu amesisiiza kumtaka Lissu mahakamani hapo.

Hakimu Simba amesema, tarehe 20 Februari 2020 anamtaka Lissu mbele ya mahakama ili aendelee na kesi yake, vinginevyo anaweza kuwachukulia hatua zaidi wadhamini wake (Robert Katula na Ibrahim Ahmed).

“Tumemweleza hakimu kwamba sisi nguvu zetu tumeishia hapo, tumemwandikia barua Mbowe (Freeman Mbowe, Mwenyekiti Chadema – Taifa) kutusaidia kumshauri Lissu arejee, lakini mpaka sasa hajatujibu,” amesema Katula.

Watuhumiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Simon Mkina, ni mhariri wa gazeti la MAWIO; Jabir Idrissa, mwandishi wa gazeti hilo na Ismail Mehbob, mfanyakazi wa kampuni ya uchapishaji ya magazeti ya Jamana, wanakabiliwa na mashitaka matano katika mahakama hapo, likiwamo uchochezi.

Wote wanne, wanatuhumiwa kuandika, kuchapisha na kusambaza taarifa hizo kwenye gazeti la MAWIO la tarehe 14 Januari 2016, kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002. Habari ambayo inadaiwa kuwa ya uchochezi, ilibeba kichwa cha maneno kisemacho: “Machafuko yaja Zanzibar.

Lissu ambaye ni Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amesema, “natamani kuwasaidia waondokane na adha hii, lakini sina namna nyingine zaidi ya hii.”

Akijibu swali kuhusu hatua ya wadhamini wake kumwandikia barua Mbowe, ili kuwasaidia kumshauri arejee nchini, amesema hakuna uhusiano wa Mbowe ama Chadema na kesi yake.

“Kuhusu kumwandikia Mh. Mbowe barua ya kumwomba ‘anirudishe’, sina hakika sana na busara au haja ya ombi hilo. Kisheria Mh. Mbowe na Chadema hawahusiki kwa vyovyote vile na kesi hii.

“Hii ni licha ya ukweli kwamba Mh. Mbowe na chama changu walifanya jitihada kubwa kunisafirisha nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, na licha ya ukweli kwamba mimi ni mwanachama na kiongozi mwandamizi wa Chadema.

“Barua hiyo haina uzito wala maana yoyote kisheria kwa sababu, masuala ya jinai ni ya uwajibikaji binafsi. Msalaba wangu wa kijinai, kama upo, hauwezi kubebwa na Mh. Mbowe au Chadema au na mtu mwingine yeyote,” amesema.

Pia mwandishi alitaka kujua namna Lissu atavyoweza kutumikia nafasi ya uenyekiti akiwa nje ya nchini, hata hivyo amesema dunia imefika mbali na hilo hakina tatuzo.

Amesema, kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliani (TEHAMA), kumesaidi kuhudumia mkutano Mkuu wa Chadema akiwa nje ya Tanzania.

“Kwa kiwango cha TEHAMA cha dunia hii ya sasa, inawezekana kushiriki shughuli nyingi za chama bila hata kwa kutoka chumbani kwangu hapa nilipo…., si nilichaguliwa Makamu Mwenyekiti baada ya kuhutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama chetu nikiwa huku nilipo?

“Hata kisheria, sheria zetu za sasa zinaruhusu kesi kuendeshwa kwa kutumia TEHAMA bila ulazima wa mashahidi kuwepo kimwili mahakamani. Ndivyo ilivyokuwa kwenye kesi ya jinai ya Profesa Costa Mahalu,” amesema.

Lissu alishambiliwa kwa risasi tarehe 7 Septemba 2017, akiwa nyumbani kwake eneo la ‘Area D’ jijini Dodoma na kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa huo.

Baadaye alihamishiwa Nairobi nchini Kenya, ambapo tarehe 6 Januari 2018, alipelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambapo yupo mpaka sasa.

error: Content is protected !!