ALIYEKUWA mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ametaka kuhakikishiwa usalama wake na serikali, ili aweze kurejea nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa chama cha Chadema (Bara) amesema, ataweza kurejea nchini mara moja, ikiwa atapa hakikisho la usalama wake kutoka kwa serikali.
“Nilisharejea nchini Agosti mwaka jana. Lakini nikalazimika kuondoka, baada ya kuwapo tishio jipya la usalama wangu,” ameeleza mwanasiasa huyo ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji.
Lissu alikwenda Ubelgiji kwa mara ya kwanza Januari 2018, baada ya kushambuliwa na kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana,” nyumbani kwake, Area D, mjini Dodoma.
Mara baada ya shambulio hilo, lililofanyika tarehe 7 Septemba 2017, Lissu alisafirishwa kwa ndege hadi katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako alipokea matibabu kabla ya kuhamishiwa Ubelgiji kwa matibabu maalumu.
Alirejea tena nchini humo, muda mfupi baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa 28 Oktoba mwaka jana.
Amesema, anahofia sana uamuzi wa kumuondolea walinzi wa usalama wake ambao alipewa mwaka 2020 alipogombea kiti cha urais, kwani uamuzi huo unatishia maisha yake.
“Baadaye nilikamatwa na kuachiliwa, kabla ya kukamilisha mchakato ambao uliniwezesha kutoroka nchi. Kwahiyo, ningependa kuwa na hakikisho katika suala hili kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan anafahamu hili vyema baada ya kunitembelea katika Nairobi Hospital,” alisema.
Akaongeza, “ninataka kujua watu waliojaribu kuniua, na usalama wangu nitakaporudi nyumbani. Je, hizo kesi za…zitaendelea na ikiwa nitaruhusiwa kushiriki katika siasa.”
Kwa mujibu wa maelezo yake, Lissu alifanikiwa kuondoka nchini, baada ya nchi wahisani kuingilia kati kwa kuiomba serikali ya Rais John Magufuli, kumruhusu kuondoka.
Mengine ambayo mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki, ameeleza kuwa anapenda yafanyike, ni kurejeshewa gari lake, ambalo alikuwa amelitumia siku aliyonusurika na risasi 16, mjini Dodoma.
Aidha, Lissu ametaka hakikisho la serikali kuwa itamlipa gharama za matibabu aliyotumia, mafao yake kama mbunge wa zamani na kuangaliwa upya kwa kesi zilizofunguliwa dhidi yake.

Kauli ya Lissu inakuja, wakati Rais wa Tanzania, Samia Suluhu, akiahidi kukutana kwa mazungumzo na viongozi wa upinzani.
Amesema, angependa kujua hatma ya mafao yake kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 wakati alipofahamishwa kuhusu kutostahili kwake kuwa mbunge wa Singida Mashariki.
Akiongea kwa hisia kali, Lissu alisema, “sijapokea malipo ya gharama za matibabu (kutoka kwa serikali). Hili Rais Hassan ambaye alinitembelea katika hospitali ya Nairobi Hospital analifahamu. Ninahitaji kujua ni kwanini sijalipwa.”

Msemaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania, David Misime amesema, uchunguzi juu kesi ya Lissu ulisimamishwa baada ya kukataa kujibu ombi la polisi la ushirikiano katika uchunguzi huo.
Akaongeza, “hawezi kukamatwa … lakini anapaswa kuripoti na kutoa maelezo.”
Leave a comment