December 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tundu Lissu aomba hifadhi Ujerumani

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Chadema

Spread the love

ALIYEKUWA mgombea urais wa Chadema, katika uchaguzi mkuu uliyopita nchini Tanzania, Tundu Antipas Lissu, amekimbilia nyumbani kwa balozi wa Ujerumani, jijini Dar es Salaam, “kuomba hifadhi ya maisha yake.” Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka kwa watu waliokaribu na kiongozi huyo zinasema, Lissu pamoja na baadhi ya wasaidizi wake, wapo nyumbani kwa balozi huyo, kufuatia kupokea vitisho lukuki vinavyolenga kuondoa uhai wake.

Lissu na baadhi ya wasaidizi wake, wamekuwa nyumbani kwa balozi wa Ujerumani, nchini Tanzania, tokea Jumatano iliyopita ya tarehe 4 Novemba, 2020.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, jana Alhamisi, Lissu amethibitisha kuwapo nyumbani kwa balozi huyo, na kwamba atakuwapo hapo hadi atakapohakikishiwa usalama wa maisha yake.

“Ni kweli kwamba niko nyumbani kwa balozi. Nimekuja kuomba hifadhi, ili kunusuru maisha yangu,” alieleza Lissu na kuongeza, kuondoka nyumbani kwa balozi huyo au kuendelea kuwapo kutategemea, hakikisho la usalama wake.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime

Alipoulizwa vitisho hivyo alianza kuvipokea lini, Lissu alisema, “nilianza kupokea vitisho vya maisha yangu, mara baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.”

Amesema, “baada ya vitisho kuzidi kuongezeka, nilitafakari kwa kina taarifa za vitisho hivyo, pamoja na taarifa kutoka kwa ‘wasamaria wema, ndipo nilipoamua kwenda kutafuta hifadhi ya muda sehemu nyingine tofauti na nyumbani kwangu.”

Taarifa zinasema, ikiwa Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema (Bara), atashindwa kuhakikishiwa usalama wake na vitisho hivyo vitaendelea, anaweza kufikiria kuondoka nchini kwa muda.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Lissu anapanga kuelekea nchini Ujerumani kwa ajili ya kutafuta hifadhi ya maisha yake na kujipanga upya kisiasa.

Lakini Msemaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania, Kamishena Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime, ameliambia MwanaHALISI Online kuwa jeshi lake, halina taarifa zozote kuhusu madai kuwa maisha ya Lissu yako hatarini.

Amesema, “jeshi linazungumzia kitu ambacho inakifahamu. Jeshi linazungumzia kitu ambacho kimetolewa taarifa. Hatuwezi kuzungumzia kitu ambacho, hakijatufikia. Hizo taarifa hatuna.”

Ameongeza, “hizo taarifa amezitoa lini? Sasa ungemuuliza yeye, maisha yake kama yako hatarini, ameripoti katika vyombo vya dola?

Kupatikana kwa taarifa kuwa maisha ya mwanasiasa huyo machachari wa upinzani nchini Tanzania yako hatarini, kunakuja miaka mitatu, tangu aliposhambuliwa kwa risasi na wanaoitwa, “watu wasiojulikana,” nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma.

Shambulio dhidi ya Lissu, lilifanyika mchana wa tarehe 7 Septemba 2017, wakati alipokuwa akirejea nyumbani, akitokea kwenye viwanja vya Bunge, kuhudhuria mkutano wa bunge la asubuhi.

Mara baada ya tukio hilo ambalo lilimjeruhi vibaya, mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki (Chadema), alisafirishwa hadi nchini Kenya kwa matibabu zaidi na baadaye nchini Ubelgiji.

Lissu alirejea nchini Jumatatu, tarehe 27 Julai 2020, kutokea nchini Ubelgiji na kujitumbukiza moja kwa moja kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Tanzania.

Katika uchaguzi huo, Lissu alitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kushika nafasi ya pili kwa kupata kura 1.9 milioni, huku Rais John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akitangazwa mshindi kwa kupata kura 12 milioni kati kura 15 milioni zilizopigwa.

Kwa upande wake, mshauri wa Lissu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho duniani, Emmaus Bandekile Mwamakula, amedai kuwa “maisha ya Lissu yako hatarini.”

Askofu Mwamakula amesema, ameongea na Lissu na baada ya kushauriana kwa kina, wamekubaliana kuomba hifadhi kwenye ubalozi huo.

Alisema, Lissu alikwenda ubalozi wa Ujerumani (Umoja House) tarehe 3 Novemba na akiwa nje ya ubalozi huo, kusubiri taratibu, Polisi walimkamata na kumpeleka makao makuu ya polisi, jijini Dar es Salaam.

Alihojiwa kwa takribani dakika 15 akituhumiwa kuitisha maandamano ya amani yaliyolenga kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba 2020, kinyume na kile kinachoitwa na polisi, “sheria za nchi.”

Anasema, “baada ya kutafakari kwa kina kuhusu hali halisi ya usalama wake katika mazingira ya sasa na baada ya kushauriana na wadau mbalimbali, imeonekana ni vema na ni hekima, Lissu kuendelea kuishi uhamishoni katika Ubalozi wa Ujerumani jijini Dar es Salaam hadi pale itakapoamriwa tena hapo baadaye.”

Askofu Mwamakula amesema, wanatoa wito kwa “watu wote walio nyuma ya mpango wa kutishia usalama wa maisha ya Lissu kwa kuelekeza, kufadhili, kutuma au kutekeleza mpango huo, kuacha mara moja kwa kuwa mkono wa Mungu na ulinzi wake upo pamoja na watu wasiokuwa na hatia.”

Baba Askofu Mwamakula anasisitiza hoa yake kwa kutumia maandiko matakatifu, akirejea Zaburi 35 na 121, pamoja na Ezekieli 33:1-20, kwamba kufanya hivyo, ni kutenda uovu.

Wakati Askofu Mwamakula anaeleza hayo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa anasema, jalada la tuhuma zinazomkabili Lissu na wenzake wawili, limepelekwa kwa mwendesha mashtaka wa Serikali kwa hatua zaidi.

error: Content is protected !!