Friday , 1 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Tundu Lissu amvaa Jaji Mutungi, ampa neno zito
Habari za SiasaTangulizi

Tundu Lissu amvaa Jaji Mutungi, ampa neno zito

Spread the love

MWANASHERIA wa Chadema na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi aache vitisho vya kuitisha chama cha Chadema na anatakiwa kujitafakari kwanza mwenyewe.

Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji kwa matibabu, ameandika waraka wake kumjibu Jaji Mutungi kufuatiwa barua yake aliyoiandikia Chadema ya kukituhumu chama hicho kufanya siasa za kibabe na vurugu na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa.

Waraka wa Lissu kwa Jaji Mutungi huu hapa chini

SAJILI MUTUNGI ASIITISHE CHADEMA, AJITAFAKARI

Nimesoma barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, yenye tuhuma na vitisho vingi dhidi ya CHADEMA.

Bila kutoa ushahidi wowote na kwa kutegemea taarifa za upande mmoja tu, Msajili Mutungi ameituhumu CHADEMA kwa kufanya siasa za kibabe na vurugu na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa.

Msajili Mutungi anastahili kujibiwa hadharani na kukumbushwa mambo kadhaa. Inaelekea amejisahau sana au anafikiria Watanzania ni wajinga wasioelewa mambo yake.

Msajili wa Vyama vya Siasa amekosa sifa na uadilifu (moral authority) ya kunyooshea kidole CHADEMA au chama kingine chochote cha upinzani kuhusiana na jambo lolote linahusu Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake.

Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, nchi yetu imeshuhudia ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Vyama vya Siasa ukifanywa na Magufuli mwenyewe, mawaziri pamoja na wateule wake wengine na Jeshi la Polisi.

Mikutano ya hadhara na maandamano ya amani, ambavyo ni haki ya vyama vya siasa kwa mujibu wa Sheria hiyo, imepigwa marufuku na Magufuli bila uhalali wowote. Msajili Mutungi hajawahi kukemea ukiukwaji huo wa sheria wala kutetea haki ya vyama vya siasa.

Viongozi wa vyama vya upinzani, hasa CHADEMA, wameuawa, wametekwa nyara na kupotezwa, wamepigwa risasi katika majaribio ya kuuawa, wameteswa, wamekamatwa na kushtakiwa kwa kesi za uongo.

Msajili Mutungi amekuwa bubu na kiziwi asiyesikia wala kukemea uonevu na ukandamizaji huu dhidi ya vyama anavyovisimamia.

CCM na serikali yake zimetoa hongo kurubuni madiwani, wabunge na viongozi wengine wa vyama vya upinzani kujiuzulu nafasi zao. Yote ni makosa ya maadili kwa mujibu wa sheria. Msajili Mutungi hajawahi kuliona hilo.

Polisi wameua mwanafunzi wa chuo aliyekuwa kwenye dala dala. Wamepiga risasi za moto na kujeruhi watu wengi bila sababu yoyote ya msingi.

Badala ya kukemea matumizi haya ya nguvu iliyopitiliza, Msajili Mutungi anaitishia CHADEMA iliyokuwa inadai haki yake ya kuwa mawakala kwenye vituo vya kura.

Tunajua kwa nini Msajili Mutungi hajawahi kuona makosa ya watawala wakandamizaji bali anaona makosa ya wanaokandamizwa tu.

Amefungwa macho na kuzibwa masikio na maboriti na mabanzi ya cheo chake. Ni msaka tonge anayejipendekeza kwa Magufuli ili aendelee kuwa kwenye nafasi aliyo nayo. Asitutishe.

Kwa vile anadai tumetenda makosa ya jinai, basi asubiri Mahakama zifanye maamuzi juu ya tuhuma hizi.

Yeye hawezi akawa mtoa tuhuma na jaji wa tuhuma hizo hizo. Nasikia amewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, anatakiwa kuyafahamu haya.

Sasa diwani wetu huko Kilombero ameuawa kinyama. Kwa vile ni wa CHADEMA, wauaji wake ni ‘watu wasiojulikana’ na Msajili Mutungi na Jeshi la Polisi watafanya kama walivyofanya kuhusiana na wale waliojaribu kuniua kwa risasi lukuki September 7 ya mwaka jana: Nothing!!! Tusubiri na tuone kama Msajili Mutungi atatoa kauli yoyote kuhusu mauaji haya ya diwani wa CHADEMA.

Katika mazingira haya ya uonevu na ukandamizaji mkubwa, ni vyema kujikumbusha maneno ya Nelson Mandela ya mwaka 1953:

“Hakuna njia rahisi ya ukombozi mahali popote, na itabidi wengi wetu tupite mara kadhaa katika bonde la uvuli wa mauti kabla hatujafikia kilele cha matarajio yetu.”

Tangu Magufuli aingie madarakani, ametuingiza katika bonde la uvuli wa mauti. Mauaji haya na ukandamizaji huu dhidi ya vyama vya upinzani ndio bonde la uvuli wa mauti lenyewe.

Tutalipita bonde hili mara kadhaa kabla ya kupata ukombozi wa pili wa nchi yetu. Lakini tutalivuka. Hii ndio gharama halisi ya ukombozi mahali popote na katika zama zote.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais Mwinyi kuzikwa Machi 2 visiwani Unguja

Spread the loveMWILI wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania,...

Habari za SiasaTangulizi

Rais mstaafu Mwinyi afariki dunia

Spread the loveRais Mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Ally Hassan...

Habari za Siasa

Waziri mkuu Ethiopia atua Tanzania

Spread the loveWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia,...

Habari za Siasa

Babu Owino: Vijana msibaki nyuma

Spread the loveMbunge wa Embakasi Mashariki nchini Kenya, Paul Ongili Owino maarafu...

error: Content is protected !!