RAIS wa chama cha wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu ameibuka na kusema, “vijembe vinavyorushwa na Ummy Mwalimu,” waziri wa afya na ustawi wa jamii, “vitajibiwa na mimi mwenyewe,” anaandika Saed Kubenea.
Akihutubia mkutano wa nusu mwaka wa mawakili nchini (AGM), kaka mkubwa wa Lissu, Alute Mughwai Lissu, ameeleza kuwa ameelekezwa na mdogo wake huyo, kutomjibu Ummy Mwalimu, badala yake kazi hiyo itafanywa na yeye mwenyewe.
Alute ambaye ni wakili wa kujitegemea anayefanya shughuli zake mkoani Arusha ameuambia mkutano huo, “nimeongea na Lissu leo saa nne asubuhi. Amenielekeza kuwa familia isijibu hoja za waziri Ummy Mwalimu.”
Amesema, “kazi hiyo itafanywa na yeye mwenyewe mara akataporejea nchini kutoka kwenye matibabu yake nje ya nchi. Ameahidi kuendeleza mapambano ya kudai haki bila kuchoka.”
Wakili Alute amesema, Lissu amemueleza kuwa “hatarudi nyuma katika harakati zake za kutetea haki na demokrasia nchini. Ameapa kupambana hadi tone lake la mwisho.”
Kwa mujibu wa Alute, afya ya Lissu inaendelea vizuri na anawashukuru madaktari wanaotibu kwenye hospitali ya Nairobi alikolazwa. Amewataka wajumbe wa mkutano huo kuendelea kumuombea.
Alute alikuwa akitoa salamu kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa TLS unaofanyika leo mjini Arusha.
Hii ni mara ya kwanza kwa Lissu kuzungumza kwa simu tokea aliposhambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika,” ambako alimiminiwa lundo la risasi zilizolenga kuondoa maisha yake.
Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Mnadhimu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni, alinusurika kifo, wiki mbili baada ya kunukuliwa akisema, “maisha yangu yako hatarini.”
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Dodoma na Nairobi, watu waliotaka kuondoa uhai wa Lissu, wanadaiwa kutumia magari mawili – Toyota Land Cruiser na Nissan Patrol.
Dereva wa Lissu ameliambia gazeti hili, “niliona ile Nissan ambayo ilibeba watu waliompiga risasi Lissu. Tulipoondoka maeneo ya viwanja bunge, lile gari lilitufuata njia nzima hadi nyumbani.”
Simon anasema, siku hiyo ya tukio, alimchukua Lissu nje ya geti la Bunge. Ametaja namba ya gari ambalo lilibeba “wauaji wa Lissu,” kuwa ni Nissan Patrol T 932 AKN.
Anasema, “…kulikuwa na magari mawili, ingawa moja lilionekana kukata njia nyingine, moja lilitufuata hadi nyumbani. Liliingia ndani ya geti la nyumba za Area D, ambako Lissu anaishi. Hilo ndilo lililobeba watu waliomshambulia Lissu kwa risasi.”
Anasema, “…jingine liliishia pale getini. Lililotufuata hadi nyumbani, liliegeshwa pembeni mwa gari letu. Akajitokeza mtu aliyekuwa ameketi kiti cha mbele cha abiria na kushusha kioo chake ili kutuangalia tuliomo ndani ya gari.”
Anasema, baadaye akashuka mtu kutoka kiti cha nyuma cha upande wa kushoto. Akajifanya kama anaongea na mtu kwa njia ya mikono. Lakini ukweli ni kuwa alikuwa anamchungulia Lissu kama yumo ndani ya gari.”
Anasema, baada ya muda mfupi akarudi kwenye gari, wakati huo dereva wa gari hilo alikuwa ameshaligeuza na kuliekeleza lilikotoka.
“Ghafla yule bwana akashuka na bunduki aina ya SMG ambayo niliiona wakati anafungua mlango. Akaanza kumimina risasi kwenye gari letu. Nilichokifanya ni kumlaza Lissu kwenye kiti cha dereva na mimi kuruka nje ya gari na kujificha mvunguni mwa gari jingine lililokuwa limeegeshwa kwenye uwanja wa nyumba za wabunge.” Haikufahamika gari hilo lilikuwa la nani.
Simon anasema, kabla ya urushaji risasi kuanza, Lissu alitaka kufungua mlango wa gari lake na kushuka ili aingie ndani ya nyumba yake. Lakini baada ya kumueleza kuwa gari lililopo pembeni limeanza kutufuatilia muda mrefu na hivyo asubiri kwanza, alikubaliana na ushauri huo.
Lissu alibaki kwenye gari lake kwa zaidi ya dakika 20 akiangalia nyendo za watu waliokuwamo kwenye gari lililokuwa linamfuatilia.
“Risasi zilipigwa mfululizo…Wakati nikiwa nimejiangusha kwenye mvungu wa gari, nilisikia yowe la Lissu mara moja, akiashiria kuwa risasi zilizokuwa zikirushwa zimempata,” anasimulia Simon.
“Nilimuona kabisa kabisa. Huyu mtu aliyekuwa anarusha risasi; ninamfahamu. Alikuwa amevaa kapero na miwani myeusi na kizubao… Ni yuleyule niliyekuwa nimekutana naye jijini Dar es Salaam,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Simon, tishio la uhai wa Lissu lilianzia Dar es Salaam walipokuwa wakijiandaa kwenda Dodoma. Anasema walipofika eneo la Tegeta, waligundua kuwapo kwa gari dogo aina ya Toyota lililokuwa likiwafuata.
Anasema, baada ya kugundua kuwa ni walewale waliokuwa wanawafuatilia siku zote, akaamua kuwakimbia. Waliacha njia ya kuelekea Bagamoyo na kufuata njia nyingine inayoelekea Mbegani.
Amesema, “hawa watu nilikutana nao kwa mara ya kwanza pale Rose Garden, Dar es Salaam. Walikuwa wamekaa pembeni mwa nilipoketi. Niliwatambua kwa kuwa walishuka kwenye gari ambalo lilikuwa linatufuatilia kuanzia mjini. Mmoja wa wale niliokutana nao Rose Garden alikuwa pia kwenye tukio lile la Dodoma.”
Akizungumza kwa hisia kali, Simon anasema, tukio hilo la kumfyatulia risasi mbunge huyo wa upinzani nchini, lilidumu kwa kipindi kifupi sana.
“Baada ya kusikika risasi nyingi zimepigwa kwenye gari la mheshimiwa Lissu, naona waliamini wamemuua na waliondoka kwa kasi kurudi mjini.
“Baada ya kuondoka, mimi nikatoka mvunguni mwa gari na kumkimbilia Lissu. Nikamuona bado anapumua. Nikapiga kelele kuomba msaada. Wakati huo, Lissu alikuwa anavuja damu nyingi mwilini mwake.”
Leave a comment