Spread the love
HATIMAYE yametimia. Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, ametinga mahakamani kupinga hatua ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kumvua ubunge wake. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Lissu, mmoja wanasheria mashuhuri nchini, amefungua shauri la kupinga kuvuliwa ubunge wake, kwenye Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, jana Jumatano, tarehe 7 Agosti 2019, chini ya hati ya dharura.

Ndugai alitangaza uamuzi wa kumvua ubunge Lissu, tardehe 28 Juni mwaka huu, wakati akiahirisha Mkutano wa 15 wa Bunge.

Katika uamuzi wake huo, Spika Ndugai alitaja sababu mbili: Kushindwa  kuhudhuria vikao vya bunge bila kutoa taarifa kwa maandishi kwa spika na kukaidi kujaza fomu ya taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma ya mwaka 1985.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, yuko nchini Ubelgiji anakopatiwa matibabu ya majeraha ya risasi, yaliyotokana na kushambuliwa na “watu wasiojulikana,” akiwa nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma, tarehe 7 Septemba 2017.

Shambulizi dhidi ya mwanasiasa huyo machachari nchini lilitokea wakati akirejea nyumbani kutokea kwenye ukumbi wa Bunge. Alikuwa amemaliza kuchangia mjadala wa asubuhi.

Katika shauri lake alilofungua mbele ya mahakama, Lissu kupitia kwa kaka yake, Alute Mughwai, anaomba Mahakama Kuu imruhusu kufungua shauri la kupinga kuvuliwa ubunge wake, kupitia utaratibu wa Judicial Review – mapitio ya maamuzi yaliyofikiwa.

Shauri hilo la kwanza la aina yake kufunguliwa nchini dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), limesajiliwa mahakamani hapo na kupewa Na. 18 /2019.

Mleta maombi – Alute Mughwai – kwa niaba ya ndugu yake – Tundu Athipas Lissu – anaiomba Mahakama Kuu isikilize maombi hayo ya awali na hatimaye imruhusu kufungua shauri la msingi, ili iweze kupata nafasi ya kuangalia uhalali wa maamuzi ya spika ya kumvua ubunge, kisha itengue na kutupilia mbali maamuzi hayo.

Aidha, Lissu anaiomba mahakama itoe amri ya muda ya kusimamisha kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo la Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu.

Mughwai anaeeleza katika hati yake ya kiapo historia mzima ya shambulizi dhidi ya Lissu, kuondoka kwake nchini kwa ajili ya matibabu na kusisitiza, “viongozi wote wa Bunge na Serikali, wanafahamu na  waliomtembelea akiwa kwenye matibabu jijini Nairobi, nchini Kenya na Ubelgiji.”

Katika maelezo yake, Alute anasema, Spika wa Bunge wakati akichukua uamuzi wa kumvua ubunge, hakumpa sababu za kufanya hivyo na kwamba Lissu alihukumiwa bila kupewa haki ya kusikilizwa.

Kuhusu madai ya kushindwa kuwasilisha tamko kuhusu mali na madeni, Alute anasema, Lissu alikuwa katika matibabu hospitalini nje ya nchi na kwamba spika alikuwa anatambua na au alipaswa kutambua hivyo kuwa alijeruhiwa vibaya wakati wa mapumziko ya vikao vya Bunge.

Anasisitiza kuwa katika muda wa miaka saba ya utumishi wake kama mbunge, alitekeleza wajibu wake kama mbunge; alitekeleza wajibu na majukumu yake kikamilifu kwa kuhudhuria vikao na kushiriki katika mijadala mbalimbalki ndani ya Bunge.

Anaiomba mahakama isikilize na kutoa maamuzi ya maombi yake haraka, vinginevyo Mtaturu ataapishwa kushika wadhifa huo.

Anasema, hatua yoyote ya kutosikiliza shauri lake kwa haraka, litamuathiri moja kwa moja kwa kuwa amepoteza haki zake zote, kinga na msilahi yake yanayoambatana na wadhifa wake wa ubunge.     

Mtaturu alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Singida Mashariki (DED), kuwa mbunge halali wa jimbo hilo, tarehe 19 Julai 19 mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *