Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Tunatafuta ‘suluhisho la mwisho?’
Makala & Uchambuzi

Tunatafuta ‘suluhisho la mwisho?’

Rais John Magufuli
Spread the love

WALE wanaozielewa siasa za Marekani kwa sasa, watakubali namna mabadiliko yanavyoibadilisha dola hii yenye nguvu kubwa zaidi za kiuchumi na kijeshi, anaandika Rashid Abdallah.

Marekani ya sasa inaongozwa na bilionea asiyeona tabu kuropokwa – Donald Trump aliyechaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Novemba 2016, akipitia Chama cha Republican.

Trump, tajiri anayemiliki majumba makubwa ya kibiashara, wakati mwengine hutangaza sera ambazo katika macho ya kawaida, zinajionesha wazi ni za kibaguzi.

Kule kulazimika kujipanga upya ndipo apitishe baadhi ya mambo aliyoyapanga, kunatosha kumuonesha alivyo mtu asiyeeleweka, asiye rahisi kuaminika, mwenye tambo na vituko. Wamarekani wanayo Marekani mpya chini yake.

Basi na hivi ndivyo ilivyo kwa Watanzania – wanayo Tanzania mpya leo, chini ya Rais John Magufuli. Ni dhahiri yapo wanayofanana.

Ukorofi wote alionao Trump, lakini hajathubutu kufungia vyombo vya habari ambavyo mara kadhaa amevituhumu kumsumbua.

Tanzania ni tofauti. Mwenendo wa serekali ni songombingo unapogusia hishima yake kwa vyombo ya habari. Inavitishia kila wakati; wahariri wake wakiambiwa wajitahadhari na wasidhani wanauhuru wa kiasi hicho.

Gazeti la MwanaHALISI linalochapishwa kila wiki na kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL), limefungiwa kwa miezi 24. Ni uamuzi mpya wa 19 Septemba 2017. Siku tisa hivi baadaye, likafungiwa la Raia Mwema kwa miezi mitatu.

Yawezekana kufungiwa kwa hili la pili ni mbinu tu ya kuzuga kwamba hakuna uonevu dhidi ya MwanaHALISI. Hebu angalia tu tofauti ya muda wa adhabu. Mbingu na ardhi.

Kupitia MwanaHALISI, umma unayajua mengi. Na haya ni mengi ambayo kama lingekuwa suala la hiyari, basi serikali isingeruhusu. Imezuia kikatili.

Lakini kufungia gazeti sio tu kunazibana sauti za watoa maoni, bali pia kumepeleka onyo kwa vyombo vyengine vya habari.

Kwamba mfungiaji anao uwezo wa kumshughulikia yeyote atakayeleta fyokofyoko kama anavyowashughulikia hawa; na sasa vyombo vingi vya habari vimepata hofu juu ya ukosoaji wa serekali.

Tanzania mpya ya Rais Magufuli anataka kuiunda kwa fito za khofu dhidi ya vyombo vya habari. Pia wale wapinzani wake kisiasa, nao hujazwa hofu katika majukwaa kwa kukemewa vikali.

Tayari hao walishazuiliwa kuhutubia kupitia mikutano ya hadhara, labda kwa masharti kadha wa kadha, yaliyo nje ya wigo wa sheria ya vyama vya siasa.

Kila mtu anatengenezewa hofu ya kuogopa kuisema, kuikosoa, kuipinga serekali. Watanzania wanaundiwa utawala ambao hawatothubutu kuusema, na wakiusema itakula kwao.

Wapinzani wake na wakosoaji wakubwa huwindwa hadi kwa risasi, lengo ni kuwanyamazisha mazima ili yale wayasemayo kwa serekali ya sasa wasiwe na uwezo tena wa kuyasema.

Wakati utawala wa Kinazi kule Ujerumani wanataka kuwaangamiza Mayahudi katika bara la Ulaya, waliketi chini na kutoa hitimisho waliloita kwa urefu “the final solution to the Jewish question.”

Kilichofuata ni mauaji ya maelfu ya Mayahudi katika njia za kutisha.
Yalikuwa ni mauaji ya kutisha yakiwemo mateso na hata gesi za sumu zilitumika kuhakikisha mradi wa suluhisho la mwisho unafanya kazi kama ulivyotarajiwa na waasisi wake.

Si lazima Tanzania kuwe na suluhisho la mwisho la namna hiyo, lakini haya maonyo na fungiafungia ya vyombo vya habari, inanipa hofu labda utawala umeamua kukaa kitako na kuja na suluhisho la mwisho kulenga vyombo vya habari vinavyoinua sauti ya ukosoaji.

Pia, napata hofu kwa ‘tekateka’ zinazotokea na mauaji yanayogonga mwamba, isijekuwa tumekaa kimya kumbe tayari suluhisho la mwisho dhidi ya upinzani limeanza kutekelezwa.

Kwa sababu hawa wanaoshambuliwa miili yao, ofisi zao, kwa risasi, kukamatwakamatwa na kutekwa, ukivuta taswira nyuma unagundua wanaolengwa ni watu wanaosimama upande tofauti na utawala.

Siombi kuwepo suluhisho la mwisho kwa makundi yote haya ya watu, lakini ikiwa tayari kuna suluhisho la mwisho maanake tutarajie mengine ya ajabu na kutisha yanakuja.

Manake kila utawala hutumia mbinu tofauti kupambana na wale wanaoamini ni maadui zao, wapo maadui wa msingi lakini kwetu ni maadui katika muktadha tu wa faida za kiutawala.

Katika nyakati hizi zilizojaa ubabe na uhuni, kila mwenye nguvu hufikiria kuanzisha suluhisho la mwisho kwa kinachomkera, ndio maana ulimwengu unashuhudia suluhisho la mwisho lililoanzishwa na serekali ya Kibudha dhidi ya raia wa kabila la Rohingya nchini Burma au Myanmar.

Na udhalimu huu ukiendeshwa chini ya serikali ya mwanamama Aung Sun Suu Kyi, aliyependwa kwa ujasiri wake wa kupambana na utawala dhalimu wa kijeshi na kuwa akiengwaengwa na kusaidiwa na jumuiya ya kimataifa chini ya mwamvuliwa Umoja wa Mataifa.

Nihitimishe kwa kusema ni jambo la ajabu ikiwa hofu ambayo imekusudiwa kupandikizwa mioyoni mwa wananchi itabebwa, kuanzia vyombo vya habari hadi wale wapinzani wa majukwaani.

Si lazima kukubaliana ya kila kisemwacho na wadau wa siasa lakini haiyumkini kuwaziba midomo eti kwa sababu wamesema usichokihitajia. Ni mambo ya kikoloni hayo, vyereje ulimwengu wa sasa?

Hakuna kunyamaza wala kuogopa hadi utawala utakapokubali haki ya kuwepo mawazo kinzani. Wakubali kuwa watakosolewa; na ni haki kwao kukosolewa kama ilivyo wajibu wa umma kukosoa wanaowaongoza.

‘Suluhisho la mwisho’ halikubaliki kwa kigezo chochote. Halikubaliki kuwa eti linalenga kuipa serikali nafasi ya kushughulikia maendeleo. Wajuzi wanaamini maendeleo huja kwa maoni tofauti ya wananchi, ikiwa na maana kuwapa uhuru wa kufikiri na kusema.
0657414889

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!