June 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tunasimamia uamuzi wa Chama – JUVICUF

Spread the love

JUMUIYA ya vijana ya Chama cha Wananchi CUF, (JUVICUF) imeunga mkono uamuzi wa chama hicho wa kupinga kushiriki uchaguzi wa marejeo kwa sababu CUF ilishapewa ridhaa halali ya kuongoza nchi na wapigakura wa Zanzibar. Anaandika Aisha Amran … (endelea).

Hayo yameelezwa leo na Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo, Mahmoud Mahinda katika tamko lake mbele ya waandishi wa habari aliokutana nao kwenye ofisi kuu za CUF Vuga, mjini Zanzibar.

Mahinda amesema viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatakiwa kuacha kung’ang’ania kuishinikiza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio kwa kuwa uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba ulikuwa halali mpaka kufikia hatua ya matokeo yake kutangazwa na Mwenyekiti wa Tume, Jecha Salim  Jecha.

Amesema CCM  ikubali ukweli kuwa vyama vingi vya siasa vimeletwa ili kupata ushindani utakaoleta mabadiliko ya utawala kulingana na matakwa ya wananchi ambao ndio wanaotoa mamlaka ya uongozi kwa vyama vya siasa.

Mahinda amesema kasumba wanayoieneza viongozi wa CCM kwamba uongozi wa serikali lazima ushikwe na CCM ni kuwadanganya wananchi.

“Tunamtaka Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kuwacha kutia ulimi wake puani badala yake asimamie maneno yake aliosema,” amesema na kuongeza:

“Utaratibu wa kukabidhiana madaraka ya nchi ni kufanya uchaguzi na aliyeshinda kukabidhiwa nchi.”

Mwenyekiti wa JUVICUF amesema Tume inatakiwa kurejea kazini na kumaliza kazi yake ya kutangaza matokeo kwa kura zilizobakia baada ya kazi ya kuhakiki kukamilishwa.

Amesema ni mtindo usiofaa kwa CCM kuwaaminisha na kuwachochea vijana kutafuta njia mbadala ya kuweka madarakani viongozi wasiochaguliwa na wananchi.

Aidha amesema kadri Tume inavyozidi kuchelewa kukamilisha kazi yake na kutangaza mshindi wa urais, ndivyo hali ya kisiasa inavyozidi kuwa ya mashaka. Amesema haiwezekani kuwa na nchi ambayo haina serikali halali iliyochaguliwa na wananchi kwa miezi mitatu.

“Gharama za maisha zimepanda, wananchi wamo katika mkorogo wa mawazo na usalama wao uko katika hali tete… makundi ya mazombi yaliyopewa baraka na viongozi wakubwa wa CCM wakiwemo walioko serikalini yanaendelea kuwahilikisha wananchi katika maeneo mbalimbali huku Jeshi la Polisi likikaa kimya na kuvifumbia macho vitendo hivyo vya kiharamia,” amesema Mahinda.

Mahinda amesema jumuiya yao inalaani vitendo vya kiharamia vinavyofanywa na vijana wanaofadhiliwa na CCM pamoja na lugha za kibaguzi zinazotolewa na makundi ya vijana wa CCM kama ilivyodhihirika mabango waliyobeba vijana kwenye matembezi ya mshikamano ya kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar.

Mahinda amesema lugha ya kibaguzi zimekuwa zikishuhudiwa kutolewa majukwaani na viongozi wa CCM wa ngazi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Mabango ya lugha za kibaguzi yamekuwa yakisomwa kwenye maskani za CCM za Muembekisonge na maskani ya Kachorora.

error: Content is protected !!