January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tunapunguza vifo vya mama na mtoto-Waziri

Dk. Seif Rashid-Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii

Spread the love

DAKTA Seif Rashid-Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, amesema siku ya maadhimisho ya wakunga duniani, yanatumika kuonyesha umuhimu wa wakunga katika kupunguza vifo vya mama na mtoto. Anaandika Sarafina Lidwino… (endelea)

Amesema kuwa pia wanafanya uhamasishaji wa watunga sera na watoa maamuzi ili kuhakikisha rasilimali muhimu zinakuwepo kwa ajiri ya wakunga.

Dk. Rashid ametoa kauli hiyo leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuelezea maadhimisho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya Mkendo, Manispaa ya Musoma mkoani Mara, ambapo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atakuwa mgeni rasmi.

Maadhimisho hayo hufanyika tarehe 5 Mei ya kila mwaka, na kuadhimishwa katika mikoa tofauti.

Akizungumzia maadhimisho hayo, Dk.Rashid amesema kuwa, siku hiyo hutumika kuonyesha umuhimu wa wakunga katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, pamoja na kufanya uhamasishaji wa watunga sera na watoa maamuzi ili kuhakikisha rasilimali muhimu zinakuwepo kwa ajiri ya wakunga.

Dk.Rashidi amesema pamoja na wakunga hao kutoa huduma za uzazi salama, pia hutoa ushauri nasaha na kufanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kuboresha huduma kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Mambo hayo yote yanaenda sambamba na mpango mkakati wa kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya mama na mtoto hapa nchini. Hivyo, tutaweza kufikia malengo ya maendeleo ya milenia namba 4 na 5 yanayohusu kuboresha afya ya mama kupunguza vifo vya wanawake vinavyotokana na uzazi,”amesema.

Ameeleza kuwa, kwa mujibu wa Shirikisho la Vyama Vya Wakunga Duniani (ICM), mkunga akitayarishwa vizuri na kufuata viwango vilivyowekwa na shirikisho hilo, na kuzingatia mahitaji ya nchi, anaweza kutoa asilimia 87 ya huduma zote anazohitaji mama na mtoto.

Kuhusu hali ya wakunga nchini, Dk. Rashid amesema, zaidi ya watu 10,000 wanaingia vyuoni kila mwaka na zaidi ya wakunga 8,000 wameajiriwa mwaka huu.

“Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika kupunguza vifo vya wazazi na watoto, na katika kuliunga mkono hilo, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu hospitalini pamoja na kuongeza zahanati za kutosha”.

“Napenda kutoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono maadhimisho haya, na kuwaomba wananchi hususani wa Musoma wajitokeze kwa wingi katika eneo husika ambapo kutakua na huduma mbalimbali zinazolenga kumuhudumia mama na mtoto,” amesema.

error: Content is protected !!