May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tunalidharau tatizo tunalolijua

Mwalimu Julius Nyerere

Spread the love

NI mshangao zaidi waliokuwanao kuliko walivyo na tabasamu na uchangamfu. Wananchi walichangamka lilipoanza gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama na pale iliposomwa hotuba ya rais, anaandika Jabir Idrisa.

Wananchi wenyewe walitoka majumbani kwao ndani ya jiji la Dar es Salaam, na mikoa ya jirani, kufika Uwanja wa Taifa (Uwanja wa Uhuru) ili kuungana na viongozi wao katika maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru.

Kutoikamilisha sentensi – kwamba uhuru wa nini – ndio hoja yangu hasa hapa. Harakaharaka linaibuka swali “wanaadhimisha miaka 55 ya uhuru gani?”

Hili swali linanirudisha kwenye ukumbi wa Kisenga, ndani ya Jengo la LAPF, Kijitonyama, Dar es Salaam, ambako wahariri chini ya mwamvuli wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), walikutana Alhamis ya 8 Disemba, kujadili hatima ya taaluma ya uandishi wa habari mbele ya sheria mpya iliyotungwa kusimamia sekta hiyo – Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016.

Katika mjadala wa eneo la kutumika kwa sheria hii, Salim Said Salim, mwandishi gwiji tangu enzi za Tanganyika Standard, alikuwa na maoni kwamba isidhaniwe sheria hiyo itatumika tu ndani ya mipaka ya “Tanzania Bara” ambayo yenyewe haijabainishwa wazi, kama ilivyoelezwa kwenye sheria yenyewe.

Anaona matumizi ya sheria inayoelekeza bayana kuwa itatumika tu kwa eneo hilo, huvuka mpaka na kutumika hata Zanzibar. Ana wasiwasi na hii mpya inayofuta ile ya Magazeti ya mwaka 1976, itatumika Zanzibar kwa sababu ya uzoefu uliopo hata kama kikatiba, suala la “habari” si katika mambo ya Muungano.

Alishawishi wahariri wenzake kuzingatia hoja hiyo kwa sababu, anasema, “nimepata kusema mara nyingi kuwa nipo tayari kuwagawia wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi karatasi mbili. Karatasi moja kila mbunge aandike mambo ya Muungano na nyingine mambo yasiyo ya Muungano. Nina uhakika nitapata majibu tofauti; hakuna anayejua kwa uhakika yepi mambo ya Muungano na yepi si ya Muungano.”

Asubuhi wakati stesheni ya televisheni ya Azam inarusha matangazo ya moja kwa moja ya sherehe za uhuru kutokea Uwanja wa Uhuru, nilikumbuka hoja hii ya nguli Salim. Kwenye uzi wa taarifa wa Azam TV, taarifa ilisema unaangalia matangazo ya moja kwa moja ya madhimisho ya miaka 55 ya Uhuru. Iliishia hapo. Hata mtangazaji wao, Nurdin Suleiman, kila alipofikia kutangaza sherehe hizo ni za nini, aliishia hapohapo “miaka 55 ya uhuru.” Hakuongeza neno.

Lakini alipochukua nafasi ya kutangaza, Shaaban Kisu, mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), yeye alisema sherehe za maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Mtangazaji wa ratiba ya sherehe iliyoanzia na kuwasili uwanjani kwa viongozi kulikohitimishwa na kufika kwa Rais John Magufuli, yeye hakuwa na kauli moja. Mara alisema miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara, mara uhuru wa taifa letu la Tanzania.

Angalia zaidi hii picha. Chukua hata sasa gazeti la Mwananchi la 9 Disemba na usome matangazo ya biashara yaliyokuwa na maelezo ya kumpongeza Rais na Watanzania kwa ajili ya sherehe hizi. Utayakuta matangazo 12 lakini kuna maelezo yanayotofautiana kuhusu suala hili. Cha kushangaza zaidi, ni tofauti hiyo kuikuta hata kwa matangazo yaliyodhaminiwa na taasisi za kiserikali – mashirika ya umma.

Lakini kinachoshtua zaidi na zaidi, ni kutofautiana kwa matangazo mawili yaliyoandaliwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Katika tangazo lililochapishwa na Mwananchi, ukurasa wa 33, imeelezwa ni maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa “nchi yetu.”

Bali katika tangazo la shirika hilihili kwenye ukurasa wa nne wa gazeti la Nipashe la siku hiyohiyo, Tanesco wanasema “miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara.” Gazeti lenyewe hilo, katika tahariri yake, limesema miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Hata Mwananchi hawakuwa na kauli moja. Maelezo yaliomo kwenye tahariri yake, yanasema “wananchi wa iliyokuwa Tanganyika” na mbele kuendelea kusema uhuru wa taifa letu, pia uhuru wa nchi yetu. Lakini wakati tahariri yenyewe imebebwa na maneno “Hongera Tanzania kutimiza miaka 55 ya Uhuru,” gazeti hilo katika ukurasa wake wa sita, limechapisha tangazo ukurasa mzima na maelezo kuhitimishwa kwa “…inaungana na Watanzania wote katika kusherehekea maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara.”

Matangazo ya pongezi ya watangazaji wengine ndani ya Mwananchi yanasomeka: Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), ukurasa wa 15 wanasema “Uhuru wa Tanzania Bara.” Mfuko wa Mafao ya Kustaafu wa GEPF, ukurasa wa 28 wanasema “Uhuru wa Tanganyika,” Shirika la Taifa la Bima (NIC) wamekwepa kutaja. Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART) wanasema “Uhuru wa Tanganyika.”

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) tangazo lao katika ukurasa wa 30 wanasema “Uhuru wa Tanzania” wakati Halmashauri ya Manispaa ya Temeke katika tangazo lao ukurasa wa 31, wanasema “Uhuru wa Tanganyika” huku wenzao wa Halmashauri ya Temeke, kwenye ukurasa huohuo wakisema, “Uhuru wa Tanzania Bara.” Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) tangazo lao katika ukurasa huo wa 31 wanasema, “Uhuru wa Tanzania Bara.”

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni tangazo lao ukurasa wa 33, wanasema “Uhuru wa Tanzania Bara” wakati Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwenye tangazo lao lililochapishwa ukurasa wa 34, wanasema “Uhuru wa Tanzania Bara.”

Nikiwa maeneo ya karibu na ofisini kwetu mtaa wa Kasaba, Kinondoni, nilipata majibu tofauti kwa watu kadhaa nilipowauliza kuhusu suala hili. Wengine walisema Uhuru wa Tanzania, wengine uhuru wa Tanzania Bara, wapo waliosema uhuru wa Tanganyika. Bali mmoja ambaye aliyesema nimemuuliza swali la kizushi, alisema, “Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Basi hii ndio kadhia ya utata uliopo kuhusu Watanzania inapofika siku hii ya 9 Disemba, huwa wanaadhimisha siku ya uhuru wa nchi ipi au taifa lipi.

Utata huu una maana kwamba mpaka leo, miaka 55 tangu Tanganyika ilipotangazwa nchi huru, imeshindwa kuwafundisha raia zake historia sahihi ya nchi yao kuhusu eneo hili. Hawajaambiwa Tanganyika ni nini, ipo au haipo, kwa maana inaishi walipo leo au imekufa. Kama inaishi iko wapi leo, na kama ilikufa ilikufaje.

Ni utata unaoendelezwa na viongozi waliopo. Hawataki kusema ukweli. Kwa bahati mbaya hata waliopitia Chuo Kikuu wanatofautiana kujibu swali hili. Angalau ninajua unapouliza swali hili kwa Mzanzibari, anajibu pasina kusita, hii miaka 55 ni ya “Uhuru wa Tanganyika.”

Sikusudii kueleza kwenye nafasi hii ni kwanini hali iko hivi. Niseme tu Watanzania tunalo tatizo kubwa ila tunalidharau kwa kuamini ndivyo alitaka muasisi Mwalimu Julius Nyerere.

error: Content is protected !!