July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tunajadili bila hatua, tunaangamia

Wanafunzi wakiwa darasani

Spread the love

MOJA ya nchi yenye mfumo bora katika elimu ni Indonesia. Kila mwaka hutenga zaidi ya asilimia 21 katika elimu peke yake. Anaandika Yusuph Katimba…(endelea).

Sisi Tanzania, sekta ya elimu bajeti yetu inacheza kwenye asilimia 5 – 7 ya bajeti yetu kuu. Kwa maana nyingine tena, wenzetu ambao miaka ya 1950 na 1960 uchumi wetu na wao ulilingana, leo wao wanawekeza katika elimu mara tatu kuliko tunavyofanya sisi.

Na kwa mtindo huu, hatupaswi kushangaa tunapoona shule ya msingi huko Manyara, au huko Tarime au Sumbawanga, ikiwa na mwalimu mkuu mmoja akiwa ndiye wa zamu, ndiye wa taaluma, ndiye wa nidhamu na ndiye mlezi wa shule.

Mwalimu huyo huyo mmoja aliyebobea katika Hisabati na Sayansi, ndiye anawafundisha watoto wetu Jiografia, Kiingereza, Uraia, Kiswahili na Maarifa ya Jamii.

Hizi nchi Indonesia, Singapore, Malaysia na zingine zilikuwa na uchumi duni kama Tanzania miaka 50 iliyopita, kulikoni leo wenzetu wametuzunguka mara 11 mara 10 mara 5, wakati wanakimbia namna hii sisi tuko wapi?

Wakati shule zetu za msingi hazina walimu, za sekondari vivyo, bado hao walimu waliopo hawana nyenzo za kufundishia, hawana nyumba za kuishi, hawana usalama wa kutosha, hawalipwi mishahara ya kutosha na inayotia aibu.

Haya yanatokea wakati serikali haikosi fedha za kusafirisha misafara ya viongozi kwenda kwenye ziara kila kukicha kwa kutumia mabilioni ya fedha za walipa kodi masikini.

Elimu ya nchi yetu hivi sasa haina mwenyewe, dira ya elimu ya taifa haipo, udhibitiwa viwango vya mitaala haupo, maamuzi makubwa ya kielimu yanafanywa kiholela tu. Ukichanganya na ukosefu wa uwekezaji wa kutosha katika elimu, tunajikuta hatujui tunachofanya.

Nchi zilizowekeza vilivyo katika elimu kupitia bajeti za serikali zao, zimeweza kukuza viwango vya ubora wa elimu, vimeweza kuimarisha mitaala ya elimu zao ili ijikite katika kuwapa wanafunzi mafunzo stahiki na uwezo wa kubuni fursa za ajira na kujiajiri.

Nchi zilizowekeza katika elimu, zimeweza kujenga msingi wa  uhusiano kati ya elimu na uchumi wa nchi zao na kwa kufanikisha hilo viwili hivyo vinashirikiana kuitoa nchi husika katika umasikini.

Nchi inapokuwa na vijana wengi waliopata elimu bora na iliyowaandaa vyema, inakuwa na vijana ambao wanajua namna ya kujiajiri, namna ya kusimamia ujasiriamali mdogo na kuukuza hadi kuwa biashara kubwa, namna ya kukusanya mapato na kuyatrunza vyema na kuyatumia kwa manufaa.

Nchi ambayo haijawapatia vijana elimu bora, hawawezi kuwa na uwezo mzuri na uelewa wa masuala yote hayo ambayo ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na kutokomeza umasikini.

Vijana wapokuwa na nidhamu na kiu za kujiajiri na kukuza vyanzo vya ujasiriamali, wanakuwa na uwezo mkubwa wa kujiweka huru na kujenga fikra sahihi za kuelekea katika mafanikio.

Kwa sababu, uchumi imara katika nchi unapaswa kulindwa, mfano mdogo ni pale unapokuwa na kilo 10 za dhahabu zenye thamani ya mabilioni ya pesa.

Dhahabu hizo ukizigawa kwa kijana aliyesoma na kuelimika vema, na zingine kwa kijana ambaye hana elimu kwa usawa, kwa kiasi kikubwa baada ya muda fulani kuna uwezekano mkubwa huyu ambaye ni “mbumbumbu” akawa aliishia kuzitapanya.

Na pia anaweza asipate faida nazo ndani ya muda mfupi, wakati kuna uwezekano mkubwa sana kwa huyu mwenye elimu kuziwekeza na kuzizalisha.

Mfano huu siyo mzuri sana kwa sababu vijana wengi waliosoma na kupata elimu ndani ya Tanzania hawaandaliwi kujitegemea, kujiajiri au kujisimamia.

Mitaala yetu ya elimu, uwekezaji katika elimu na namna tunavyofundishwa, haitoi fursa kwa vijana wengi kujengewa fikra huru mbele ya safari.

Ndiyo maana nikasema, mfano huo wa dhahabu unaweza kuwa si sahihi sana kwa sababu hata huyu kijana msomi, bado mwisho wa siku atatapanya kilo tano za dhahabu japo kwa kuchelewa kidogo, na sababu nimeieleza, naye hakupewa msingi wa elimu ya kujitegemea kifikra, kiubunifu, kiuelewa na kujiamini.

Nchi inapokuwa na vijana wanaoweza kutapanya kilo tano za dhahabu na kesho yake wakawa masikini wa kutupwa, ni nchi ambayo imeambukizwa ugonjwa mbaya.

Ugonjwa huu pia unatumika katika masuala makubwa yanayoweza kuimarisha au kufifisha na kutikisa uchumi wa nchi.

Ikukumbukwe kuwa, kama tuna vijana wengi ambao wamesoma lakini hawajaelimika, na hawawezi kujitegemea kielimu huku wengi zaidi wakiwa hawana elimu kabisa, uwezekano wa kuwa na viongozi wa nchi ambao hawana fikra huru, wasioweza kujiamini, wasioweza kujisimamia na kufanya majukumu yao na wasiotambua wajibu wao ni mkubwa mno.

Viongozi wa namna hii ndiyo walewale walipokuwa vijana wakapewa kilo tano za dhahabu na wakazitapanya, na ndio haohao ambao leo watashushiwa neema ya trilioni na trilioni za kilo za ujazo za gesi na mafuta na bado wakavitapanya visilisaidie taifa lao masikini.

Ndiyo maana tokea awali nimesisitiza kuwa, kuna uhusiano mkubwa sana katika ya elimu na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Nchi ambayo inawezekeza asilimia nne tu ya bajeti yake kwa mwaka kwenye elimu, haiwezi kuwa na raia wenye uelewa kutosha kulinda na kukuza uchumi wa nchi yao ili tena uchumi huo uwekezwe katika elimu kwa mapana.

Tanzania imekuwa ikifanya makosa makubwa kwa kuichezea elimu, tumekuwa hatuna mipango ya muda mrefu katika elimu.

Kila jambo linafanywa kuwa zima moto tu, matokeo yake tuna elimu inayoongoza kwa kutoa vyeti badala ya ufanisi, matokeo yake tutakuwa na wachumi ‘feki” wa daraja la kwanza.

Tunakuwa na wahandisi feki ambao hawakufundishwa na kuivishwa vya kutosha, tunakuwa na walimu wasiojua wajibu wao na waliokata tamaa, tunakuwa na viongozi ambao wao “wanajua kutapanya” tu, na siyo kutumia kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.

Kuna ule msemo unaosema, ukiona elimu ni gharama jaribu ujinga. Ujinga una gharama kubwa mno. Taifa lililojaa watu wasiojitambua, linaweza kufanya mambo ya ajabu kwelikweli.

Nakumbuka hadithi ya “Kikombe cha Babu Loliondo” na namna nchi ilivyogeuka yote na kuimba wimbo wa babu wa Loliondo.

Kikombe cha babu ungedhani kimewabeba raia tu wasiojua mambo mengi, kiliwabeba hadi mawaziri na hadhi na heshima zao wakatumia fedha za umma, wakakodi mahelkopta na kwenda Loliondo kunywa Kikombe cha babu.

Hawa ni mawaziri ambao walikuwa na wajibu wa kuwahimiza wananchi kuamini huduma za afya zinazotolewa na wataalamu wa afya na hospitali zetu, ndio walioongoza kwenda kwa babu.

Wapo walioacha matumizi ya ARVs, kwa sababu ya kikombe cha babu, kiwango hiki cha ujinga kilitokana na mitaala mibovu. Hivi karubuni mjadala wa elimu ujuzi ulishika kasi, lakini sasa tuliiii. Tuanzie hapo kuokoa taifa letu.

error: Content is protected !!