August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tunahitaji sheria isiyonyamazisha wananchi

Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Spread the love

KAMATI za Kudumu za Bunge la Jamhuri zinaanza vikao vyake leo Jumatatu mjini Dodoma. Mikutano ya Kamati ni mahususi kwa wabunge kupata fursa ya kukutana na serikali na wadau kupitia miswada ya sheria inayowasilishwa bungeni kwa lengo la kupokea maoni na, au ushauri, anaandika Saed Kubenea.

Miongoni mwa yanayoweza kujadiliwa katika mkutano huu, ni pamoja na muswada mpya wa Sheria ya Huduma za Habari – The Media Services ACT (2016).

Muswada wa Huduma za Habari ulisomwa kwa mara ya kwanza kwenye mkutano wa nne wa Bunge la 11, Alhamisi 15 Septemba 2016. Utafikishwa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii.

Tayari baadhi ya wadau wakiongozwa na Umoja wa Muungano wa Klabu za waandishi wa Habari (UTPC), wamepaza sauti kuitaka serikali kuongeza muda wa wadau kutoa maoni.

Hii ni kwa sababu, ndani ya muswada kumesheheni vifungu vinavyoweza kuwa kitanzi kwa waandishi wa habari; wamiliki wa vyombo vya habari; wachapishaji; watangazaji na wasambazaji.

Ndani ya muswada kumewekwa vifungo kwa waandishi wa habari, wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari, wachapishaji na watangazaji.

Kumewekwa faini za mamilioni ya shilingi kwa waandishi, watangazaji, wapigapicha na wakurugenzi wa kampuni au mashirika yanayojihusisha na utoaji habari na vyombo vya habari.

Kumewekwa mamlaka kwa jeshi la polisi, kufunga sehemu ya mtambo wa uchapaji au mtambo wote, wakati shauri dhidi ya mchapishaji, mwandishi, mhariri, mmiliki au mkurugenzi, linaposubiri kumalizika mahakamani.

Muswada umetoa kinga kwa ofisa wa polisi kutoshitakiwa kwa lolote atakalolitenda wakati anatekeleza jukumu hilo. Hataweza kushitakiwa kwa jinai wala madai.

Kifungu cha 50 (8) cha muswada kinasema, mahakama itakuwa na uhuru wa kutoa amri ya kuiruhusu serikali kuchukua mashine ya kupigia chapa au kutangazia, mara itakapojiridhisha kuwa mashine hiyo imetumika kupigia chapa gazeti au kutoa chapisho linalochochea uasi.

Aidha, kifungu cha 50 (9) (a) na (b) cha muswada kinatoa mamlaka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), “kwa ridhaa yake anaweza katika hali yoyote ile,” kuagiza yafuatayo kwenye mashine iliyochukuliwa na serikali:

Kuondoa sehemu yoyote ya mshine hiyo; kuzibwa sehemu fulani ya mashine; na au kufunga baadhi ya sehemu ili kuzuia isitumike.

Kwamba IGP wakati akitekeleza madaraka yake hayo, hatahesabiwa hatia kwa hasara yoyote itakayotokea kwenye mashine za kuchapia ambazo ziko chini ya uangalizi wake.

Kifungu cha 50 (11) kinasema, mtu yeyote atakayetumia au kujaribu kutumia mashine ya kupigia chapa iliyochukuliwa na serikali kwa mujibu wa kifungu cha (4) atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyopungua Sh. 15 milioni au kutumikia kifungo kwa muda usiopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Mtu yeyote anayechapisha gazeti kwa kukiuka amri iliyotolewa chini ya kifungu kidogo cha (6) anatenda kosa, na akitiwa hatiani atatozwa faini isiyopungua Sh. 5 milioni na isiyozidi Sh. 10 milioni au kutumikia kifungo kisichopungua miaka mitatu na kisichozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja.

Yule atakayetengeneza au kueneza taarifa yoyote ya uongo, uzushi au taarifa ambayo yaweza kuwatia watu woga na wasiwasi au kuchafua amani katika nchi atakuwa ametenda kosa.

Huyo akipatikana na hatia, atatozwa faini isiyopungua Sh. 10 milioni na isiyozidi Sh. 20 milioni au kutumikia kufungo kwa muda usiopungua miaka minne na isiyozidi miaka sita au vyote kwa pamoja.

Kifungu cha 51 (2) kinaeleza kuwa ni utetezi kwa kosa lililoanzishwa chini ya kifungu kidogo cha (1), endapo mshtakiwa atathibitisha kwamba kabla ya kutangaza au kueneza habari hatua madhubuti za kuhakikisha ukweli wa jambo hilo na kwamba matokeo yake yalimfanya asadiki kwamba habari au taarifa hiyo ilikuwa ya kweli.

Hata wakurugenzi wa makampuni, vyama vya hiari na vyama vya siasa, hawakuachwa nyuma na kitanzi cha sheria hii.

Ibara ya 52-(1) inasema, pale ambapo kosa litatendwa na kampuni, shirika hodhi, chama, umoja au kikundi cha watu basi kampuni hiyo au shirika hilo hodhi, au chama, umoja au kikundi hicho cha watu ila mtu ambaye wakati wa kosa hilo lilipotendeka alishiriki au kuhusika, kama mkurugenzi au afisa katika uongozi au uendeshaji wa kazi na shughuli za taasisi hizo, atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atatozwa faini isiyopungua Sh. 15 na isiyozidi Sh. 25 milioni.

Naye waziri anayehusika na habari, anapewa mamlaka chini ya kifungu cha 54 cha sheria, kupiga marufuku uingizaji wa chapisho lolote nchini ambalo kwa maoni yake, ni kinyume na maslahi ya umma.

Anakuwa na mamlaka ya kuzuia uchapishaji au utangazaji wa maudhui yanayohatarisha usalama wa taifa au afya ya jamii.

Kifungu cha 56 cha sheria kinampa mkurugenzi wa habari, afisa wa polisi au afisa yeyote muidhiniwa uwezo, ikiwa ana sababu za msingi na kuamini kuwa chombo cha habari kimeanzishwa au kinaendeshwa kinyume na sharti ya sheria hii, kutwaa kifaa chochote ambacho kimetumika au kitatumika kwa madhumuni hayo.

Kifungu cha 57 (1) kinasema, amri au maelekezo yatakayotolewa na Bodi au Idara ya Huduma za Habari, hayalazimiki kutangazwa katika gazeti la serikali, amri au maelekezo hayo yatawasilishwa kwa wahusika watakaoathirika na amri au maelekezo hayo kwa namna yoyote itakayoamriwa.

Kifungu cha 57 (2) kinasema, kama amri au maelekezo hayo yatatangazwa katika gazeti la serikali, watu wote wanaohusika watahesabiwa kuwa wana taarifa husika.

Mtu ambaye bila ya kuwa na sababu zinazokubalika kisheria atashindwa au kukataa kutekeleza maelezo halali ya bodi; ataizuia kutekeleza mamlaka yake; atatoa taarifa au tamko kwa bodi huku akijua kuwa taarifa hizo ni za uongo au za kupotosha kwa namna yoyote ile, na au.

Akiitwa mbele ya Bodi kwa mahojiano na akatoa taarifa huku akijua kuwa taarifa hizo ni za uongo au kupotosha kwa namna yoyote ile, atakuwa anatenda kosa na akitiwa hatiani chini ya kifungu hiki atatozwa faini ya shilingi milioni tano au kifungo cha mwaka mmoja au vyote kwa pamoja. Rejea kifungu cha 59 (1).

Mtu atakayekutwa na hatia chini ya kifungu hiki kwa kosa jingine linalojirudia atatozwa faini isiyopungua Sh. 10 milioni au kutumikia kifungo cha miaka saba.

Kuanzia kifungu cha 60 (1) na 60 (2), vinapendekeza kutoa mamlaka waziri kutunga kanuni kwa ajili ya utekelezaji bora wa masharti ya sheria hii.

Kifungu cha 60 (2), kinaeleza kuwa waziri aweza kutengeneza kanuni kwa kutumia “vigezo na masharti ya leseni ya vyombo vya habari; utoaji wa leseni ya mapachapisho na masharti ya umiliki wa hisa kwa vyombo vya habari vya kigeni.”

Aidha, masharti mengine, ni utoaji wa adhabu, utayarishaji wa taratibu za kuthibitisha waandishi wa habari; utayarishaji wa taratibu za utoaji kitambulisho cha mwandishi wa habari na utoaji taarifa za vyanzo vya mapato kwa vyombo vya habari na vyama vya mwanahabari.

Kupitia muswada mpya wa Sheria ya Huduma za Habari, sheria ya magazeti ya mwaka 1976 na sheria zinazounda Shirika la Habari Tanzania, zitakuwa zimekufa.

Hata hivyo, ukisoma kwa makini muswada uliosomwa bungeni, utaweza kuona kuwa mengi ya yaliyokuwamo kwenye sheria katili ya magazeti, yamerejeshwa kwa mlango wa nyuma katika muswada wa Huduma za Habari.

Kama ilivyo kwenye sheria katili ya magazeti – Newspapers Act 1976 ambapo serikali ndiyo inashitaki na ndiyo inayohukumu – ndani ya sheria mpya serikali imeunda bodi na kuibebesha jukumu hilo.

Bodi imesheheni waajiriwa wa serikali na wateule wa waziri. Inafanya kazi kwa maelekezo ya serikali. Ni mvinyo wa kale kwenye chupa mpya.

Kwa muktadha huo, sheria katili ya magazeti ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa miaka zaidi ya 50 na waandishi wa habari na wadau wa habari, bado ingali hai. Haijafutwa.

Watawala wanaonekana bado wanahitaji sheria hii kuitumia kunyang’anya uhuru wa wananchi wa kufikiri na uhuru wa kutoa maoni na kuwasiliana.

Sheria za sasa zinampa mamlaka waziri kuwa mhariri kwenye chombo cha habari na papo hapo, kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka na jaji.

Sheria mpya inayotaka kupitishwa bado imeacha mamlaka hayohayo, lakini safari hii kupitia kinachoitwa, “Bodi ya Wahariri.”

Ni kinyume na ibara ya 18 kifungu cha 26 (1) na cha (2) na kifungu cha 30 (1) na cha 8 (2) (a)-(e) cha Katiba ya Jamhuri (mwaka 1977).

Inaeleza, “kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake; na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

Muswada mpya unakwenda kinyume na matwaka ya raia ya kuwa na haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.

Muswada waweza kuwa ni kinyume cha Ibara ya 19 ya Agano la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1966 na Ibara ya 6 ya Agano la Fungamano la Afrika Mashariki.

Muswada waweza kuwa kinyume cha Ibara ya 8 ya Agano la Haki za Binadamu na watu la Afrika la mwaka 1981.

Hivyo basi, ni muhimu kwa wananchi kuusoma kwa makini muswada ulioko mbele ya Bunge ili kuhakikisha uhuru na haki ya kutafuta na kusambaza habari, haiporwi kupitia njia hii.

Nchi hii ni yetu sote. Tusiruhusu wachache wakaturejesha au kutubakiza gizani.

Sheria inayohitajika nchini, siyo ya kuwatia wananchi hofu na kuwanyamazisha waandishi, wapigapicha, wamiliki na wachapishaji.

Wananchi wanahitaji sheria inayolinda na kutetea uhuru wao. Ni vema muswada wa Sheria ya Huduma za Habari – The Media Services ACT (2006), ukamalizika na kupitishwa bungeni kwa kutufikisha huko.

 

error: Content is protected !!