August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tumuamini JPM au gavana?

John Magufuli, Rais wa Tanzania

Spread the love

RAIS John Magufuli, akiwa katika mahafali ya Chuo Kikuu Huria (OUT), eneo la Bungo, Kibaha, Pwani, alitumia nafasi hiyo kuelezea sababu za kutengua uteuzi wa mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Kodi (TRA), Bernard Mchomvu na kuvunja bodi yake, anaandika Shabani Matutu.

Bodi hiyo iliyokuwa na wajumbe tisa, kati yao watano wanaingia kwa mujibu wa sheria na wanne ni wa kuteuliwa.

Wajumbe waliokuwa wakiingia kwenye bodi hiyo kwa mujibu wa sheria ni Gavana wa BoT, Kamishna Mkuu wa TRA; Katibu Mkuu Wizara ya Fedha wa Jamhuri ya Muungano; Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar na Katibu Mkuu Mipango.

Rais Magufuli alisema kuwa Bodi ya TRA iliyokuwa na watendaji hao wakuu wa idara na taasisi za serikali, ilifanya dhambi ya kuidhinisha uamuzi wa manejimenti kuweka mabilioni ya shilingi katika benki za binafsi.

Katika maelezo yake,Rais Magufuli alisema alishawishika kufanya hivyo baada ya kukuta kiasi cha Sh. 26 bilioni zilizokuwa zimetolewa kwa matumizi ya TRA, kuhifadhiwa kwenye benki tatu.

Akadaifedha hizo katika akaunti ya TRA, zimekuwa zikitolewa, lakini baadaye zinachukuliwa, jambo ambalo alilitilia shaka na kuona kutokuwepo kwa uaminifu,hivyo ikambidi kuchukua uamuzi wa haraka kuvunja bodi hiyo ili uchunguzi ufanyike.

Rais Magufuli pia akailalamikia Mamlaka ya Elimu (TEA) kwakuwa miongoni mwataasisi zinazoingiza fedha zake katika akaunti za muda maalum.

Sakata hilo la kuweka fedha katika akaunti maalumu, kwenye benki za biashara, Prof. Benno Ndullu ambaye ni mjumbe wa bodi hiyo aliyekuwa akiingia kwa kutumia nafasi yake kwa mujibu wa sheria.

Prof. Ndullu alibainisha kwamba hakuna hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti maalum, isipokuwa hilo suala lilikuwa na hali nyingine.

Anasema “suala linalozungumzwa kwamba kuna athari za kiuchumi kwa taasisi za umma kuweka fedha kwenye akaunti maalum, tena za benki binafsi ni mbaya hilo si kweli”.

Akielezea namna mabenki yalivyokuwa katika wakati mgumu kujiendesha, alisema kwa sasa faida za mabenki zimeshuka, ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, hatua inayotatiza utoaji wa mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji nchini.

Lawrence Mafuru, Msajili wa Hazina, ameeleza kuhusu uamuzi wa watumishi wa umma kuweka fedha kwenye akaunti ya muda maalumu, akisema ni salama Zaidi.

Kauli yake imetofautiana na maelezo ya Rais Magufuli aliyosema kwamba uamuzi wake wa kuivunja Bodi ya TRA, umetokana na chombo hicho kuidhinisha uamuzi wa TRA kuweka fedha kwenye akaunti za muda maalumu kwa lengo la kujinufaisha.

Hapa najiuliza nani anatakiwa kuaminiwa je, ni hawa wataalamu wawili wanaosema kuweka fedha za umma katika akaunti ya muda maalimu si kosa kisheria na ni salama kwa sababu si rahisi fedha kuibwa kwa sababu miamala ya benki ni ya uwazi au Rais Magufuli anayesema ni kosa na si salama kwa sababu zinanufaisha watu binafsi?

Nani tumuamini kati ya Rais Magufuli anayesema kuweka fedha hizo katika akaunti ya muda maalum ni hasara kuchumi au Profesa Ndullu, kiongozi mwenye dhamana ya fedha za Watanzania, anayesema hakuna hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti hiyo?

Je, tumuamini Magufuli anayesema kwamba kuna wizi unaofanyika kwenye akaunti maalumu za muda au Mafuru ambaye moja ya majukumu yake ni kuchambua taarifa za Hesabu zilizokaguliwa kutoka katika taasisi na mashirika ya Umma kwa lengo la kuchunguza mwenendo wa utendaji na kushauri Serikali ipasavyo anayesema wizi hauwezekani zaidi ya jambo hilo kuwa tuhuma?

Je, tumuamini Rais Magufuli anayesema kuna uwezekano wa mtu kujinufaisha na riba au Mafuru aliyefanyakazi katika taasisi za kibenki miaka 20 na kufanyia utafiti mfumo huo ambao pamoja na kutumiwa na taasisi za umma hajawahi kushuhudia au kuwepo kwa njia za benki kumlipa mtu binafsi riba ya fedha zilizowekezwa na sekta ya umma?

Miongoni mwa hawa watatu yupo anayesema kweli na mwingine atakuwa ameingizwa mkenge au amepotoshwa kwa kutojua kwake kati ya Rais, Ndulu au Mafuru?

Nani tumuamini kati ya Mafuru anayesema kwamba utaratibu huo umekuwa ukiyapatia mashirika mengi faida, pindi fedha zinapopevuka hupata kiasi kikubwa cha fedha kutokana na riba, jambo ambalo halikuwa rahisi kwa serikali kupata faida hiyo fedha zikiwa zimekusanywa pamoja au Rais anayesema zikiwa pamoja pale BoT watu hawatapiga?

Kama kila mwanauchumi anatilia shaka uwezekano wa akaunti hiyo kutumiwa na watendaji kuiba fedha za umma kutokana na uwepo wa sheria ya fedha zinazoelekeza, kuna wakaguzi wa ndani na nje na hata CAG, hivyo upo uwezekano mkubwa wa uamuzi kufanywa kwa kukurupuka?

Inawezekana nia ya Rais Magufuli ikawa njema, lakini kama wataalamu wa uchumi wakiwemo akina Mafuru na Prof. Ndullu watakuwa wamenena sahihi kuhusu ugumu wa kuchotwa fedha katika akaunti hiyo, basi rais atakuwa ameingizwa mkenge katika uamuzi wake.

error: Content is protected !!