Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Tumthamini mwanamke, kulinda utu wake
Habari Mchanganyiko

Tumthamini mwanamke, kulinda utu wake

Spread the love

 

WAKATI leo tarehe 28 Mei 2021, dunia ikiadhimisha siku ya hedhi, bado jamii inahitaji uelewa mpana kuhusu suala zima la hedhi salama na jinsi linavyohusiana na haki za binadamu. Anaandika Jemima Samwel, DMC…(endelea).

Mataifa mbalimbali duniani huitumia tarehe 28 Mei kila mwaka, kujadili masuala yahusuyo afya ya uzazi ya wasichana, hasa hedhi salama.

Yakiamini kwamba, elimu juu ya hedhi salama huwaokoa wasichana na wanawake, hasa walio katika mazingira magumu. Kwani huwasaidia kujistiri na kuendelea na shughuli zao za kila siku, kama kuhudhuria masomo.

Juhudi hizo zimechangia kwa asilimia kubwa, wasichana hasa wa maeneo ya vijiji kukabiliana na changamoto ya hedhi isiyo salama, kwa maana ya kujistiri.

Pia, zimesaidia kupunguza tatizo la utoro shuleni, linalochangiwa na wasichana kutokwenda shule kwa kukosa taulo za kujistiri na hata kupata maumivu makali ya tumbo.

Hata hivyo, bado elimu juu ya hedhi salama inatakiwa kutolewa ili iwafikie wasichana na wanawake wengi, hususan wa vijijini.

Kufuatia umuhimu wa suala hilo, makala haya yanakusogezea taarifa mbalimbali juu ya hedhi salama na faida zake.

Hedhi ni nini ?

Ni kipindi maalumu katika mzunguko wa mwanamke mwenye umri wa kuzaa, ambacho kwa kawaida kinajirudia kila baada ya mwezi mmoja, ambapo katika kipindi hiko, mwanamke hutokwa na damu kwenye uke.

Sababu ya damu kutoka, ni yai lililokomaa kutoka nje ya mfuko wa mayai, baada ya kukosa mbegu ya mwanamume.

Na kwamba, ndani ya siku moja lnaharibika harakaharaka, kisha ngozi nyembamba ya tumbo la uzazi, iliyotanuka kwa damu ili kupokea na kulisha mimba, inajiengua na kutoa damu.

Kumbe mbegu ikikifikia yai, mimba inapatikana na kujishikiza kwenye kuta za tumbo la uzazi, ili iendelee kukua.Hapo damu haitoki na mama anaweza kujihisi mjamzito.

Mizunguko mingi ya hedhi, huwa na siku kadhaa za mwanzo ambapo mimba haiwezi kupatikana (muda wa kutoshika mimba kabla ya kudondosha yai), halafu siku ambazo mimba inaweza kutungika na kisha siku kadhaa tu kabla ya hedhi ambazo mimba haiwezi kutungika (muda wa kutoshika mimba baada ya yai kudondoshwa).

Hedhi salama nini ?

Hedhi salama ni ile ambayo inahusisha mtoto wa kike au mwanamke, kupata mahitaji yake yote muhimu akiwa kwenye siku zake za hedhi. Mahitaji hayo uhusisha taulo za kike (Pedi, maji safi na salama, pamoja na sehemu ya kubadilishia.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa, mtoto wa kike akipata hedhi salama ataweza kuondokana na matatizo mengi ya kiafya, kama vile miwasho, fangasi pamoja na magonjwa mengine na hivyo huwa hedhi yenye amani na furaha.

Suala la hedhi halipaswi kuwa kero kwa mtoto wa kike, hata hivyo imekuwa tofauti kwa watoto wengi wa kike ambao wamekuwa wakipata wasiwasi na kukosa raha pindi wanapokaribia mzunguko wao. Hii inatokana na changamoto ambazo watoto hawa wanazipitia katika kupata hedhi salama.

Jambo la kusikitisha ni kwamba, mara nyingi tumekuwa tukigusia tu masuala ya kiafya pindi tunapozungumzia hedhi salama na kusahau kuwa kukosekana kwa jambo hili kunaweza kuleta athari katika nyanja mbalimbali za maisha ya mwanamke huyu.

Baadhi ya mazingira yanayoweza kumkwamisha mtoto wa kike ni pamoja na;

Kutojihusisha katika shughuli mbalimbali za jamii kutokanaambapo mara nyingi hujitenga katika shughuli mbalimbali kama vile shule, kazi, michezo na mikutano mbalimbali. Kwani huona aibu na hofu ya kuonekana kwa watu akiwa na hali ile.

Kutojihusisha na shughuli hizo, huweza kuleta madhara makubwa kwa mtoto wa kike na yanaweza kuwa ya papo kwa papo au ya muda mrefu.

Athario nyingine ni, kukosa fursa kama mwanamke kufuatia kukaa nyumbani akiwa kwenye siku zake, kutokana na kukosa vitu vya kumsaidia kupata hedhi salama.

Hivyo, ni wazi kwamba atakosa fursa nyingi zinazoweza kujitokeza katika jamii yake, kipindi yeye akiwa katika siku zake za hedhi

Ni kwa jinsi gani hedhi salama inahusiana na haki za binadamu?

Ni wazi kuwa, kila mtu ana stahili haki za kimsingi bila kuangalia cheo , Taifa, tabaka, jinsia na dini. Anapaswa kufaidi haki zake za msingi kwa sababu yeye amezaliwa binadamu.

Kuna baadhi ya haki za binadamu ambazo mtoto wa kike atazikosa, ikiwa tu hedhi salama itakosekana.

Haki ya kuthaminiwa utu wake.

Ikiwa mwanamke atakosa nyenzo zinazoweza kumsaidia kupata hedhi salama, basi ni wazi utu wake kwa watu wengine wanaomtazama utashuka. Hasa kwa wale wasioelewa suala lake pindi watapomtazama.

Hebu fikiria maoni ya watu katika jamii yako, yatakavyokuwa pindi watakapomuona msichana akitembea nguo yake ikiwa imechafuka na damu ya hedhi.

Ni wazi katika jamii yetu hapa Tanzania, wengi watamtazama kwa kumdharau na kumkebehi na ile aibu atakayoipata itaponza utu wake.

Haki ya kupata matibabu stahiki na kuwa na afya bora.

Wanawake wanaweza kukumbwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, pindi watakoshindwa kupata nyenzo muhimu za kuwasaidia wakiwa katika siku zao za hedhi.

Wanaweza pata fangasi, miwasho, maumivu sehemu zao za siri pamoja na madhara ya kisaikolojia yanayotokana na hali ya unyonge na aibu ya kujua madhara hayo yametokana na wao kukosa vifaa muhimu vya kujisitiri vinaweza kumfanya aone aibu kwenda kwenye kituo cha afya ili kupata matibabu.

Haki ya kupata elimu.

Mtoto wa kike anaweza shindwa kupata haki yake ya kupata elimu, pindi awapo katika siku zake za hedhi. Kwa kuwa amekosa vitu vya kumsitiri kipindi kwenye hicho.

Kipindi hicho kwake huwa kigumu, kwani hushindwa kuhudhuria shule hali inayoweza pelekea matokeo mabaya na muda mwingine hata adhabu kwa walimu, wasioelewa mazingira anayopitia.

Haki ya kufanya kazi.

Kukosekana kwa vitu muhimu vya kujisitiri kwa mtoto wa kike, kunamfanya ashindwe kufanya kazi au kupoteza fursa mbalimbali za kazi.

Mwanamke atalazimika kubaki nyumbani, kwa muda wote atakaokuwa katika siku zake za hedhi na matokeo yake yanaweza kuwa ni kupoteza nafasi ya kazi au malipo aliyopaswa kupata kutokana na kazi hiyo.

Hebu fikiria wale watu wanaofanya kazi za malipo ya kila siku, ni wazi kwamba suala hili litaathiri kazi na kisha kipato chake.

Haki ya kutokubaguliwa na mtu au chombo chochote katika kutekeleza majukumu yake.

Mwanamke anaweza kubaguliwa na watu wanaomzunguka, pindi atakapokosa nyenzo muhimu za kujistiri akiwa katika siku zake.

Jaribu kufikiria wale watu ambao bado wana imani potofu kuhusu damu ya hedhi ya mwanamke, kuwa ni sumu na inaweza kusababisha mimea kukauka, chakula kuchacha, pombe kuwa chungu na kadhalika.

Anaposhuhudia damu ya hedhi ya mwanamke imesambaa kwenye nguo zake, ni wazi kuwa atamtenga na kumbagua. Na ubaguzi huo unaweza jitokeza katika shule na hata shughuli mbalimbali za jamii.

Kwa nini ni muhimu wavulana kushiriki kwenye masuala ya hedhi ?

Ni muhimu wavulana kushiriki kupata elimu ya musuala ya hedhi, kama washiriki wenza na kiini cha mabadiliko .

Katika kuadhimisha siku ya hedhi duniani , shirika la Marie Stopers Tanzania kwa kushirikiana na Lavy Limited Company, wametembelea baadhi ya shule na kutoa elimu ya masuala ya hedhi kwa wasichana.

Lakini ushirika huu utaweza kuwashika mkono wasichana, kwa kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo taulo za kike.

Wito

Kwa mashirika ya afya , mashirika ya maendeleo na taasisi mbalimbali, kuzisaidia jamii kwa namna mbalimbali katika kuhakikisha wasichana, hasa walio shuleni wanakuwa na mazingira rafiki ili wanapoingia kwenye siku zao za hedhi, wasikose mahitaji yao muhimu yatakayowasababisha kushindwa kushiriki kwenye masomo na masuala mengine ya jamii, kutokana na hedhi .

Kuliangalia suala la upunguzaji wa garama za taulo za kike, upatikanaji wa maji safi na salama katika shule , kusaidia maeneo yenye uhitaji ili wasichana waweze kupata taulo za kujisitiri kwa muda wa mwaka mzima ili wasiweze kukosa mahudhurio shuleni.

Ushauri

Kwa wasichana wanaokutana na changamoto za hedhi ikiwemo maumivu yasiyo ya kawaida, watembelee vituo vya afya vilivyo karibu nao kwa msaada zaidi.

Lakini pia wanaweza kutupigia Marie stopes bure 0800 753 333 kwa ajili ya ushauri wa masuala ya hedhi na wanaweza pia kutembelea vituo vyetu vilivyopo Dar es salaam, Zanzibar, Mwanza, Musoma, Kahama, Arusha , Iringa , Mbeya na Kimara .

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NMB yakabidhi vifaa vya ujenzi, samani kwa shule ya msingi Sinyaulime, Chuo cha FDC Morogoro

Spread the loveBENKI ya NMB imekabidhi vifaa vya ujenzi kwa shule ya...

Habari Mchanganyiko

NMB Bonge la Mpango – ‘Moto Uleule’ yazinduliwa, Milioni 180…

Spread the loveMSIMU wa tatu wa Kampeni ya kuhamasisha utamaduni wa Kuweka...

Habari Mchanganyiko

Rais Samia awataka wahariri kufanya kazi bila uoga, upendeleo

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amewataka wahariri wa vyombo...

Habari Mchanganyiko

STAMICO yasaini mkataba wa bilioni 55.2 kuchoronga miamba GGML

Spread the loveSHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limezidi kufanya vizuri katika...

error: Content is protected !!