Saturday , 13 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Tumpime kwa viwango hivi
Makala & UchambuziTangulizi

Tumpime kwa viwango hivi

Rais John Magufuli
Spread the love

KITABU cha “The Prince” kilichoandikwa na Machievelle imeelezwa kuwa, kufaulu au kutofaulu kwa mtawala yeyote hutegemea anavyoweza kuwateua wasaaidizi wake. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Ikiwa atawateua wasaidizi waaminifu na wenye uwezo wa kuchapa kazi, mtawala huyo huhesabika amefaulu hata kabla ya muda wa utawala wake kumalizika, lakini uteuzi wa wasaidizi ukiwa kinyume basi huwa na kazi ngumu mno.

Imewahi kutokea katika utawala wa Rais John Magufuli kuteua kiongozi na kisha kumwondoa kwenye mamlaka aliyomteua kwa sababu kadhaa ikiwemo kushindwa kwenda na kasi yake.

Mamlaka ya Urais ni kuunda bara za mawaziri kwa ushauri wa Waziri Mkuu lakini kulivunja baraza hilo lazima lifanywe na yeye mwenyewe. Hata anayekaimu urais hana ruhusa ya kulivunja.

Katika nchi yetu rais amepewa mamlaka kisheria hata kuwaingiza kwenye mamlaka kupitia nafasi zake za uteuzi wale walio nje ya mfumo ili kukidhi dhamira yake kwa wananchi.

Rais anaposhindwa kuteua wasaidizi wanaoweza kumfikisha katika malengo yake, mambo kadhaa hutokea ikiwa ni pamoja na kutoaminika na kuondoa imani ya wananchi katika chama cheke.

Ipo mifano katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, alipoingia madarakani alitungiwa kitabu kilichoitwa ‘Tumaini lililorejea’.

Kile wananchi walichokitarajia ni kufanyika kwa mapinduzi makubwa ya kiuendeshaji katika nyanja za utawala, siasa, uchumi na jamii, lakini sehemu kubwa ya utawala wake alioteua walikuwa wakimwangusha.

Kushindwa kwake kulisababisha wananchi wengi kuibeza serikali na CCM yenyewe, na hapo alipaswa kuketi chini kuangalia upya uteuzi wa wasaidizi wake toka mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya.

Tunafahamu kabla ya uteuzi wa viongozi, hufanyika upekuzi kuangalia anayetarajiwa kumwakilisha rais ni mwadilifu hadi ngazi za chini pia mzoefu katika shughuli za utawala na utumishi wa umma.

Kama rais mara baada ya kuwateua, angebadilika na kuwataka wasaidizi wake wawajibike ipaswavyo basi kila anapoapishwa angewapa kila mmoja hadidu za rejea kama kipimo cha mafanikio kwenye eneo anakalopewa kuliongoza. Na hiki ni kizuri kufanywa na tawala zote.

Isitoshe kuwepo na kipindi cha kufanya mapitio kwa mwaka kuona kwamba, kiongozi huyo anatekeleza yale yaliyopo kwenye hadidu za rejea.

Ingefaa rais kuwa na utaratibu wa kuwapatia anaotaka kuwateua kabla ya kuapishwa kwao, awapatie kwanza hadidu hizo na kuzisoma na anapoziafiki kuwa ana uwezo wa kuzisimamia na kuzitekeleza ndipo aapishwe.

Kuna mifano mingi mno ya viongozi wanaoteuliwa huku hawana ubunifu wa kuwaongoza wananchi kumaliza kero na kusukuma maendeleo.

Mathalani viongozi wa Mkuo wa Iringa wanashindwaje kumaliza tatizo ya madawati shuleni wakati kuna msitu wa taifa unaozalisha mbao.

Iweje watoto wanaendelea kuketi chini ya sakafu wakati ng’ambo ya barabara kuna mbao na matokeo yake wanasubiri kuanzishwa kwa kampeni ya utengenezaji wa madawati kutoka Dar es Salaam.

Wakuu wilaya kando ya bahari wanaliaje kuhusu suala la ajira kwa vijana hakuna huku wana uwezo wa kuchota maji baharini na kutengeneza mabwawa yatakayozalisha chumvi na badala yake eti kama nchi, tunakubali kununua chumvi kutoka Malindi nchini Kenya ambayo inatengenezwa kutoka kwenye bahari hiyo hiyo tena Tanzania ina eneo kubwa kuliko Kenya. Achilia mbali kazi ya uvuvi wa samaki.

Wakuu wa Wilaya wanaendeleaje kuwepo kazini leo hii wakati wakazi wake hawana vyoo huku Mkuu wa wilaya akilalamika kuwa, kuna magonjwa ya mlipuko.

Hakika naamini rais akitamka kuwa, atapeleka timu ya wakaguzi huru kwenye wilaya na mikoa kuona uwajibikaji wa viongozi aliowateua, anaweza kushangaa.

Licha ya kuhubiri ruzuku ya mbolea kutolewa kwa wakulima tangu awamu iliyopita, inawezekanaje wakuu wa wilaya na mikoa unapotembelea kandokando ya barabara iwe kuu au ya mkoa inayopita wilayani humo huoni shamba japo ekari moja imepandwa kwa mstari au kutumia mbolea.

Badala yake kiongozi mwenye dhamana hulalamika tu na kuomba msaada wa chakula kutoka ngazi ya taifa. Kuteua viongozi wanaongoja kulishwa kwa vijiko ni mzigo kwa taifa.

Utembeleapo wilayani aghalabu kusikia kwa viongozi tumeshindwa kufanya jambo kwa vile tunasubiri maagizo au fedha kutoka Makao Makuu.

Kwa shughuli ambazo zingeweza kumalizika kwa kutumia vifaa vinavyowazunguuka. Wakati mwingine uzembe kama huu hutokana na urahimu wa utawala uliopo madarakani.

Ni aibu kwa viongozi wa ngazi hizo kutokuwa na utamaduni wa ufuatiliaji wa mambo mbalimbali hadi mambo yanapoharibika au kuandikwa na vyombo vya habari.

Wateule wa rais kushindwa kujibu maswali ya utekelezaji ama shida za mwananchi mmoja mmoja na badala yake kusuburi mikutano ya rais na kumlazimu kuwanyanyua kujibu maswali yaliyoulizwa mbele yao, kunaonesha namna wanavyoshindwa kuwajibika nje ya msukumo kutoka kwa kiongozi wa juu.

Kama viongozi hawa wana majibu kwanini wangoje wananchi waulize mbele ya rais ndipo wapate majibu hayo?

Machiavelli anasema, kama wasaidizi wa mtawala watashindwa kuwa wenye uwezo na waaminifu kwa kiongozi wao, wanaweza kusababisha mtawala kushindwa kutawala.

Wasaidizi wengi wa wilaya na mikoa hutekeleza shughuli bila maandalizi wala ufuatiliaji na matokeo yake maendeleo kidogo hupatikana na hivyo huwaletea sifa mbaya wale waliowateua.

Viongozi wasiokubali ukosoaji kutoka kwa wananchi huwa ni sababu ya kudharauliwa kwa rais, kwani viongozi hao si wanaopenda kuwa karibu na watu.

Asili ya uongozi wetu inatokana na watu wenyewe, kama kiongozi hawi kinara na chachu za kumaliza kero, basi kiongozi huyo si mwadilifu.

Iwapo rais atawaita mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya waliopo na kuwauliza katika uongozi wao wameweza kumaliza kero zipi kwa kutumia ubunifu? Hawatafika robo.

Mambo mengi yanashangaza mno, ni aibu kwa mkuu wa wilaya kushindwa hata kuhamasisha wananchi kufanya usafi na taka taka matokeo wananchi kufariki kutokana na magonjwa ya uchafu.

Laini yote tisa, kumi ni je rais aliyewateua anatumia vigezo vipi? Anateuaje watu asiowajua na badaa yake mabadiliko yanafanyika mara kwa mara? Mafanikio ya yoyote ya kiongozi hupimwa katika teuzi zake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Nchimbi aanika ugonjwa wa CCM

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emanuel Nchimbi,...

Habari za SiasaTangulizi

Makonda kuanika mawaziri wanaomtukana Samia

Spread the loveMKUU Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewataka watu wanaowatuma mawakala...

Habari MchanganyikoTangulizi

Mafuriko yaua 33 Morogoro, Pwani

Spread the love  SERIKALI ya Tanzania imetoa tathmini ya athari ya mafuriko...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali yafafanua hatima ya viongozi NEC

Spread the loveWAKATI mjadala ukiibuka  juu ya hatma ya viongozi wa sasa...

error: Content is protected !!