April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Tumieni fursa zinazojitokeza-Mavunde

Spread the love

ANTONY Mavunde, Naibu Waziri Ofisi ya Rais anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, amewataka vijana kutumia vyema fursa wanazozipata ili kujiingizia kipato badala ya kukaa vijiweni. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Mbali na hilo amesema, umefika wakati wa kuondokana na dhana ya kusubiri ajira kutoka serikalili, badala yake watumie fursa mbalimbali zinazojitokeza.

Mavunde ametoa kauli hiyo leo tarehe 24 Septemba 2019, wakati wa kukabidhiwa pikipiki 30 za usambazaji bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Sh. 108 Mil kutoka Kampuni ya RoutePro na kuzikabidhi kwa vijana 30 kutoka mikoa mitano.

Amesema, serikali inatambua kuwepo kwa changamogo ya ajira kwa vijana.

“Ukosefu wa ajira kwa vijana ni moja ya changamoto inayolikabili taifa letu, ili kukabiliana nalo serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kushirikiana na wadau wanaoonesha nia ya kusaidia kubuni mipango endelevu ya kuwezesha ajira kwa vijana.

“Kama ilivyofanya Kampuni ya Route Pro, kwa kutoa mafunzo ya biashara kwa vijana wetu. Tutaendelea kutoa ushirikiano  mkubwa kufanikisha suala hili la ajira linatatuliwa,” amesema Mavunde.

Jaja Mbazila, Meneja Uratibu wa Kampuni ya Route Pro akizungumza katika zoezi hilo amesema, kampuni hiyo imepata walengwa wa kushirikiana nao katika mpango huu.

Na kwamba, ni kutokana na rekodi  ya vijana ambao imewahi kufanya nao kazi katika miradi  mbalimbali ya usambazaji bidhaa katika siku za nyuma.

“Tumelenga kuwawezesha vijana wenye bidii ya kazi na kujituma kupata fursa kuwa na biashara zao, tumefanya nao kazi kwa karibu katika miaka iliyopita na wameonesha kuwa na nia ya kufanya vizuri biashara ya usambazaji,” amesema Mbazila na kuongeza;

“Mbali na kuwapatia pikipiki, RoutePro itawapatia vijana hao kiasi cha shilingi 100,000 kila mmoja ziwasaidie kuanzia kazi.”

Amesema, baada ya miezi 24 pikipiki hizo zitakuwa mali yao kwa ajili ya kuwasaidia katika shughuli za usambazaji “ingawa watakaopenda kufanya kazi katika mpango huu wa Route Pro wa kuwezesha vijana watajiunga tena katika mpango wa miaka 2 na kupatiwa tena tena pikipiki mpya.”

error: Content is protected !!