Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Tume ya uchaguzi yasusiwa na vyama vya siasa Tanzania
Habari za SiasaTangulizi

Tume ya uchaguzi yasusiwa na vyama vya siasa Tanzania

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo
Spread the love

VYAMA vitatu vikubwa vya siasa nchini Tanzania – Chama cha Demekrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR- Mageuzi naa ACT-Wazalendo – vimegoma kushiriki hafla ya kukabidhi taarifa ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 2020. Wanaripoti Noela Shila na Mwanaharusi Abdalla, TUDARCo … (endelea).

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na vyama hivyo kwa nyakati tofauti imetaja miongoni mwa sababu za kutohudhuria hafla hiyo, ni pamoja na madai uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2020, ulivurugwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC).

“Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, haukuwa uchaguzi huru na haki. Haukuwa uchaguzi, ulikuwa ni uchafuzi wa demokrasia” na kwamba kushiriki kwao, kungekuwa ni kuhalalisha uchafuzi huo.

Hafla hiyo imeandaliwa na NEC na ripoti hiyo ya uchaguzi, imepangwa kukabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri, Samia Suluhu Hassan.

“Tumepokea mwaliko kutoka kwa mkurugenzi wa NEC, kwa ajili ya Mwenyekiti wa taifa, Katibu Mkuu na aliyekuwa mgombea wetu wa urais, kuhudhuria hafla fupi ya kukabidhi kwa Rais taarifa ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kesho Jumamosi, tarehe 21 Agosti, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Samia Suluhu Hassan

“Chama kupitia katibu mkuu, kimemjulisha mkurugenzi wa uchaguzi, mwaka 2020, hakukuwa na uchaguzi nchini Tanzania. Kulikuwa na uchafuzi mkuu, uliohusisha uporaji wa ridhaa ya wananchi, kuchagua viongozi wao na ukiukwaji mkubwa wa sheria na haki.

“Haya yametokea, kwa sababu ya kukosekana kwa uhuru wa taasisi ya kusimamia uchaguzi (NEC), ambayo ilishiriki moja kwa moja, kuharibu uchaguzi huo,” imeeleza taarifa ya Chadema, iliyosainiwa na John Mrema, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje.

idha, Chadema kimetaja sababu nyingine zinazosababisha kutohudhuria hafla hiyo, nni kile ilichoita, “kubambikiwa kesi ya ugaidi, kwa mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kutokana na chuki za kisiasa,” kuondoka nchini kwa sababu za kiusalama na kutohakikishiwa usalama wake, aliyekuwa mgombea wake urais, Tundu Lissu na NEC kushindwa kumtaja aliyesaini barua ya utambulisho wa wabunge wa Viti Maalum, waliodaiwa kutokea Chadema.

John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema

Chadema wanasema, barua hiyo ya tarehe 25 Novemba 2020, ambayo ilibeba Kumb. Na.C/HQ/ADM/20/TU/05/14, iliyosainiwa na John Mnyika, katibu mkuu wa chama hicho, kutaka kupatiwa taarifa ya aliyewasilisha majina ya wanachama wa Chadema, waliodai kuwa waliteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum kupitia chama hicho, haijabiwa mpaka sasa.

Sababu nyingine iliyotolewa na chama hicho, ni madai kuwa “kwa sasa na siku zijazo,” ajenda kuu ya chama hicho, ni kuhakikisha kunapatikana Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano, “itakayotengeneza mfumo huru na wa kidemokrasia wa uchaguzi wa nchi.

“Kushiriki katika mialiko na shughuli za Tume isiyokuwa huru, ni kuipa baraka za kisiasa na kupunguza nguvu na ari ya jitihada za kufanya mabadiliko yanayohitajika katika nchi.”

Kwa upande wake, ACT-Wazalendo kimesema, pamoja na kupokea mwaliko kutoka (NEC), kutaka kuhudhuria hafla hiyo, wamejulisha kuwa hawatashiriki.

“Uamuzi huu umefikiwa kutokana na ukweli kwamba mwaka 2020 hakukuwa na uchaguzi bali uchafuzi. Hivyo basi, chama chetu kushiriki kwenye tukio hilo, itakuwa ni sawa na kuhalalisha hujuma kubwa iliyofanyika mwaka 2020,” imeeleza taarifa ya chama hicho, iliyosaniwa na Salim Bimani, Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma.

Anasema, “uzoefu wa ripoti ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), katika uchaguzi uliyopita unaonesha kuwa, ripoti za uchaguzi za ZEC na NEC zinatumika kuhalalisha (justify) kilichotokea kwa kuandika hadaa na uzushi.”

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi

ACT- Wazalendo ambayo ni mshirika wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Visiwani na ambacho kilichotangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu uliyopita kinasema, “hivyo basi, hatutarajii kitu tofauti hapo kesho.”

Nacho chama cha NCCR- Mageuzi, katika barua yake iliyoandikwa na katibu mkuu wake, Matha Chiomba, kimeeleza kuwa hatashiriki hafla kwa kuwa kufanya hivyo, ni kinyume na dhamira yake ya kuwapo tume huru ya uchaguzi.

Anasema, “…kwa barua hii, nakutaarifu rasmi kuwa chama chetu cha NCCR- Mageuzi, hakitashiriki hafla hiyo fupi, kwa sababu ofisi yako haikutoa ushirikiano stahiki kwa maoni na malalamiko yetu wakati wa mchakato mzima wa kile kilichoitwa, ‘uchaguzi mkuu wa 2020.”

Barua ya NCCR- Mageuzi, kwenda kwa mkurugenzi wa NEC, imebeba kichwa cha maneno kisemacho, “mwaliko wa kuhudhuria hafla fupi ya kukabidhi taarifa ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.”

Barua iliandikwa tarehe 20 Agosti 2021 na kupewa Kumb. Na.NCCR-M/MM/BS/21/07 na  inamaliza kwa maneno, “pamoja na salaam ya UTU, itikadi yetu.”

Kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2020, kumeibuka malalamiko lukuki juu ya mwenendo wa chombo hicho katika kusimamia uchaguzi, madai ambayo mengi yalijikita katika dhana mzima ya upendeleo kwa chama kilichopo madarakani.

Baadhi ya viongozi wa upinzani wamekuwa wakiituhumu tume hiyo, kutokuwa huru na kufanya kazi zake kwa maelekezo ya viongozi wa CCM na serikali yake.

Hakujawahi kufanyika kikao chochote cha kutafuta maridhiano yanayolenga kuponya vidonda vya uchaguzi huo.

MwanaHALISI Online limeshindwa kumpata Prof. Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), kueleza msimamo wa chama chake juu ya kushiriki ama kutoshiriki mkutano huo.

Mara baada ya uchaguzi mkuu huo, CUF ilikuwa miongoni mwa vyama vinne ikiwemo NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo na Chadema waliotangaza kutouatambua matokeo ya uchaguzi huo.

2 Comments

  • Willson mahera ni mtu mpumbavu Sana, Jeshi la polisi wao direct wameonyesha wasiwasi kuwa wako kwa ajili ya kulinda Ccm na sii wananchi wote,, wapinzani Tanzania wao Pekee ndio wahatarishi WA amani,kufanya fujo na Kula njama za ugaidi, Wale magaidi pure waliotajwa na Sabaya ni raia wema tena serikali inaibariki matendo yao ,, lakin Wale wanaodai tume huru ya uchaguzi na katiba mpya ni magaidi,

  • Asante sana vyam vitatu vya upizani visuvojua nini maana ya upizani isipokuwa na vipongeza kwakuwa wanaelewwa ccm kuwa ndio chama bora na ndio chama wananchi wanakimini na ndio chama chenye uwezo wa kutongoza. Watazania hawatakubari kuongozwa na vyama visivo weza kujiongoza ndani ya vyama vyao. Idadi kubwa ya watanzania wanatambua uchunguzi e
    Wa 2o 20.nihalali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!