January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tume ya Nyanduga yaingilia mgogoro wa Z’bar

Spread the love

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUU) inafanya utafiti wa dharura wa mgogoro wa kisiasa ulioanza upya Zanzibar kufuatia hatua isiyotarajiwa ya kufutwa uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, na itatoa ripoti yake “siku chache zijazo.” Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Mwenyekiti wa Tume hiyo, mwanasheria Bahame Nyanduga amesema mjini hapa leo, kwamba wameshakutana na wadau mbalimbali walioshiriki uchaguzi huo wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa.

Nyanduga ambaye amewasili hapa kutoka makao makuu ya tume jijini Dar es Salaam, amesema walikutana na viongozi wa vyama vya siasa mapema leo kabla ya kukutana na waandishi wa habari kwenye ofisi kuu za tume hiyo, mtaa wa Mbweni, nje kidogo ya mji.

Amesema wamefanikiwa kukutana na Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Uchaguzi Zanzibar – Zanzibar Electoral Commission (ZEC), Salum Kassim Ali lakini hawajapata kukutana na makamishna wa tume hiyo.

Pia amesema miongoni mwa watu muhimu waliokutana nao na kufanya majadiliano yanayolenga kupata kujua kwa undani kuhusu kilichotokea katika uchaguzi, ni mashirika yasiyo ya kiserikali (AZAKI), zikiwemo jumuiya za wanasheria hapa.

Mwandishi wa habari hizi alimuuliza Nyanduga kama ujumbe wake wamefanikiwa kukutana na Dk. Ali Mohamed Shein na Maalim Seif Shariff Hamad, wagombea washindani wakuu katika uchaguzi huo, alishikilia tu kwamba wamekutana na viongozi wa vyama vya siasa.

“Nimesema tumekutana na vyama vya siasa. Tumezungumza na viongozi wao kwa sababu wote wanawakilishwa,” amesema bila ya kusema moja kwa moja kama wamekutana na viongozi hao.

Wanasiasa hao ndio walio katikati ya mgogoro huu uliochochewa na Mwenyekiti Jecha: Dk. Shein chama chake CCM kimemshinikiza Jecha kufuta uchaguzi wakati Maalim Seif alishatoa indhari tarehe 26 Oktoba, kuwa kura zake zilikuwa zinaelekea kumpatia ushindi wa asilimia 52.87 wakati huo Jecha mwenyewe akiwa ameshatangaza matokeo ya urais kwa majimbo 31, kati ya majimbo 54 yote ya Zanzibar.

Nyanduga amesema mbali na kukusanya taarifa mbalimbali zitakazowawezesha tume kutoa mapendekezo ya kutoka kwenye mkwamo, pia ujumbe wao unaangalia masuala yanayohusu hali ya haki za binadamu kwa sababu yapo yanayotendeka na kuonekana ni mambo ya uvunjaji wa haki za watu kipindi hichi.

“Kwa hivyo tunayo nafasi pia ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu matendo mabaya waliyotendewa ambayo yanaashiria kuvunjiwa haki zao kibinaadamu… huwa tunachukua yale ambayo hayakushughulikiwa inavyotakiwa na vyombo vya serikali kwa mujibu wa sheria,” amesema Nyanduga.

Tume ya Haki za Binadaamu na Utawala Bora ambayo ni asasi huru ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatoa elimu ya masuala ya haki za binadamu na utawala bora na kufuatilia matukio yanayoashiria kugusa maeneo hayo mawili.

Hata hivyo, pamoja na kuitwa tume huru, haina uwezo wa kumfungulia mtu yeyote awae mashitaka ya jinai bali inachokifanya ni kuchunguza kwa kutumia wachunguzi wake na kuandika ripoti yenye mapendekezo ya kutekelezwa na serikali.

Baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kutoa tangazo la kufuta uchaguzi tarehe 28 Oktoba, Tume hiyo ilitoa taarifa ya awali ikitofautiana naye kwa kusema hana mamlaka ya kufanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 11 ya Mwaka 1984.

Katika taarifa yao, walimtaka Jecha “atafakari upya” tangazo lake na kuchukua hatua ifaayo ili kuiepusha Zanzibar na hatari ya kutumbukia kwenye mgogoro unaohusu uchaguzi mkuu.

Nyanduga amesema kwa kuzingatia sheria hiyo ya uchaguzi, Jecha na hata Maalim Seif walikosea kisheria.

Tume pia imejizuia kutoa msimamo kuhusu ubishani unaoendelea sasa kuhusiana na kama ni kweli Zanzibar kwa sasa haina rais halali kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984. Nyanduga amesema eneo hilo pia watalitolea pendekezo katika ripoti yao kwa kuwa lina ubishani na isingekuwa vema kulitolea uamuzi sasa.

Kuna mtizamo wa wanasheria kupitia Chama cha Wanasheria wa Zanzibar – Zanzibar Lawyers Society (ZLS), imeelezwa kuwa Zanzibar ina pengo la urais kwa sababu “muda wa rais aliyepo ulimalizika rasmi Novemba 2.”

Novemba 2, mwaka 2010, ndiyo siku ambayo Dk. Shein aliapishwa kushika wadhifa huo, na kwamba ilitakiwa aapishwe kiongongozi wa kumrithi kabla ya kupita hapo ambapo miaka mitano ya uongozi wake inahesabiwa kukoma.

Hata hivyo, Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, ilisema uchambuzi huo si sahihi,

Kwa kuwa Katiba kupitia kufungu cha Kwanza (a) katika Ibara ya 28, inaelekeza kuwa “Mtu ataendelea kuwa Rais mpaka: (a) Rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais.”

Dhana hii inapingwa na wanasheria wa ZLS wanaosema inazingatia kama rais aliyekuwepo (b) amefariki (c) amejiuzulu (d) amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; au (e) kwa sababu yoyote nyengine ameacha kuwa kiongozi kwa mujibu wa vifungu vyengine vya Katiba hii.”

Wanasheria hao wanasema panapohusu jambo lililotokea, kizingatiwe kifungu (2) cha Ibara hiyo ya 28 kinachosema, “Kufuatana na maelezo ya kijifungu (1) cha kifungu hiki, Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe, ambapo:

(a) Kama yeye ni mtu ambaye ndiye mara ya kwanza amechaguliwa kuwa Rais chini ya Katiba hii alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais; na

(b) Kwa sababu nyenginezo mtu wa mwisho kushika madaraka hayo kwa Katiba hii alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais, au pasingelikuwa na sababu ya kifo chake, basi angalikula kiapo.”

Tume ya Haki za Binadaamu na Utawala Bora inafanya utafiti wake huku jitihada mbalimbali zikiendelea kufanywa na watu mashuhuri chini ya Umoja wa Mataifa, zikiwa hazijafunuliwa hasa zilipofikia. Inajulikana kuwa Maalim Seif alikutana na Rais Jakaya Kikwete jana Ikulu ya Dar es Salaam. Hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na yeyote mpaka sasa.

error: Content is protected !!