October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tume Huru ya Uchaguzi yamtesa Dk. Bashiru

Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM

Spread the love

MADAI ya Tume Huru ya Uchgauzi yanayotolewa na wanasiasa wa vyama vya upinzani nchini, yanakinzana na mtazamo wa Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM). Anaripoti Martin Kamote … (endelea).

Dk. Bashiri ametoa kauli hiyo leo tarehe 27 Novemba 2019 , wakati akizungumza na kipindi cha Konani kinachorushwa na televisheni ya mtandaoni ya ITV. amesema, tume inayoridhisha kila mtu, siyo tume huru, bali ni tume holela.

Amewanyooshea kidole wanasiasa wa vyama vya upinzani kwamba wanakosea pale wanapodhani, tume inakuwa huru pale tu inapowatangaza kuwa washindi katika uchaguzi.

 “Tatizo kwenye nchi za Afrika ni kwamba, wanasiasa wanadhani tume inakuwa huru inapowatangaza kwamba wameshinda. Ukiwa na tume inayotaka kuridhisha kila mmoja, na kutangaza kila anayetaka kutangazwa kuwa mshindi, haitakuwa tume tena, itakuwa ni uholela ule ule,” ameeleza Dk. Bashiru.

Amesema, Tume Huru haihusishi wanasiasa, haitegemei  msaada wa kifedha kutoka mataifa ya nje,  bali inaundwa na wenye taaluma pamoja na uzoefu kuhusu masuala ya uchaguzi.

“Mimi kwa tafisiri yangu, ni tume ambayo haihusishi wanasiasa. Iundwe na watu ambao kwa rekodi yao, kwa taaluma zao kwa uzoefu wao,  wanaweza wakatoa huduma ya kusimamia uchaguzi kwa misingi ya haki. Sifa ya pili ni tume yenye uwezo wa kiutendaji, watalaamu wenye mafunzo,” amefafanua Dk. Bashiru na kuongeza;

“Na watendaji waendeshe uchaguzi kwa ufanisi, watangaze matokeo kwa wakati, watoe elimu kwa ufanisi, wawe na fedha ambazo chanzo chake ni serikali husika na si wafadhali, tume nyingi za Afrika ukiona tume inaanza kuwa tegemezi inakuwa si uhuru.”

Dk. Bashiru amedai vyama vya siasa vya upinzani havina misingi ya demokrasia, na kwamba vikiruhusiwa kujihusisha na masuala ya tume, vitapeleka ugomvi kwenye tume.

“Kama vyama havina utamaduni wa demokrasia, lakini vinataka visimamiwe na tume, vitapeleka ugomvi kwenye tume huru, lakini itawezekana kama vyama vya siasa vina utamaduni wa demokrasia katika vyama  vyao,” amesisitiza Dk. Bashiru.

error: Content is protected !!