July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Tumbili’ amtimua ‘Mwizi’

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulula

Spread the love

MWANASHERIA Mkuu aliyeitwa “mwizi” bungeni amejiuzulu. Ni Jaji Fredrick Werema, mwenye hasira fupi na msamiati finyu; na hivyo kuvimba fundo haraka kooni.

Anatarajiwa kufuatiwa na mawaziri waliotajwa katika kashfa ya uchotaji fedha kutoka Akaunti ya Escrow na hivyo kutoa nafasi kwa rais kuunda baraza jipya la mawaziri wakati wowote sasa.

Taarifa kutoka vyanzo vya ndani ya serikali zinasema, karibu mawaziri watano wapya watateuliwa kujaza nafasi zitakazoachwa wazi; wengine kuhamishwa na baadhi ya naibu mawaziri kupanda ngazi.

Mwanahalisi Online limeshindwa kupata majina ya mawaziri wapya, ingawa limedokezwa kuwa miongoni mwa wanaotarajiwa kupanda kutoka naibu mawaziri, ni January Makamba na Mwigullu Nchemba.

Habari zinasema, rais alitarajiwa kuhutubia taifa jana kwa kutumia mkutano wake na wazee wa jiji la Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee.

Ofisi ya Rais ilitangaza juzi Jumanne kuwa Werema ameandika barua kwa Rais Jakaya Kikwete kuomba kuachia ngazi na kwamba rais amekubali ombi lake.

Katika barua yake kwa Rais Kikwete, Jaji Werema amesema, ameomba kujiuzulu kwa kuwa ushauri wake kuhusu uchotaji wa fedha katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta, “hakueleweka na umechafua hali ya hewa.”

Werema alipata wakati mgumu bungeni pale David Kafulila, mbunge wa NCCR-Mageuzi (Kigoma Kusini), alipomg’ang’ania kuwa alihusika katika uchotaji fedha za Escrow.

Akiwa kwenye kilele cha hasira, Werema alimwita Kafulila kuwa ni “tumbili.” Naye Kafulila akajibu kuwa Werema ni “mwizi.”

Sasa historia imeandikwa; “tumbiri” amemfukuza “mwizi.”

Werema alijiuzulu juzi Jumanne. Kujiuzulu kwake kunatokana na kuwapo shinikizo kutoka ndani na nje ya Bunge, kuhusu kashfa ya ukwapuaji Sh. 321 bilioni kutoka Akaunti ya Escrow.

Bunge, baada ya kupokea Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) liliagiza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuchambua ripoti hiyo na kuja na mapendekezo juu ya ukwapuzi.

Katika mkutano wake pacha wa 16 na 17 uliomalizika mjini Dodoma wiki tatu zilizopita, Bunge lilijadili mapendekezo ya PAC, kutoa maazimio manane na kuitaka serikali kuyatekeleza; yakiwa ni pamoja na kuwawajibisha baadhi ya mawaziri.

Miongoni mwa maazimio ya Bunge ni lile lililomtaka rais kutengua uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, waziri wa nishati na madini Profesa Sospeter Muhongo na katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.

Sakata la ukwapuaji wa zaidi ya Sh. 321 bilioni, ndani ya Benki Kuu ya Taifa (BoT), lilianza kushikiwa bango na David Kafulila ambaye alimwandama moja kwa moja mwanasheria mkuu.

Taarifa za kibenki na kutoka serikalini zinaonyesha mabilioni hayo ya shilingi yalikwapuliwa BoT kati ya Novemba na Desemba 2013. Werema ndiye alishauri serikali kutoa fedha hizo na bila kulipiwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Uchotaji ulifanywa baada ya James Rugemalira, mmoja wa wamiliki wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), kufuta mashauri mawili ya madai aliyokuwa amefungua mahakama kuu juu ya mgogoro na mwanahisa mwenzake.

Kampuni ya Rugemalira, VIP Engineering & Marketing Limited (VIP-EM), ikiwa na hisa asilimia 30, ndiyo ilikuwa na ubia na kampuni ya Mechmar ya Malaysia (asilimia 70) katika kumiliki IPTL.

Rugemalira aliondoa mashauri mahakamani tarehe 5 Septemba 2013. Mashauri hayo ni Na. 49/2002 na 254/2003 kutokana na kile kinachoitwa na serikali, “makubaliano ya mauzo ya hisa za kampuni ya VIP EM Limited kwa Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP).”

Jaji Werema alipoona Kafulila anamzidi kwa hoja, aliamua kumwita “tumbili.” Naye Kafulila alimjibu Werema kwa kumwita “mwizi;” jambo ambalo liliibua mshikemshike bungeni.

Katika majibizano makali na joto la kuzima ndimi za moto wa Escrow, Prof. Muhongo alimwambia Kafulila kuwa ushahidi wa makatarasi alionao, “ukafungie maandazi.”

Hata hivyo, wiki tatu baada ya Bunge kufungasha virango, Werema amekubali kuachia ngazi.

Tangu kutolewa kwa maazimio ya Bunge, ikulu imekuwa ikitoa kauli zinazokinzana. Kauli ya kwanza ilitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

Alisema Rais Kikwete hawezi kuchukua hatua kwa sasa dhidi ya watuhumiwa hadi uchunguzi wa kashfa hiyo ukamilike.

Sefue alisema, tayari rais ameagiza vyombo vya uchunguzi kufanya kazi ya uchunguzi na kwamba ripoti yake itatolewa hadharani na hapo ndipo hatua zitachukuliwa. Alisema ripoti ya uchunguzi ndiyo itakayompatia undani wa suala hilo.

Taarifa ya pili ya Ikulu kuhusu kashfa hiyo ilitolewa na Kurugenzi ya Mawasilino ya Rais. Ilisema, Rais Kikwete amepokea ripoti, nyaraka na ushauri wa Bunge kuhusu kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow na ataifanyia maamuzi wiki moja kutoka sasa.”

Hii ilikuwa wiki moja baada ya Bunge kutoa maazimio yake.

Kwa mujibu wa kurugenzi ya rais, kiongozi huyo wa nchi ameagiza ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iwekwe hadharani kwa ajili ya umma kuisoma na kujua nini hasa kimesemwa na kupendekezwa.

Ripoti ya CAG ambayo ilitumiwa na PAC kufanyia uchambuzi, iko wazi na tayari imewekwa kwenye mitandao ya kijamii. Inasomwa na imeeleweka kwa wananchi wengi.

Rais amesema anaelekeza vyombo vya dola kufanya uchunguzi wakati uchunguzi tayari umefanyika.

Aidha, Kikwete anayeonekana mzito katika hili la Escrow, ndiye aliridhia kujiuzulu kwa waziri wa maliasili na utalii, Balozi Khamisi Kagasheki.

Akawa mwepesi kuwafuta kazi mawaziri wengine watatu, Emmanuel Nchimbi, Shamsi Vuai Nahodha na David Mathayo.

Hii ilikuwa muda mfupi baada ya Bunge kupokea ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira. Mawaziri wote wanne, walituhumiwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili.

Haijfahamika kwanini rais anaonekana kuwa na kigugumizi kutekeleza kilichoagizwa na bunge.

Bali mtoto wake, mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa hakuna waziri hata mmoja atakayejiuzulu.

error: Content is protected !!